2904; Roho nzuri.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayejiambia unataka kuwa na roho nzuri na ukubalike na watu wote.
Hicho ni kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu kuwepo kwa maisha hapa duniani. Na kama utaendelea kukisisitiza basi utashindwa vibaya sana.
Kwa asili, sisi binadamu ni wavivu, wazembe na tunaopenda kupata manufaa makubwa kwa kuweka juhudi kidogo au kutokuweka juhudi kabisa.
Ndiyo maana kamari na michezo ya kubahatisha, ambayo kila mtu anajua nafasi ya kushindwa ni kubwa kuliko ya kushinda, bado inapata wafuasi walio wengi.
Sasa basi, ili uonekane una roho nzuri, inabidi ukubaliane na watu kwenye huo uvivu na uzembe wao, kitu ambacho pia kitakuja kufanya uonekane una roho mbaya baadaye. Kwa sababu kwa kuwaendekeza watu hao kwenye tabia zao hizo, watakuja kupata anguko kubwa na wewe utaonekana hukuwasaidia kukwepa hilo.
Hivyo katika maamuzi yako yote na katika kushirikiana na watu, futa kabisa dhana ya roho nzuri au roho mbaya. Badala yake maamuzi yako yafanyike kwa kuangalia kipi kilicho sahihi kufanyika. Kipi ambacho kina matokeo bora kwa wote wanaohusika.
Kilicho sahihi kufanya huwa siyo rahisi au kinachopendeza kufanya. Hivyo wengi hukwepa na kukimbilia vilivyo rahisi, ambavyo siyo sahihi.
Wajibu wako ni kusimamia kilicho sahihi ndiyo kifanyike, bila ya kujali watu wanaona una roho nzuri au mbaya.
Hivi unadhani asili ingekuwa inafanya kazi yake kwa kuangalia watu wanaona roho nzuri ni ipi kungekuwa na maisha hapa duniani?
Fikiria jua linataka kuchomoza, lakini kuna mtu hataki jua siku hiyo, asili ikasema basi leo jua halitachomoza kwa sababu hatutaki kuwa na roho mbaya! Kama asili ingekuwa inafanya mambo yake hivyo, pasingekuwa na maisha hapa duniani.
Unataka kujenga biashara yako na kupata mafanikio makubwa. Kanuni ni moja, mara zote fanya yale yaliyo sahihi na siyo yale yatakayofanya uonekane una roho nzuri.
Nimalizie kwa kukukumbusha kanuni ya theluthi tatu.
Kwa chochote utakachofanya, iwe kizuri au kibaya, sahihi au siyo sahihi, theluthi moja ya watu watakubaliana na wewe, theluthi moja watakupinga na theluthi moja hawatajali.
Kutaka ukubalike na kila mtu ni kiashiria cha wazi kwamba hutaweza kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Badilika mara moja, simamia yaliyo sahihi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe