2838; Ukishapotea, ni vigumu sana kurudi.
Kama umeshawahi kwenda mahali usipopajua kwa kufuata ramani ya kwenye simu (google map), unajua jinsi ambavyo unaweza kuwa unazunguka mahali pamoja kwa muda mrefu bila kujua.
Hiyo ni kwa sababu ramani hizo zina udhaifu mmoja, kama imekuelekeza ukifika mbele kata kulia, halafu hukukata hapo kulia, ukawa umepitiliza, haitakuambia rudi nyuma, bali itaangalia njia nyingine ya mbele na kukuelekeza.
Hivyo unaweza kupapita unapoelekea na kwenda kuzunguka sana mpaka tena kuja kurudi.
Hivyo pia ndivyo maisha yetu yalivyo, mara nyingi huwa tunaenda sawa, mpaka pale kitu kinapoharibika au tunapopotea. Baada ya hapo inakuwa vigumu sana kurudi kwenye hali zetu za awali.
Nimekuwa naliona hili kwa watu wengi mno. Mtu tayari alikuwa na tabia ya kuandika kila siku, anapitia changamoto fulani inayomzuia asiweze kufanya hivyo kwa siku kadhaa. Lakini hata baada ya changamoto hiyo kupita, bado anashindwa kurudi kwenye hali ya kuandika kila siku.
Kadhalika kwenye mambo mengine kama kuwahi kuamka, kufanya mazoezi, nidhamu kwenye kazi, biashara, fedha na mengineyo.
Unakuwa unaenda vizuri sana pale kila kitu kinapokuwa sawa, mpaka pale mambo yanapobadilika ndipo unapotea kabisa na hurudi tena kwenye mstari wako sahihi.
Kuhakikisha hili haliwi kikwazo kwako unapaswa kula kiapo na wewe mwenyewe kwamba utakaa kwenye njia sahihi kwa maisha yako yote. Hata kama utakutana na ugumu kiasi gani, kama tu upo hai, hutaacha kufanya kile ulichopanga kufanya.
Hata kama unaumwa na umelazwa kitandani, hakikisha umefanya ulichopanga kufanya, kwa namna yoyote ile.
Ni kwa nidhamu hii kali kabisa ya kuamua na kufanya ndiyo utaweza kubaki kwenye njia sahihi kwako.
Na pale kila kitu kinapokuwa nje ya uwezo wako kabisa na ukashindwa kabisa kufanya, basi hilo lililokuzuia linapoondoka, mara moja unarudi kwenye njia yako.
Usikubali kabisa kuacha njia yako uliyochagua, rudi kwenye njia hiyo na kaa ndani yake kwa msimamo bila kuacha.
Hatua ya kuchukua;
Kuwa na nidhamu kali ya kuamua na kufanya bila kuacha. Hata kama dunia inawaka moto, usiache kufanya kama ulivyopanga kufanya. Chagua machache ya msingi kwako ambayo lazima uwe unayafanya na fia kwenye hayo.
Tafakari;
Ni rahisi kuendelea kufanya kitu kuliko kuanza kufanya. Hivyo ukishaamua utakachofanya, ng’ang’ana kubaki kwenye kufanya kuliko kuacha. Maana ukishaacha, ni vigumu sana kuja kuanza tena kufanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed