2840; Hatupendi mambo magumu.

Kitu kimoja kuhusu sisi binadamu ni hiki, huwa hatupendi mambo magumu.
Huwa tunapenda mambo rahisi kuyaelewa na kufanyia kazi.

Na ndiyo maana matapeli huwa wana ushawishi mkubwa kwa watu. Kwa sababu huwa wanaelezea mambo kwa urahisi kabisa ambao mtu anaelewa.

Ndiyo maana pia mambo yanayohusu burudani na starehe yanapata wafuasi wengi. Kwa sababu ni rahisi kueleweka na kufanyia kazi.

Chochote kigumu, kinachomtaka mtu afikiri kwa kina na kufanya maamuzi, kinawapoteza watu.

Chochote unachofanya kuwalenga watu, kifanye kuwa rahisi sana kueleweka na kufanyiwa kazi.
Waondolee watu uhitaji wa kufikiri na kufanya mazoezi.
Ifanye iwe kuchukua hatua kwao ni moja kwa moja.

Mafanikio yako yanategemea sana ushawishi wako kwa watu wengi.
Ili uweze kuwashawishi wengi, lazima ufanye kitu kuwa rahisi kabisa.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, angalia jinsi ya kukirahisisha kwa namna ambayo mtoto wa darasa la tano anaweza kuelewa na kujua nini anapaswa kufanya.

Tafakari;
Kwenye mfumo wa elimu tumefundishwa kuyafanya mambo kuwa magumu. Lakini kwenye ulimwengu wa kawaida, urahisi ndiyo unaoeleweka na kukubalika.
Chochote unachofanya, kirahisishe sana ili uweze kuwa na ushawishi kwa wengi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed