2892; Dikteta Mwema.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye umejaribu kuwapa wafanyakazi wako kile wanataka lakini bado hawakupi matokeo unayotaka.

Wakati Elon Musk anainunua kampuni ya twitter, wengi hawakujua nini kinaenda kutokea. Waliona ni kama mzaha tu na kudhani hilo halitafanikiwa.

Alipokamilisha manunuzi na kumfukuza mkurugenzi mkuu na yeye kushika nafasi hiyo, bado wengi hawakujua nini kinaenda kutokea. Walidhani hatakuwa na muda wa kuhangaika na kampuni hiyo, maana tayari ana makampuni mengine makubwa.

Ni mpaka pale alipotoa tangazo lililowatikisa wengi ndiyo watu walianza kuelewa nini kitaendelea.
Alieleza wazi kwamba kila mfanyakazi awe tayari kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya alivyozoea au aache kazi na kupewa malipo ya fidia.

Wafanyakazi wengi waliona ni mzaha na kuamini hilo halitafanikiwa. Walidhani wote watagomea hilo la kufanya kazi muda mrefu na kutishia kuacha kazi wote kitu kitakachotikisa kampuni na Musk asiwe na la kufanya bali kukubaliana na matakwa yao.

Lakini Musk hakurudi nyuma, aliendelea kusimamia alichoelekeza.
Na kweli wengi wakaacha kazi, lakini wengine wakabaki.
Cha kushangaza sasa, waliobaki wakawa ni wale bora kabisa.
Na wafanyakazi wengine bora nje ya kampuni hiyo wakawa wanatamani kufanya kazi kwenye hiyo kampuni.

Wale waliodhani tangazo hilo litaua kampuni, wakabaki midomo wazi baada ya kuona likiifanya kampuni kuwa bora zaidi.
Tangazo limefanya kazi ya kuwaondoa wasio bora, ambao hawajajitoa kweli na hapo kuacha uwanja kwa waliojitoa kufanya kazi zao vizuri.

Tunajifunza nini kwenye hili?
Uongozi wa biashara haupaswi kuwa wa kidemokrasia, bali unapaswa kuwa wa udikteta mwema.
Viongozi bora wa biashara siyo wale wanaojaribu kumridhisha kila mtu na kuwapa watu kila wanachotaka.
Uongozi bora wa biashara ni ule unaosimamia maono makubwa ya biashara na kuhakikisha wote wanayaelewa na kuyapigania.

Udikteta mwema kwenye biashara unahakikisha kila mmoja yupo kwenye mwelekeo wa maono makubwa yanayofanyiwa kazi.
Kwa wale ambao hawataki kukaa kwenye maono hayo, hawavumiliwi, wanaonyeshwa mlango wa kutokea ulipo.

Udikteta mwema kwenye biashara unajua kwamba siyo wote watapenda msimamo wa aina hiyo. Wale wasio bora wanakuwa wa kwanza kulalamikia hilo. Lakini wanajua kwa kusimamia hilo, wasio bora wanaondolewa na kubaki walio bora tu.

Mafanikio ya biashara siyo wafanyakazi kumpenda kiongozi, bali biashara kuweza kujiendesha kwa faida.
Hivyo kama biashara haijiendeshi kwa faida, ni wajibu wa kiongozi kufanya kila kitu kuhakikisha hilo linabadilishwa.

Njia ya haraka kwa biashara kushindwa ni kuendeshwa kidemokrasia, wengi wape.
Wengi ni wavivu na wazembe, ukisema uwape kile wanachotaka, biashara inakwenda kufa.

Uongozi wa udikteta mwema kwenye biashara huwa unaanza na maono makubwa ambayo biashara inayo na kuhakikisha hayo yanafanyiwa kazi na wote waliopo kwenye biashara.
Pia uongozi huo unafanya maamuzi yake yote kwa namna, maana namna hazidanganyi.
Haijalishi watu wana nia njema kiasi gani, wanapaswa kuwasilisha namba zao wanazofanyia kazi.

Wewe kama kiongozi wa biashara, unapaswa kuwa na uelewa kwamba kukua au kufa kwa biashara yako kunatokana na maamuzi yako na mtindo wako wa uongozi.
Kwa kuwa wewe ndiye unayewalipa watu na kama biashara ikifa wewe ndiye unayepata hasara, usidanganyike na demokrasia. Unapaswa kuwa dikteta mwema kwa kusimamia maono ya biashara na mchakato sahihi.
Na yeyote anayeenda nje na hayo, mlango wa kuondoka unamhusu.

Usikubali kushikiliwa mateka na watu uliowaweka kwenye biashara yako mwenyewe.
Kumbuka wewe ndiye unayebeba hatari yote kwenye biashara yako.
Una wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila kitu kinaenda vizuri.

Jiamini na simama kwenye kile kilicho sahihi hata kama wengi hawaelewi.
Kama wanakutishia wakiondoka biashara itayumba, usilegeze ili wabaki, bali waache waondoke na hata kama biashara itayumba, uwe tayari kuanza upya na watu sahihi.

Ni bora kuanza upya na watu sahihi kwa mfumo sahihi, kuliko kuendelea na watu ambao ni mzigo.
Kuwa dikteta mwema, biashara yako inahitaji sana hilo ndiyo iweze kufanikiwa.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe