2907; Ushauri.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayepoteza muda mwingi kutoa au kupokea ushauri.
Nimewahi kusema huko nyuma usitoe ushauri kama hujaombwa na usipokee ushauri kama hujaomba.
Wengi hawakulielewa hilo na waliona ni kama kauli tata tu.
Lakini hiyo ni kauli yenye nguvu sana ambayo ukiifanyia kazi, utajiepusha na mengi sana yanayokukwamisha.
Wengi huona kuepuka kuchukua ushauri ambao hujaomba ni kujinyima mawazo mazuri.
Lakini ukweli ni kwamba kama mtu anaweza kukushauri kitu chenye manufaa kabla ya wewe kumweleza kwa kina hali yako, basi una tatizo kubwa zaidi ya huo ushauri unaotaka.
Ninachomaanisha ni kwamba mtu anaweza kukushauri vizuri pale unapokuwa umemweleza kwa kina hali uliyonayo, kisha akatafakari kwa kina na kutumia ujuzi na uzoefu wake kukushauri.
Kama mtu anaweza kukushauri mambo ya maana kabla hata hujamweleza kwa kina kuhusu hali yako, maana yake kuna mengi ya msingi bado hujayafanya.
Kwa maana hiyo, unachohitaji sana siyo ushauri, bali kwanza kuacha uvivu na uzembe.
Tukienda upande wa pili wa kutokutoa ushauri kama hujaombwa.
Hapa napo watu huwa wabishi, wakijiona wanawajibika kuwashauri wengine pale wanapoona wanapotea.
Lakini ukweli ni kwamba kama mtu hajakuomba ushauri, hataki ushauri wako.
Na kama utakaidi hilo na kulazimisha kumshauri mtu, kwa sababu umeona anahitaji sana ushauri wako, kinachotokea ni wanakuchukia.
Chuki yao inajidhihirisha wazi pande zote.
Kama ushauri uliowapa utakuwa na manufaa kwao, hawatakuambia chochote.
Lakini kama ushauri uliowapa utakuwa na madhara kwao, watakulaumu sana kwamba umewashauri vibaya.
Kwa hiyo hapo unajionea mwenyewe jinsi zoezi zima la kutoa ushauri pale ambapo hujaombwa linavyokuwa limekosa maana.
Kuchukua ushauri ambao hujaomba na kutoa ushauri ambao hujaombwa pia ni dalili ya kutokujua hasa unataka nini au kutokujitoa hasa hasa kwenye kile unachotaka.
Kaa mbali sana na huu ushauri wa bure na reja reja, kama wewe ni mtu makini, hakuna unachoshauriwa bure ambacho hukuwa unakijua.
Kama unahitaji ushauri, tafuta mtu sahihi, mwenye uelewa na uzoefu juu ya jambo unalohitaji kushauri, mweleze kwa kina hali iliyonayo na yote ambayo umeshafanya kisha msikilize kwa makini anapokushauri. Mwulize maswali ili kupata ufafanuzi zaidi.
Kama unataka kutoa ushauri kwa wengine, hakikisha wamekuja kwako na kukuomba uwashauri. Na hata wakikuomba, usikimbilie kutoa ushauri, msikilize kwanza kwa makini, mhoji maswali mengi ili upate uelewa wa kina kabla hujaanza kumshauri.
Na kama biashara yako ya msingi siyo ya kutoa ushauri, epuka sana hilo zoezi zima la kutoa ushauri kwa wengine.
Kuwa ‘bize’ sana na kile unachopambania kiasi kwamba hujui hata umshauri nini mtu kwenye hali anayokuwa anapitia.
Kingine nitakachoongesa hapa ni swala la bure. Ushauri unaotoa au kupokea bure, thamani yake ni sawa na bure pia. Ni vigumu sana kupata kitu cha maana kwenye bure.
Huwa nasema, gharama ya ushauri wa bure ni pale unapofanyiwa kazi. Hapo ndiyo utagundua kwamba haukuwa ushauri sahihi.
Kama kweli mtu anataka ushauri wa kumtoa alipokwama, anapaswa kuwa tayari kuingia gharama katika hilo.
Mwisho kabisa, jua kutofautisha ushauri na elimu. Maana usipoweza kutofautisha hayo, utajikuta unahangaika sana na ushauri ukidhani unatoa elimu.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe