2903; Muda wako ndiyo umekosa thamani kiasi hicho?

Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye umekuwa unatumia muda kuokoa fedha.

Unakuwa mwangalifu sana kwenye kila unachofanya ukiangalia mianya ya fedha kupotea au gharama kubwa kubwa.

Katika uangalifu wako huo, umekuwa unaishia kutumia muda wako mwingi zaidi ili kuokoa kiasi hicho cha fedha.

Sasa yote unayofanya ni sahihi na muhimu. Lakini changamoto kubwa inakuja kwenye thamani ya muda wako, ambayo mara nyingi umekuwa hauifanyii kazi.
Hilo linapelekea wewe kutumia muda wa thamani kubwa ili kuokoa fedha ambayo thamani yake ni chini sana ya thamani ya muda wako.

Tutumie mfano ili tuweze kuelewa zaidi.
Una jukumu fulani kwenye biashara yako ambalo huwa unamlipa mtu shilingi laki moja kwa mwezi kulifanya.
Lakini mtu huyo anakupa changamoto mbalimbali katika ufanyaji wa jukumu hilo.
Unaamua umfukuze na jukumu hilo ulifanye wewe mwenyewe.

Kwa haraka hara utaona umepata ushindi, kwa sababu umeokoa gharama ya laki moja uliyokuwa unalipa.
Lakini tukizama ndani, umepoteza, kwa sababu umejipa jukumu ambalo linachukua muda wako, huku likikulipa kiasi cha laki moja tu.

Kwa kufanya jukumu hilo na kuokoa kiasi hicho, unashindwa kufanya majukumu mengine makubwa zaidi na ambayo yangekulipa zaidi.
Hilo linapelekea wewe kuwa umetingwa zaidi, huku kipato chako kikizidi kuwa duni.

Lengo kuu la fedha kwenye maisha ni kununua muda.
Kama huwezi kutumia fedha kujinunulia muda, utanasa kwenye lindi la umasikini kwa muda mrefu sana.
Kila unapotumia muda kuokoa fedha, jua dhahiri umejichimbia kwenye umasikini zaidi.

Ni jambo lenye mtego mkali, kwamba unachotaka ni fedha, na ili uzipate, lazima uzitumie kujinunulia muda zaidi.

Maana yake unapaswa kuijua thamani halisi ya muda wako, kisha kuhakikisha chochote unachofanya kinaendana na thamani hiyo.

Kwa mfano kama unataka uingize kipato cha milioni 10 kila mwezi, kwa kufanya kazi siku 6 za wiki na masaa 10 kwa siku. Kwa kukokotoa unapata masaa 6 x 4 x 10 ambayo ni 240.
Ukigawa kipato kwa hayo masaa unapata 10M ÷ 240 unapata 417,000.
Hiyo ina maana kwamba kila saa yako ya kazi thamani yake ni shilingi 417,000.
Maana yake kubwa kabisa ni kwamba chochote unachoamua kufanya kinapaswa kuwa na thamani hiyo, la sivyo hupaswi kufanya.

Sasa unakuwa na muda wenye thamani kubwa kiasi hicho, halafu unaishia kufanya mambo ambayo thamani yake ni ya chini mno kulinganisha na hiyo thamani.
Kwa haraka utaona unaokoa fedha, lakini kiuhalisia umepoteza fedha nyingi mno.

Tumia lengo la kipato au mauzo ulilonalo kisha kokotoa thamani ya muda wako.
Ukishajua thamani ya muda wako, itumie kupima kila unachotaka kufanya.
Kama kitu hakiendani na thamani ya muda wako, hukifanyi, badala yake wape wengine wafanya.

Na hii ndiyo maana nimekuwa nakuambia jukumu pekee ninalokuruhusu ufanye kwenye biashara yako kwa sasa ni kukamilisha mauzo. Usakaji na uhudumiaji waajiri watu wengine wakusaidie kufanya.
Kwa malengo makubwa ya mauzo uliyonayo, kuhangaika na majukumu mengine nje ya kukamilisha mauzo ni kujihujumu wewe mwenyewe.

Kwenye ukamilishaji, una nguvu ya kuweza kuwakamilisha wateja wakubwa na zoezi hilo likaendana na thamani ya muda wako.
Lakini kwenye usakaji na uhudumiaji, unaweza kupata watu wakayatekeleza hayo vizuri kabisa.

Usipoteze thamani ya muda wako kwa kukimbilia kufanya vitu ili kuokoa fedha.
Badala yake ijue thamani ya kitu kabla ya kukifanya.
Pale thamani ya kitu inapokuwa chini sana ukilinganisha na thamani ya muda wako, hakikisha unatafuta mtu sahihi wa kukifanya na wewe upeleke muda wako kwenye vitu vyenye thamani kubwa zaidi.

Unaweza kuwa unalaumu watu hawathamini muda wako, lakini hebu tuanzie kwako mwenyewe, unauthamini muda wako kwa kiasi gani.
Ukishajioma unatumia muda kuokoa fedha, jua umenasa mahali pabaya sana.
Mara zote tumia fedha kuokoa muda, kwa sababu unaweza kupata fedha zaidi, lakini huwezi kupata muda zaidi.

Kokotoa thamani ya muda wako kisha hakikisha hufanyi chochote ambacho thamani yake ni chini ya thamani ya muda wako.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe