2899; Njia haipotezi.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye umekuwa unajaribu njia mbalimbali lakini hupati matokeo unayotaka.

Ni rahisi kujiambia tatizo lipo kwenye njia. Kwamba njia hiyo siyo sahihi na inapoteza.
Lakini huo siyo ukweli, tatizo halipo kwenye njia, bali lipo kwenye namna unavyofanyia kazi njia hiyo.

Kwa mfano, njia ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha inajulikana wazi kabisa.
Kama mtu atatoka Dar, lakini asifike Arusha, je unadhani njia ndiyo imempoteza?
Jibu ni hapana, mtu huyo anakuwa hajapotezwa na njia, bali mengine anayokutana nayo njiani.

Funzo kubwa unalopata hapa ni kwamba kabla hujalalamika njia inakupoteza, jiulize kwanza kama umeifanyia kazi njia hiyo kwa uhakika.
Bila ya kufanya hivyo, kila wakati utakuwa unajaribu njia mpya na bado usipate unachotaka.

Hakikisha kwanza njia imefanyiwa kazi kwa uhakika kabla ya kuhamia kwenye njia nyingine.
Kila njia inafanya kazi, lakini kwanza lazima ifanyiwe kazi kwa uhakika.

Kama unategemea njia unayopata iwe ni ya mkato na ambayo haihitaji kuweka kazi, tayari unakuwa umepotea kabla hata hujaianza safari.

Mafanikio hayajengwi na vitu vinavyofanyika kwa juu juu, bali yanajengwa kwa yale yanayofanyika kwa kina.

Njia ya uhakika ya kupata unachotaka ina vipengele hivi;
1. Kujua kwa hakika nini hasa unachotaka.
2. Kujua njia ya kupata hicho unachotaka.
3. Kujua gharama za kukaa kwenye njia hiyo.
4. Kulipa gharama na kukaa kwenye njia.
5. Kutoondoka kwenye hiyo njia mpaka umepata kile hasa unachotaka.

Kupata unachotaka kwenye maisha ni sawa na kupata chakula kwenye sherehe, lazima ukae kwenye foleni mpaka ufike kwenye eneo la chakula.
Kwa sehemu kubwa, njia yoyote ile ina nguvu ya kukufikisha unakotaka, ila unapaswa kuifanyia kazi njia husika ndiyo ilete matokeo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe