2834; Mwache akuambie mwenyewe.
Huwa tunajikatalia mambo mengi sisi wenyewe kuliko tunavyokataliwa na wengine.
Ninachoweza kusema kwa uhakika ni kwamba yale hapana za watu ambazo umekuwa unajipa wewe mwenyewe ni nyingi kuliko hapana unazosikia kweli kutoka kwa watu.
Yaani majibu unayojipa kwamba watu watakataa kitu fulani kama utawaambia ni mengi kuliko yale ambayo watu wanakupa kwa uhalisia.
Tukienda kwenye mfano zaidi, kama kuna kitu unauza na kuna mtu unaona anaweza kuwa mteja, ila ukajiambia hatakubali kununua, majibu ambayo umejipa kwa aina hiyo ni mengi kuliko uhalisia.
Kwa kuwa mtu bado hajakubaliana na wewe, kwa sababu hujawambia, acha kujiambia wewe mwenyewe na taka kusikia kutoka kwao wenyewe.
Kama unajiambia mtu hatakubali, sawa, sasa muulize ili umsikie yeye mwenyewe akikujibu hivyo.
Ya nini umlishe mtu maneno ili hali anaweza kuongea mwenyewe?
Wewe uliza, ukitegemea atasema hapana. Na ukiuliza wengi zaidi, kuna ambao watasema ndiyo.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapojiambia mtu hatakubali kitu ni sawa. Sasa hakikisha unamsikia yeye mwenyewe akikikataa. Tofauti na hapo inakuwa ni uzushi wako mwenyewe. Na uzushi siyo mzuri.
Kama kuna kitu unataka kuuliza, uliza. Kama kuna kitu unataka kuomba, omba. Usijipe majibu mwenyewe, wacha watu wakupe majibu yao.
Tafakari;
Ukirusha matope mengi kwenye ukuta, kuna baadhi yatanasa. Kadhalika ukiwauliza/kuwaomba wengi unaojiambia hawatakubali, kuna baadhi ambao watakubali.
Wewe tekeleza sehemu yako na uwaache wengine watekeleze sehemu zao pia.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed