2846; Cheza kamari kwako mwenyewe.

‘Kila kitu kwenye maisha ni kamari….’
Ni kauli wanayopenda kuitumia wale wanaocheza kamari mbalimbali kwa kutegemea kupata matokeo makubwa bila kufanya kazi.

Ni kweli kwamba kila kitu kwenye maisha ni kamari, kwa sababu hakuna kitu chochote ambacho kina uhakika wa asilimia 100.

Kwa chochote tunachofanya kwenye maisha, kuna nafasi ya kupata na kukosa, kushinda na kushindwa.
Hiyo ndiyo kamari yenyewe.

Wanapokosea watu ni pale wanapocheza kamari kwa wengine, kuweka mategemeo yao kwa wengine ndiyo wawape matokeo.
Mfano unaweka fedha zako kwa mtu, ukitegemea akupe faida kubwa.
Hiyo ni kamari hatari na nafasi ya kushindwa ni karibu na asilimia 100. Yaani unaweza kuwa na uhakika wa kushindwa zaidi kuliko kushinda.

Kamari pekee unayopaswa kucheza kwenye maisha yako, ni kwako wewe mwenyewe.
Jichezee kamari wewe mwenyewe.
Jitegemee wewe mwenyewe katika kupambana na kuleta matokeo unayoyapata.
Hata kama utashindwa, angalau unajua kuna juhudi kubwa ambazo umeweka.
Na kama utarudia tena kufanya, utakuwa bora kuliko awali.

Kwa mfano, kama una kiasi fulani cha fedha, halafu mtu akakuambia ana njia ya kuzalisha fedha haraka, ukiweka fedha hiyo kwake unapata faida kubwa, hapo ni kucheza kamari kwa wengine na nafasi ya kushindwa ni kubwa sana.

Lakini kama utachukua kiasi hicho hicho na kuanzisha biashara, ambayo utaisimamia mwenyewe na kuweka juhudi zote katika kuijenga na kuikuza, unakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa.
Na hata kama utashindwa, utakuwa umejifunza mengi ambayo wakati mwingine utakuwa bora zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Kama kuna hatua za hatari unachukua kwenye kitu chochote, hakikisha wewe mwenyewe una udhibiti mkubwa kwenye kitu hicho. Tofauti na hapo unakuwa umejiandaa kushindwa, kitu ambacho hakina manufaa yoyote kwako, maana hutapata hata nafasi ya kujifunza.

Tafakari;
Cheza kamari kwako mwenyewe ili kuwa na udhibiti mkubwa huku pia ukijiimarisha na kuwa bora zaidi kwenye kuchukua hatua za hatari. Kamwe usiweke matumaini yako kwa watu wengine, bali hakikisha una udhibiti kwenye kila kitu kinachokuhusu moja kwa moja.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed