#SheriaYaLeo (359/366); Jiweke kwenye uwanja wa kifo.
Tangu enzi na enzi, majenerali wa majeshi wamekuwa wakitafuta njia ya kuwasukuma wanajeshi wao kupambana kwa kila namna ili kupata ushindi.
Wapo ambao wamekuwa wakitunia maneno ya hamasa ili kuwahamasisha wanajeshi wao kupambana.
Maneno hayo yamekuwa na mafanikio kiasi lakini nguvu yake huwa haidumu.
Kwani hamasa inayopatikana kwa maneno huwa inadumu kwa muda mfupi.
Mwanamkakati wa kivita wa China aliyeitwa Sun Tzu aligundua njia ya uhakika ya kuweza kuwahamasisha wanajeshi kupambana mpaka kupata ushindi.
Njia hiyo ni kuwaweka wanajeshi mahali ambapo hawawezi kutoroka.
Aliita mahali hapo uwanja wa kifo (Death Ground).
Kwenye uwanja huo ni kupambana mpaka kushinda au kufa, hakuna njia ya kutoroka.
Pale watu wanapojikuta kwenye hali ambayo ni lazima wapambane la sivyo watakufa, wanapambana kwa kila namna na kupata ushindi.
Lakini watu wanapokuwa na njia ya kuweza kutoroka, wanaitumia kutoroka pale mambo yanapokuwa magumu.
Kifo kina nguvu ya kuweza kuwasukuma watu wajitume kuliko walivyozoea.
Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kufanya kama unataka kufanya makubwa na kufanikiwa.
Kama umekuwa unaahirisha mambo na kupoteza muda, ni kwa sababu hujajiweka kwenye uwanja wa kifo. Unakua huna cha kupoteza kama hutafanya, na ndiyo maana umekuwa hufanyi.
Unapaswa kujiweka kwenye uwanja wa kifo, ambapo kuna kitu kikubwa unapoteza kama hutafanya unachopaswa kufanya. Kitu hicho unachopoteza kinapaswa kukuuma kweli ili usukumwe kuchukua hatua unazopaswa kuchukua.
Weka ahadi ambazo zinakusukuma kutekeleza la sivyo unaingia hasara kubwa.
Wape watu wajibu wa kukusimamia utekeleze la sivyo unalipa faini kubwa.
Fanya chochote ambacho kinakuweka mahali ambapo huwezi kutoroka wala kuzembea na utashangaa jinsi utakavyofanya makubwa.
Sheria ya leo; Jiweke kwenye hali ambayo una mengi ya kupoteza kama utaacha kufanya. Kama huwezi kumudu kupoteza, hutapoteza. Jiweke kwenye uwanja wa kifo, ambapo mgongo wako unakuwa kwenye ukuta hivyo huwezi kutoroka, badala yake unapaswa kupambana mpaka tone la mwisho. Hilo litakusukuma kufanya kwa uhakika.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji