2917; Usibake

Kwako rafiki yangu mpendwa unayeona usipouza kwa mteja mara moja basi umekosa kila kitu.

Rafiki, nimekuwa nakuambia mara kwa mara na nitaendelea kukuambia sana kwamba mauzo ni mchakato na siyo tukio.

Na kadiri unachouza ni cha bei kubwa, ndivyo mchakato unavyokuwa mrefu zaidi.

Kutaka ukutane na mteja mara moja na hapo hapo anunue haina tofauti na kubaka.
Utajikuta ukilazimisha sana, kitu ambacho kitamuumiza mmoja kati yenu au wote.

Utamuumiza mteja kwa kumpa kitu ambacho hakina manufaa kwake. Kwa kulazimisha kwako anaona anunue ila akishanunua ndiyo umempoteza kabisa. Sasa hayo siyo mauzo, mauzo unatakiwa upate pesa zao na urafiki wao. Akinunua mara moja halafu asitake kurudi tena au hata kukuletea wengine, umepoteza.

Pia utajiumiza mwenyewe kwa kupunguza sana bei na kuuza kwa hasara ili tu uyakamilishe mauzo. Pale unapoona kikwazo kwa mteja ni bei au mteja anakitumia kama njia ya kukupa mapingamizi, wewe unakazana kupunguza bei bila kujali.

Huko ndiyo kubaka na ubakaji haujawahi kumwacha mtu salama.

Ninaposema kubaka, namaanisha kubaka kweli.
Maana pia mauzo ni kama mapenzi.
Unaweza kukutana na mtu njiani ukawa umempenda.
Kama ukimwendea mara moja na kumwambia nimekupenda sana, nataka leo tuoane na tufanye mapenzi, kwa hakika atakataa.
Sasa kama utatumia mbinu zozote ulizonazo kulazimisha kufikia azma yako hiyo, ndiyo unaishia kubaka.

Mauzo ni mahusiano, ni kumjua mteja kwa undani, mahitaji yake, matatizo yake, maslahi, vipaumbele, matamanio na hofu zake kabla hata hujampendekezea kile unachouza.

Ukishamjya mteja kwa kina kwenye maeneo yote hayo, ndipo sasa utampa mpango wa kile unachouza na jinsi ambavyo kitamfaa yeye, kwa kuwa na manufaa makubwa sana kwake.

Huwezi kujenga mahusiano bora kwenye maisha kama wewe ni mbakaji. Watu watakukimbia na utakuwa mpweke mara zote.

Kadhalika, huwezi kufanya mauzo makubwa kwenye biashara kama wewe ni mlazimishaji.
Kwa mbinu zenye nguvu utaweza kuwauzia baadhi ya wateja, lakini wakishanunua kwako hawatarudi tena.

Kama unataka kujenga utajiri mkubwa kwenye biashara, ni lazima ujifunze na kubobea kwenye mauzo yaliyo sahihi, ambayo ni ya kujenga mahusiano bora na wateja wako.

Ili kujenga mahusiano hayo hupaswi kuwa mvivu na mzembe. Unahitaji kuweka kazi kubwa kuwafuatilia wateja wako na kuwajua kwa undani, kuwafanya wajue upo na kuwapa mapendekezo yenye manufaa kwao.

Uzuri ni kwamba hayo yote unaweza kujifunza bila ya kujali upo kwenye hali gani kwa sasa.
Eneo la mauzo ni eneo la kila mfanyabiashara kubobea ili aweze kufikia ndoto kubwa alizonazo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe