2909; Vipaumbele.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayelalamika kwamba huna muda wa kufanya baadhi ya mambo ambayo unapaswa kuyafanya.
Kiuhalisia, tatizo lako siyo muda, bali tatizo lako ni vipaumbele.
Kila siku unapata masaa yako 24, yaliyojaa kabisa na wewe ndiye unayepanga unayatumiaje masaa hayo.
Unapolalamika huna muda, unajua kabisa kwamba siyo umepunjwa masaa ya siku, bali kwa namna ilivyoyapangilia na kuyatumia, kuna vitu vinakosa nafasi kwenye huo muda wako.
Vitu unavyoona ni muhimu huwa unapata muda wa kuvifanya au vyenyewe huwa vinajipenyeza mpaka kuingia kwenye muda ulionao.
Hivyo kila unapojiambia huna muda, jikamate mara moja na jiulize umekuwa unatumiaje muda ambao tayari unao.
Inapokuja kwenye biashara, nafasi ya biashara kufanikiwa inategemea na imepewa kipaumbele gani kwenye maisha ya mtu.
Sababu namba moja ya biashara kushindwa ni kutokuwa kipaumbele cha kwanza kwenye maisha ya mtu.
Yaani mtu anakuwa anaruhusu mambo mengi yaweze kuathiri biashara.
Ujumbe anaokuwa anapeleka ni kwamba biashara siyo kitu muhimu zaidi kwako.
Kwa walio wengi, biashara zao hazipo hata kwenye tatu bora ya vitu muhimu zaidi kwao.
Mtu anaweza kufunga biashara ili tu akaangalie mchezo fulani.
Sasa hebu fikiria mteja anayekuja akiwa na uhitaji halafu anakuta hujafungua biashara kwa sababu umeenda kuangalia mchezo, unadhani ni picha gani anayoondoka nayo kuhudu wewe na biashara yako?
Au upo unamhudumia mteja, ghafla siku yako inaita, unapokea na kuanza kuongea, maongezi ambayo yanaonekana ni binafsi na hayana uhusiano wowote na biashara, unadhani mtu huyo anaondoka na picha gani?
Kwamba mteja kwako siyo kipaumbele cha kwanza.
Unadhani mteja wa aina hii akipata mahali anahudumiwa vizuri na kuthaminiwa, atakuja tena kwako?
Rafiki, uko hapo ulipo leo kwa sababu ya vipaumbele ulivyochagua huko nyuma, iwe kwa kujua au kutokujua.
Kutoka hapo ulipo sasa na upige hatua kubwa zaidi, unapaswa kuanza na upangiliaji wa vipaumbele vyako.
Yachukulie maisha yako yote kwa ujumla na weka orodha ya vipaumbele vyako, kuanzia kilicho muhimu zaidi na kinachofuata.
Unapoweka vipaumbele, maana yake kilicho juu kinafanyika kabla ya kilicho chini. Zingatia sana hili katika mipango unayokuwa nayo ya kutekeleza majukumu mbalimbali na kufikia malengo uliyonayo.
Muda tayari unao, tena mwingi sana mpaka umekuwa unaupoteza kwa kufanya mambo yasiyokuwa na tija.
Ukianza kuupangilia muda wako vizuri, utaziona fursa nyingi za kukamilisha unachotaka.
Kama hakuna kitu chochote ulichochagua kukipa kipaumbele cha kwanza, wengine watakutumia wewe katika kukamilisha vipaumbele vyao muhimu.
Kama bado ulikuwa hujawa na kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako, leo nakupa, ni biashara yako.
Hakikisha biashara yako ndiyo inakuwa kipaumbele muhimu kuliko vitu vingine vyovyote.
Lazima uwe tayari kutoa kafara vitu vingine vyote ili tu kuipambania biashara yako.
Ni mpaka ufike ngazi ya juu kiasi hiki ya umuhimu wa kitu ndiyo utaweza kupata mafanikio makubwa sana.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe