2852; Kuwa mtumwa wa tabia nzuri.
Tulipokuwa watoto, tulikuwa watumwa wa hisia.
Tuliendeshwa na hisia na kila mara kufanya yale tuliyojisikia kufanya.
Tumekuwa watu wazima na sasa tumekuwa watumwa wa tabia.
Tumejenga tabia na sasa tabia zinatujenga.
Mambo mengi tunayofanya tunayafanya kwa tabia, kwa jinsi ambavyo tumezoea kufanya.
Ubaya wa tabia ni kwamba, huwezi kuziondoa.
Badala yake unaweza kuzibadili.
Hivyo ili ufanikiwe, unapaswa kubadili tabia mbaya ulizonazo na kutengeneza tabia nzuri.
Tengeneza tabia ambazo ni nzuri na uwe mtumwa wa tabia hizo.
Kwa kuwa mtumwa wa tabia ambazo ni nzuri, mara zote unakuwa kwenye kufanya yale yaliyo sahihi.
Kwa kuwa yote tunayoyafanya ni kwa tabia, kujijengea tabia nzuri na kuwa mtumwa wa tabia hizo kuna manufaa makubwa.
Hatua ya kuchukua;
Orodhesha tabia zote ulizonazo, kulingana na yale unayofanya kila siku. Kisha chagua tabia ambazo siyo nzuri na zibadili kwa tabia ambazo ni nzuri. Chagua tabia ambazo utakuwa mtumwa kwenye hizo ili uweze kufanikiwa. Chagua tabia zako za msingi kabisa utakazoziishi kila siku bila kuacha ili uweze kujenga mafanikio ya kudumu.
Tafakari;
Huwa tunajenga tabia kisha tabia zinatujenga. Chochote tunachotaka kujenga kwenye maisha yetu, tunapaswa kuanza kujenga tabia yake kwanza.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed