2912; Hakuna Amani.

Kwako rafiki yangu mpendwa unayedhani mafanikio makubwa yatakuwa chanzo cha amani na utulivu kwako.

Nina habari ambazo siyo njema sana kwako. Mafanikio makubwa unayoyasaka hayatakupa amani na utulivu.

Kwa hakika, kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyozidi kukosa amani na utulivu.

Kwanza kabisa kadiri unavyofanikiwa, wajibu wako pia unaongezeka. Unawajibika kwa mambo mengi zaidi unapokuwa na mafanikio makubwa.
Kuna usemi, madaraka makubwa yanakuja na wajibu mkubwa. Hilo ndiyo linalotokea kadiri unavyozidi kufanikiwa.

Pili ni unatengeneza maadui wengi kadiri unavyozidi kufanikiwa. Hata kama hujafanya lolote baya kwa watu, kadiri unavyozidi kufanikiwa ndivyo unavyozidi kutengeneza maadui wengi.
Kutakuwa na washindani kwenye kile unachofanya, ambao watakuwa wanatafuta kila njia ya kukuangusha.
Kutakuwa na wanaotaka kujinufaisha na mafanikio yako, kupitia madai mbalimbali watakayokuja nayo.
Kuna watu wa karibu yako ambao watapata wivu kwa sababu tu umefanikiwa kuliko wao.
Halafu kuna taasisi za kiserikali ambazo zitakuandama sana kutokana na mafanikio yako.
Kwa kifupi kadiri unavyofanikiwa ndivyo utakavyokuwa unaibua maadui kila kona.
Huwa kuna kichekesho kwamba ukiwa masikini maisha yako yote serikali haihangaiki kujua chanzo cha umasikini wako. Lakini ghafla ukiwa tajiri, serikali inaanza kuchunguza chanzo cha utajiri wako.

Tatu ni mafanikio makubwa yanapunguza uhuru wako binafsi. Kuna mambo unaweza kuyafanya unapokuwa huna mafanikio makubwa, lakini ukishakuwa na mafanikio makubwa huwezi tena kuyafanya. Kadiri unavyokuwa na mafanikio makubwa ndivyo kila unachofanya kinafuatiliwa na wengi. Huwezi tena kujiachia na kufanya mambo kwa namna unavyojisikia wewe mwenyewe.

Rafiki, siyo kwamba nakutisha, bali nakupa uhalisia wa mafanikio makubwa, ili uwe na picha ya sahihi ya kitu gani unachokiendea.
Wengi wamekuwa wanakuja kukutana na hayo bila kutarajia na hilo linawaumiza na kuwakatisha tamaa.

Sikuelezi haya kukukatisha tamaa, bali kukuandaa vyema na yale unayoyaendea.

Lakini kama moyo wako ni dhaifu, kama huna uimara wa kuweza kuyakabili yote hayo, haina ubaya ukachagua kuachana na mafanikio makubwa.
Bado unaweza kuwa na maisha mazuri kwa mafanikio ya kawaida.
Lakini jua wazi hakuna alama kubwa utakayoiacha hapa duniani bila gharama kubwa utakayolipa kwenye kupambania mafanikio makubwa.

Nimependa nikupe uhalisia wa hii safari, usije kusema sikujua.
Kuwa na matarajio sahihi ni hitaji muhimu kwenye hii safari ya mafanikio.
Kadiri unavyozidi kufanikiwa ndivyo unavyozidi kukosa amani na utulivu.
Ni hali ya kawaida kabisa kwa kila mtu, jiandae kuikabili.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe