2857; Tawala hisia zako.
Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia.
Huwa tunafanya maamuzi yetu kwa hisia, kisha tunayahalisha kwa mantiki.
Tatizo la hisia huwa hazina msimamo, ni kitu cha kupita kama mawimbi.
Pia hisia zinaathiriwa na mambo mbalimbali.
Ukiwa mtu unayetawaliwa na hisia, hutaweza kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yako.
Kwa sababu kila mara utakuwa unahangaika na kitu kipya, kilichonasa hisia zako kwa wakati huo.
Unapaswa kutawala hisia zako kwa kuhusisha fikra zako kwa kila maamuzi unayoyafanya.
Kwa kila unachosukumwa kufanya, usikimbilie kukifanya kwa ule msukumo unaokuwa nao.
Badala yake kaa chini na fikiri kwa kina na kuweka mpango wa ufanyaji.
Wengi wenye nia njema wamekwama kwa sababu ya kuanza kufanya mambo kwa hisia bila kuhusisha mantiki.
Hisia na mantiki ni kama farasi na mwendesha farasi.
Farasi ni hisia, ana nguvu nyingi lakini zisipodhibitiwa zinaishia kupotea kwa mambo yasiyo na tija.
Mwendesha farasi ni mantiki, ana udhibiti mkubwa, lakini udhibiti huo ukiwa mkali sana farasi haendi popote.
Hivyo hisia na mantiki ni vitu vinavyopaswa kwenda pamoja kwa ushirikiano mkubwa.
Hupaswi kuziondoa kabisa hisia, huwezi kuyaendesha maisha yako bila hisia.
Unachopaswa kufanya ni kuzitawala hisia zako na kuzitumia kwa yale yenye tija.
Kwa kila unachosukumwa kufanya, kaa chini na uweke mpango sahihi wa kukifanya ili kiweze kuwa na matokeo mazuri.
Hatua ya kuchukua leo;
Angalia maamuzi yote ambayo umekuwa unayafanya, ona yapi umekuwa unafanya kwa hisia na yapi kwa mantiki.
Kwa yote unayofanya kwa hisia, jifunze kuyapangilia kwa mantiki ili yaweze kuwa na tija.
Tafakari;
Hisia bila mantiki ni sawa na farasi asiye na mwendeshaji, ataruka ruka sana lakini hakuna popote ataenda. Zitawale hisia zako ili uweze kuzitumia kufanya makubwa kwenye maisha yako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed