2900; Sikitika nao, lakini usinunue matatizo yao.

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unapojaribu kujenga urafiki na wateja, wao wanajaribu kuutumia kujinufaisha binafsi.

Wanatumia fursa hiyo kukueleza matatizo yao binafsi na kutaka uwakopeshe kile unachouza.

Kibinadamu, ni mambo ambayo yanaumiza na unashawishika kutaka kuwasaidia watu wa aina hiyo.
Hapo ndipo ninapotaka kukupa tahadhari, kwa sababu unaweza kuishia kuyanunua matatizo waliyonayo watu na yakawa yako.

Rafiki, urafiki tunaokazana kujenga na wateja wetu ni urafiki wa kimkakati. Ni urafiki wa kutufanya tuaminike na wateja na washawishike kununua kile tunachouza.

Sasa basi, pale mtu anapotoka nje ya hilo lengo lako na kutaka kujinufaisha zaidi na urafiki unaojenga, usikubali.

Wateja wanapokueleza shida zao binafsi, wasikilize na sikitika nao, ila usiwashauri chochote, jizuie sana katika hilo. Kwenye mambo ya biashara washauri, ila nje ya biashara usiwashauri.

Kuwashauri watu kwenye mambo yao binafsi ni kupoteza muda wako, kwa sababu hawatafanyia kazi ushauri wako kama hauendani na kile wanachotaka wao.

Lakini pia, matatizo mengi ambayo watu wanayo, wamejisababishia wao wenyewe kupitia uvivu na uzembe ambao wanao. Hicho ni kitu ambacho hawatakikubali kabisa ukiwaambia.

Hivyo msaada mkubwa unaoweza kuwapa ni kuwasikiliza na kusikitika nao, lakini fumba mdomo wako usije ukawashauri chochote.

Pale wateja wanapotaka kutumia urafiki unaojenga nao kutaka uwakopeshe, usikubali kufanya hivyo. Hapa pia sikitika nao lakini kamwe usiwakopeshe, maana utaishia kuyanunua matatizo yao.

Kuna sababu kwa nini mtu ameshindwa kuwa na fedha mpaka anakukopa wewe. Kuna nidhamu anakosa kwenye eneo la fedha. Unapomkopesha, humsaidii, bali unaishia kuyanunua matatizo yake na kuyafanya kuwa yako.

Pale unapoona kuna wateja ambao kila wakati wanakuja kwako na matatizo tu na yanakuchosha, achana nao, wakwepe. Haiwezekani kila mteja akawa wako. Wale unaowaona ni wasumbufu, wasukume waende kwa washindani wako, ili waende wakawasumbue huko.

Kila unachokifanya kwenye biashara yako hakikisha unakuwa na lengo, kisha lengo hilo unalidhibiti wewe.
Watu watajaribu kukuteka kihisia ili ununue matatizo yao.
Kuwa imara eneo hilo, usikubali kununua matatizo ya watu.
Wasikilize na sikitika nao sana, ila usiwashauri chochote na wala usiwakopeshe.
Na pale unapochoshwa na hilo, achana nao.

Usijaribu kuwa kiranja wa dunia,
Mambo mengi yataenda vizuri tu bila wewe kutia neno.
Kaa kwenye biashara yako na acha kuhangaika na mambo ya wengine.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe