2888; Angalia Marupurupu.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayeendelea kushangazwa na jinsi watu wanavyoamua kufanya au kutokufanya mambo fulani.

Moja ya sifa kuu kwetu binadamu ni ubinafsi.
Huwa tunaweka maslahi yetu mbele kabla ya wengine.

Unapoona watu wanafanya au kutokufanya kitu fulani, jua wazi kwamba kuna maslahi fulani ya mtu yako hapo.

Kabla hujashangaa watu kufanya au kutokufanya vitu fulani, anza kwa kuangalia maslahi yao yako wapi.
Watu wanaamua kufanya au kutokufanya kitu kwa kuangalia marupurupu.

Unaweza kuona mtu anafanya jambo la kijinga, lakini jua kwake binafsi siyo jambo la kijinga, maana kuna namna maslahi yake yanazingatiwa na yapo marupurupu anayopata.

Ukitaka watu wafanye kitu fulani, weka marupurupu zaidi kwenye kitu hicho. Hilo litawasukuma wakifanye ili wayaoate marupurupu hayo.
Kadhalika kama hutaki watu wafanye vitu fulani, ondoa kila aina ya marupurupu ambayo mtu amekuwa anayapata kwenye kufanya kitu hicho.

Marupurupu ni kitu chenye nguvu kubwa ya kuwasukuma watu kufanya au kutokufanya vitu fulani.
Hii ni silaha ambayo kila anayejihusisha au kushirikiana na watu anapaswa kujua jinsi ya kuitumia vyema ili aweze kukamilisha yaliyo muhimu.

Ukiweza kuyatumia vizuri marupurupu, hakuna kinachoshindikana.
Wajibu wako mkuu ni kuyajua maslahi ya watu kisha kuwaandalia marupurupu yatakayowasukuma kufanya kile unachotaka wafanye.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe