2849; Watu na matokeo.

Kama kiongozi, una mambo hayo makubwa mawili ya kuzingatia.
Una watu unaowaongoza na kuwasimamia na una matokeo ambayo unapaswa kuyazalisha.

Haya mawili yanakwenda pamoja kwa sababu ni watu ndiyo wanaozalisha matokeo unayoyataka.
Na hapo ndipo penye mtego mkubwa kwenye uongozi, kwa sababu unahitaji mlinganyo mzuri sana kwenye hayo mawili.

Kuwa na mlinganyo sahihi kwenye hayo mawili ni zoezi gumu na linalowashinda viongozi wengi. Na hiyo ndiyo sababu ya viongozi wengi kushindwa.

Ni rahisi kiongozi kuegemea kwenye eneo moja na kupuuza jingine. Anaweza kupata matokeo mazuri kwa muda mfupi, lakini kwa muda mrefu anaishia kupoteza.

Kiongozi anayeegemea kwa watu anakuwa na huruma na kuwajali sana watu. Watu wanampenda na kumwona ni kiongozi mzuri.
Lakini anashindwa kuzalisha matokeo. Kwa sababu watu kwa asili ni wavivu na wazembe, hivyo wakiendekezwa, hakuna kinachofanyika.

Kiongozi anayeegemea kwenye matokeo anaangalia tu ni matokeo gani anapata bila kujali hali ya watu. Kiongozi huyu atawasukuma watu kuzalisha matokeo bila kujali hali zao. Hilo litampa kiongozi matokeo mazuri, lakini mahusiano yake na watu yanakuwa siyo mazuri na anakuwa anawapoteza kwa wingi.

Kiongozi bora ni yule anayekuwa na mlinganyo, anayejali kuhusu watu, huku akihakikisha matokeo yanapatikana.
Hivyo anaanza kwa kuhakikisha anawajenga watu bora, kisha anawasaidia watu hao kupata matokeo mazuri.
Hili linahitaji kazi zaidi kwa upande wa kiongozi, lakini matokeo yake ni mazuri.
Kwani watu wanakuwa vizuri huku matokeo yakizalishwa.

Njia ya kiongozi kufanya hayo ni kwa malengo, sifa na maboresho; rejea ukurasa wa 2848.

Kuna wakati watu wanakuwa siyo sahihi, licha ya kujaliwa na kusaidiwa wazalishe matokeo, bado wanakuwa hata hawajisumbui.
Na hapo kiongozi anakuwa anajua hao ni watu ambao hawezi kwenda nao.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini leo wewe ni kiongozi wa aina gani. Je unajali zaidi watu, wanakupenda ila hupati matokeo, au unapata matokeo lakini huna mahusiano mazuri na watu wako?
Chukua hatua leo ya kuwa kiongozi bora kwa kuzingatia yote mawili. Wajue watu wako na shirikiana nao vizuri kuzalisha matokeo bora.

Tafakari;
Kiongozi ukitaka upendwe na kila mtu, hutazalisha matokeo yoyote, maana watu watatumia udhaifu wako kutokufanya wanayopaswa kufanya.
Na pia ukitaka kupata matokeo unayotaka bila kujali kingine chochote, utapoteza watu wengi.
Unahitaji kuwa na mlinganyo sahihi, kitu ambacho ni kigumu sana, lakini kinawezekana kama utaweka kazi.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed