#SheriaYaLeo (340/366); Zamisha akili yako kwenye wakati uliopo.

Kutokutulia kwa akili zetu imekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kukosa umakini na kufanya makosa ambayo yanatugharimu sana.

Kwa asili, akili yetu haiwezi kutulia sehemu moja, huwa inahama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Akili zetu ni rahisi sana kuhamishwa na usumbufu unaokuwa unaendelea kwenye mazingira yetu.

Ili kuweza kuondokana na hilo la akili kuzurura na kupunguza umakini wetu, tunapaswa kuzamisha akili yetu kwenye wakati uliopo.

Hilo linafanyika kwa tahajudi, ambalo ni zoezi la kuyaweka mawazo yako kwenye kitu kimoja bila kuruhusu yazurure.
Zoezi hili linatuliza akili na kuongeza umakini kwenye kila jambo, kitu kinachopunguza sana makosa tunayofanya.

Unapaswa kutenga muda wa kufanya zoezi hili kila siku, kutenga muda ambao utaelekeza mawazo yako kwenye kitu kimoja bila kuruhusu yazurure.
Zoezi hilo lina nguvu kubwa ya kukupa utulivu wa kiakili na kukuongezea umakini.

Mwanzoni zoezi hilo linakuwa gumu, kwa sababu akili ilishazoea kuzurura bila kudhibitiwa.
Lakini unapolifanya bila kuacha, unaanza kupata udhibiti wa akili na kuweza kuiweka kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu.

Sheria ya leo; Hatua ya juu kabisa unayoweza kufikia kwenye kufanya jambo lolote lile ni pale unapoweza kudhibiti fikra zako na kuzamisha akili yako kwenye wakati uliopo. Kila siku fanya zoezi la kuzamisha akili yako kwenye wakati uliopo ili upate ulituvu wa kifikra na kuongeza umakini wako.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji