2889; Tunaanza na matokeo, kisha njia.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unapata wakati mgumu kuwashawishi watu watumie njia mpya ambayo ni bora kuliko ya nyuma.

Watu huwa wanapenda kufuata mazoea yao, hata kama kuna namna mpya inayoleta matokeo bora zaidi.

Watu huwa ni wabishi na wagumu sana kubadilika, wanapenda uhakika wa matokeo wanayopata hata kama ni madogo.

Kuwashawishi wabadilike ni zoezi ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa msimamo mkubwa bila kuchoka.

Pingamizi kubwa watakalokupa pale unapotaka wabadilike ni uzoefu wao.
Watakuambia tayari tuna uzoefu kwenye hili.
Wataona uzoefu wao ni bora kuliko mabadiliko unayoleta.

Kama utaenda nao kwa njia hiyo, itakuwa vigumu sana kuwaondoa kwenye mazoea waliyonayo.

Ipo njia bora ya kuwaondoa watu kwenye mazoea waliyonayo.
Njia hiyo ni kuanza na matokeo kabla ya njia.
Unachotaka wewe ni wabadili njia zao, lakini wao hawataki kwa sababu tayari zinawapa matokeo fulani.

Unachopaswa kufanya ni kuwataka wakupe matokeo ya tofauti, kwa njia wanazochagua wao. Watakapotumia njia zao na wakashindwa, hapo sasa inakuwa rahisi kuwapendekezea njia mpya.

Kwa kuwapa uwanja wa kutumia njia zao ila wakashindwa kuleta matokeo, watakuwa tayari kujaribu njia nyingine ili walete matokeo.

Kwa mfano kama una watu wa mauzo ambao unawapa njia mpya za kuuza ila wanazikataa na kutumia za kwao walizozoea, anza kwa kuwapa lengo jipya na kubwa la mauzo.
Unaweza kuanza na lengo la mauzo mara mbili ya yale yanayofanyika sasa.
Watajaribu kwa njia zao ila haitawezekana.
Na hapo sasa ndipo utawaonyesha njia mpya inayoweza kufanya kazi.

Usihangaike sana kuwalazimisha watu kwenye njia fulani, wewe anza na matokeo ya tofauti wanayopaswa kuyazalisha. Hayo yatawasukuma kutumia njia za tofauti na walivyozoea.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe