2871; Maajabu, hakuna anga.
Kwako rafiki yangu unayedhani kuna vitu haviwezekani kwenye maisha yako.
Jibu ni moja tu, hakuna chochote kisichowezekana kwenye maisha yako.
Wazungu huwa wana kauli inayosema; sky is the limit. Wakimaanisha anga ndiyo ukomo.
Lakini unapokuja kuangalia, anga ni nini? Anga ni mwisho wa macho yetu kuona.
Ukiwa ardhini, unapoangalia juu, unaliona anga, kama vile ndiyo paa linalofunika dunia.
Ukiwa kwenye ndege ambayo inapaa juu sana angani, bado hufikii mwisho na kukutana na huo ukomo.
Badala yake unaendelea kuona anga likiwa juu zaidi.
Maana ya haya yote ni nini?
Ni maajabu ambayo hakuna mtu amewahi kukuambia, hakuna anga.
Anga kama dhana ya paa la dunia ni kitu ambacho hakipo.
Kile tunachoona kama anga ni mwisho wa uwezo wa macho yetu kuona.
Kwa kifupi ni hakuna ukomo wowote ule, unaweza kwenda juu utakavyo bila ya kufikia ukomo.
Nayasema haya kwa sababu kuna baadhi ya watu nawapendekezea kuyakuza maradufu malengo yao ya namba kwenye biashara.
Nawapa namba ambazo ni mara 10 ya walivyopanga sasa.
Wengi wanashtuka na kuona ni namba kubwa zisizowezekana.
Kwa mfano huu wa anga, naamini kila mmoja anapata picha kwamba kila kitu kinawezekana.
Ukomo wowote tunaouona sasa siyo uhalisia, bali ni kitu tumetengeneza wenyewe.
Ukitaka kuthibitisha hilo, wapo watu kama wewe ambao wanafanya zaidi ya kile unachoona kwako ni ukomo.
Ukomo wowote unaoufikiria sasa, haupo. Unachoona ni ukomo ni mwisho wa macho yako kuona na fikra zako kufikiri.
Ukifungua macho ya ndani na kuboresha fikra zako, utaweza kuvuka ukomo wowote unaoona unao sasa.
Leo nakupa zoezi fupi la kufanya.
Anza na ukomo wowote unaoamini sasa, kisha zidisha mara 10.
Mfano, chukua kiwango cha juu kabisa cha kipato unachoamini ndiyo mwisho wako kutengeneza, kisha zidisha mara 10.
Hilo linakuwa ndiyo lengo lako jipya.
Chukua kalamu na karatasi, kisha orodhesha mambo yote unayopaswa kufanya ili ufikie lengo hilo jipya kwa uhakika.
Zoezi hili fupi kitabadili sana fikra na mtazamo wako na utaona jinsi ambavyo mambo mengi unayodhani hayawezekani, yanawezekana sana.
Utajionea mwenyewe jinsi gani kila kitu kinawezekana.
Tukimalizia kwa kurudi kwenye kauli sky is the limit, siyo kweli. Ukweli ni there is no limit, kwa sababu there is no sky.
Hakuna ukomo wa mafanikio unayoweza kupata zaidi ya ule uliojiwekea wewe mwenyewe.
Hivyo rudia kila siku kujiambia sentensi hii; KILA KITU KINAWEZEKANA.
Na pale unapokuwa na wasiwasi kwamba inaweza isiwe kweli, waangalie wale ambao wameshafanya makubwa ambayo kwako unadhani hayawezekani.
Sasa jiulize, huyo ambaye ni binadamu kama wewe ameweza, kwa nini na wewe usiweze?
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe