#SheriaYaLeo (344/366); Vuka ubinadamu na fikia uwezo usio na ukomo.

Mara nyingi tunaishi kwenye hali ya ubinadamu ambayo huwa ina ukomo mkubwa.
Tunakuwa tumezama kwenye mazoea yetu ya kila siku, ambayo yanatuzuia kufikia uwezo usio na ukomo wa ulimwengu.

Wapo wanaojaribu kuondoka kwenye hali hiyo, lakini bado hawafanikiwi kwa sababu hawafanyi kwa usahihi.
Wanaojaribu kufanya hivyo husafiri na kwenda nyikani, lakini wanajikuta wamebeba teknolojia mbalimbali na bado wana mawazo yale yale wanayokuwa nayo kila siku.

Kama kweli unataka kuondoka kwenye ukomo wa ubinadamu na kufikia uwezo usio na ukomo wa ulimwengu, unapaswa kufanya yafuatayo;

Moja ni kutembelea maeneo ambayo hayana watu na wala hakuna vitu vinavyowahusu watu. Unahitaji kutembelea maeneo ambayo hayakukumbushi chochote kuhusu ubinadamu.

Mbili hupaswi kuambatana na teknolojia yoyote ile. Unapaswa kukabiliana na kila kitu kama kilivyo badala ya kutegemea teknolojia kurahisisha mambo.

Tatu achana na mawazo yako yote ya nyuma, nenda ukiwa na fikra tupu ili kuangalia mambo kwa jinsi yalivyo badala ya kuyaangalia kwa fikra unazokuwa nazo wewe.

Kwa kuzingatia hayo matatu, utaweza kuvuka hali ya ubinadamu na kuuona ukuu wa ulimwengu usio na ukomo.
Unaporudi kwenye hali ya ubinadamu, unajionea wazi tofauti kubwa kwenye hali hizo mbili.

Sheria ya leo; Ondoka kwenye mazoea ya kibinadamu na ingia kwenye uwezo mkubwa wa ulimwengu usio na ukomo ili uweze kuona jinsi mambo makubwa yanavyowezekana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji