2914; Usitoboe sikio.
Kwako rafiki yangu mpendwa unayepima mafanikio yasiyo mafanikio.
Kipimo kisicho sahihi cha mafanikio kimekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wengi kuyafikia mafanikio ya kweli.
Moja ya njia ambazo huwa natumia kupata utulivu wakati nafanya kazi kubwa ya uandishi ni kusikiliza muziki.
Na katika kusikiliza muziki, huwa kuna nyimbo chache ambazo huwa nazirudia rudia mara kwa mara kwa sababu nakuwa nimependa mtindo au maudhui yake.
Lakini pia katika nyimbo ambazo huwa nasikiliza, nimekuwa napata kauli mbiu mbalimbali ambazo nimekuwa natumia kwenye huduma mbalimbali ninazotoa.
Kwa mfano kauli mbiu yetu ya mwaka wa mafanikio 2022-2023 ni ‘Kata Simu, Tupo Site.’
Hii ni kauli mbiu ambayo nilikuwa naisikia sikia mitandaoni, lakini nikaja kuisikia kwenye wimbo unaitwa Dear X ambao ninaupenda na huwa nausikiliza mara kwa mara.
Kwa kuisikia sana kauli hiyo, nikaona ni kitu tunaweza kufanyia kazi, tuachane na usumbufu (kukata simu) na kukaa kwenye lengo kuu (kuwa site).
Hivi karibuni kuna wimbo mwingine umenasa sana kwenye rada zangu na nimekuwa nausikiliza mara kwa mara. Wimbo unaitwa Champion na umeimbwa na mwanamziki anayeitwa Kontawa.
Ni wimbo ambao maudhui yake yana uhalisia mkubwa wa maisha ya mapambano, vitu vingi alivyotaja huko nimevipitia binafsi.
Kwenye mashairi ya wimbo huo, kuna mstari anasema; ‘Mtaani kwetu siyo, mtu aliyetoboa sana alitoboa sikio.’
Huu ni mstari ambao umekuwa unanifikirisha sana.
Moja ya uzuri wa usanii ni kwamba sentensi moja inaweza kuwa na maana tofauti nyingi na zote zikawa sahihi.
Hivyo moja ya maana nilizotoka nazo kwenye sentensi hiyo ni tunaweza kuwa tunapima mafanikio yasiyo mafanikio.
Na hapo ndipo nilipounganisha na moja ya kauli mbiu zetu kwenye safari ya ubilionea.
Kauli mbiu hiyo ni #LazimaNitoboe
Hapo nikapata picha, kumbe mtu anaweza kusema NIMETOBOA.
Halafu ukamuuliza umetoboa nini? Akakujibu nimetoboa sikio!
Ni kweli ametoboa, lakini kutoboa huko kunampa nini?
Hilo ndiyo jambo nimependa tunadiliane leo.
Kwa sababu kikwazo kikubwa ninachoona kwenye mafanikio ya wengi ni kutokujua hata mafanikio yana maana gani kwao.
Wengi wanajiendea na maisha yao kwa kufuata mkumbo.
Mafanikio kwao ni kujilinganisha na wengine, wale waliosoma nao, wanaofanya nao kazi/biashara au wa rika moja.
Ndiyo maana jamii zetu zina ulinganisho kwenye kila eneo la maisha.
Utasikia, wenzako wana nyumba, magari, familia n.k.
Ulinganisho huo ndiyo unawasukuma watu kuachana na ndoto zao na kukimbizana na ndoto hizo za mkumbo.
Mtu aliyeajiriwa akachukua mkopo na kujenga nyumba, hawezi kuwa sawa na anayejenga biashara yake akianzia chini. Hata kama wamesoma pamoja na wanalingana umri.
Huwezi kujenga biashara na kujenga nyumba kwa wakati mmoja, hasa pale mtaji unapokuwa kikwazo kikubwa kwako.
Lakini presha ya jamii inapokuwa kubwa, kwamba ona wenzako wamejenga, anayejenga biashara naye anakimbilia kujenga nyumba, anachota mtaji kwenye biashara na kupeleka kwenye ujenzi.
Kinachotokea, nyumba haikamiliki na biashara inakufa. Mtu anakuwa anaanzia pointi sifuri tena.
Huo mfano mmoja tu ni hadithi ya kweli ya jinsi ndoto nyingi za kibiashara zinavyokufa.
Na huko ndiko ninakoita kutoboa sikio. Unapima mafanikio ambayo siyo mafanikio. Kijamii inaweza kuonekana ni kitu kikubwa, lakini kwako siyo. Una ndoto kubwa zaidi, ambazo hizo ndiyo unapaswa kuzipambania.
Ukijichanganya na jamii, utaishia kujisifia umetoboa, lakini kumbe umetoboa sikio.
Binafsi sijawahi kujisikia vizuri mtu akinisifia kwa nyumba au gari, hivyo havipo kwenye orodha ya mafanikio kwenye maisha yangu. Navihesabia kama mahitaji ya msingi, kama ilivyo kula na kuvaa. Najua kwa wengi kuwa na vitu hivyo ni mafanikio makubwa mno, ya kuwafanya wajisikie vizuri na kuhakikisha kila mtu anajua.
Lakini kwangu vitu hivyo ndiyo naita kutoboa masikio.
Nilinunua gari yangu ya kwanza nikiwa nakaa kwenye chumba kimoja cha kupanga. Kila aliyenijua alisema kila aliloweza kuhusu maamuzi hayo, kwa nini hiyo pesa nisingenunua kiwanja na mengine mengi.
Lakini nilipuuza yote hayo, kwa sababu kwangu kuwa sehemu nyingi kwa muda mfupi ilikuwa muhimu zaidi.
Moja ya vitu ambavyo huwa vinavuruga sana ratiba yangu ni safari ndefu. Safari ambayo unatumia siku nzima, inaharibu ratiba zangu kwa siku zaidi ya 2. Wakati ratiba yangu ya siku moja ina vitu vingi mno, zaidi ya vitu vya wiki nzima kwenye ratiba ya mtu wa kawaida.
Hivyo nimekuwa nakwepa sana kusafiri mpaka pale inapokuwa muhimu hasa.
Na kwa safari muhimu, nimejiwekea sera kwamba kama ni kilomita zaidi ya 400, basi natumia usafiri wa ndege.
Hata kama nitatumia gharama kubwa kwenye safari kuliko lile naenda kufanya, lakini nakuwa nimeokoa muda mwingi ambao naweza kuutumia kwa tija zaidi.
Kuna kipindi msanii mmoja mkubwa alikuwa anasema anapanga kuwa na ndege yake binafsi. Kama ilivyo kawaida, watu wakawa wanasema ni anasa na matumizi mabaya ya fedha na mengine ya aina hiyo.
Mimi huwa siyo mfuatiliaji wa maisha ya wasanii, hivyo habari za aina hiyo huwa sizipati haraka. Nakumbuka mtu aliyenieleza hilo alikuwa mke wangu, sijui alikuwa anasema nini, akasema, msanii fulani ananunua ndege.
Nakumbuka bila kusita mara mbili nikamwambia hilo ni wazo zuri, hata mimi nitakuja kununua ndege.
Akashangaa sana na kuuliza kwa nini.
Nilipojiwekea sera ya kutumia usafiri wa ndege ili kuokoa muda, nilidhani nitaokoa muda kwa kiwango cha juu sana.
Kama kawaida nikaingia kwenye kupima na kutathmini hilo. Nikagundua bado napoteza nusu ya muda ambao nilitaka kuokoa.
Kwa mfano, kwa safari ya saa moja angani kwa ndege, napoteza zaidi ya masaa matatu ya kuikamilisha safari.
Inabidi kuripoti uwanja wa ndege masaa mawili kabla ya safari, upitie mlolongo mrefu mpaka uje kuanza safari. Na ili ufike masaa mawili kabla, lazima utoke ulipo saa nyingine nzima kabla.
Hapo ndipo nilipoona kwa lengo la kuokoa muda, bado kutumia usafiri wa wengi haiwezi kusaidia. Hasa hapo ukiweka kwamba huwezi kupanga ratiba yako ya safari, inabidi ujipange kulingana na ratiba ambayo tayari imeshawekwa.
Sasa kulingana na maono niliyonayo, safari ndefu na nyingi zitakuwa sehemu kubwa ya maisha yangu kwa kipindi kirefu.
Na hivyo suluhisho la hilo itakuwa ni kuwa na ndege binafsi.
Nitakapokuwa na ndege binafsi, sitayahesabu hayo kama mafanikio, kwa sababu hiyo ni njia tu ya kuchangia mafanikio ninayoyapambania.
Nimegusa mengi kwenye ujumbe huu wa leo, lengo ni kutaka kukupa picha halisi ili usivurugwe na jamii inayokulazimisha upime mafanikio yasiyo mafanikio.
Wacha watu wafurahie yale wanataka, lakini wewe, macho yako yote weka kwenye mafanikio makubwa unayoyaoambania.
Una nyumba za kuishi, magari binafsi, umesomesha watoto na mengine ya aina hiyo siyo orodha ya mafanikio kwako. Hayo ni mahitaji ya msingi ambayo ulitegemewa uyatekeleze, kama usingeyatekeleza ungekuwa uzembe wako binafsi. Lakini siyo utembee kifua mbele ukihesabu hayo kuwa mafanikio.
Watu watakusifia kwenye hayo, usipotezwe na hizo sifa. Washukuru, ila puuza mara moja na rudi kazini, yapambanie mafanikio halisi kwako.
Nimalizie kwa kukazia, #LazimaUtoboe lakini #UsitoboeSikio.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Asee umeandika kitu cha ukweli!!mengi haya kuwa na majumba magari siyo mafanikio asee ila ndo vitu vinawapa watu stress wanapoona wenzao wanavimiliki na wao hawana wanahesabu kuchelewa.
Huu ukurasa ni lazima uwe umekomaa sana kujua maana ya mafanikio maana utapingana na mengi jamii inayoyaita ni mafanikio.
LikeLike
Kweli kabisa
LikeLike