#SheriaYaLeo (341/366); Muda hai au muda mfu?

Muda ambao upo hai ndiyo kitu pekee unachokimiliki. Vitu vingine vyote ulivyonavyo unaweza kuvipoteza – familia yako, nyumba, magari, kazi na hata biashara.
Muda ambao upo hai ndiyo kitu pekee kilicho ndani ya udhibiti wako.

Jinsi ya kutumia muda wako, ni maamuzi yako mwenyewe.
Unaweza kuufanya kuwa muda wako kwa kufanya yale yenye tija kwako.
Au unaweza kugawa muda huo kwenye mambo yasiyokuwa na tija.

Unaweza kutumia muda wako kuwafanyia watu wengine kazi, wanaumiliki muda wako na kuchukua udhibiti wako.
Unaweza kutumia muda wako kuhangaika na starehe mbalimbali na kugeuka kuwa mtumwa wa hisia zako.

Au unaweza kumiliki muda wako, kwa kuutumia kwenye mambo yako, mambo yenye tija na yanayokufikisha kule unakotaka kufika.
Hapa ndipo muda unakuwa chini ya udhibiti wako na kuweza kuleta matokeo bora kwako.

Ili uweze kuwa na maisha bora, unapaswa kuwa na umiliki mkubwa wa muda wako na kuutumia kufanya mambo yenye tija kwako na siyo kudhibitiwa na wengine au kuendeshwa na hisia.

Sheria ya leo; Kamwe usipoteze muda wako. Miliki kila muda wa siku yako kwa kuutumia kwa tija. Haijalishi uko wapi, iwe kwenye foleni, unaumwa kitandani, upo kwenye kazi ya muda mrefu, hakikisha unakuwa na udhibiti wa muda wako kwa kuutumia kwenye mambo yenye tija.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji