2918; Washindwe kunyamaza.
Kwako rafiki yangu mpendwa ambaye unashindwa kuwashawishi wateja wa biashara yako kukuletea wateja zaidi.
Katika njia zote za masoko zilizopo, njia ya wateja kuambiana ndiyo njia yenye nguvu kubwa na matokeo mazuri.
Watu wanaposikia kitu kutoka kwa watu wao wa karibu wanashawishika haraka kuliko wakisikia kutoka kwa mfanyabiashara.
Kuna nyakati unatamani kuwaomba wateja wako wakuletee wateja wengine wengi zaidi.
Lakini hilo linaishia kwenye mawazo na siyo utekelezaji.
Ipo njia ya uhakika ya kuwafanya wateja wako wawe tayari kuwaambia watu wao wa karibu kuhusu biashara yako.
Kwa njia hiyo, unawafanya wateja hao washindwe kunyamaza.
Wanajikuta wakiwa na msukumo wa ndani wa kuwaeleza wengine.
Njia hiyo ni kufanya kile unachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana kiasi cha watu kujikuta wakiwa na msukumo wa kuwaeleza wengine kuhusu kile walichopata.
Unapaswa kuhakikisha kila unachompa mteja ni bora na cha hali ya juu. Hilo linamfanya ashindwe kabisa kukaa kimya.
Kwa njia hii unapaswa kuwafanya wateja waone kila mtu anapaswa kutumia kile mnachouza. Wafanye wawashangae wale ambao hawajui au hawajawahi kutumia kile unachouza.
Haya yote yanawezekana kama tu utajisukuma na kwenda hatua ya ziada kwenye kila unalofanya.
Wateja ambao tayari unao ni hazina kubwa ya kupata wateja wapya wengi zaidi.
Unachohitaji ni kuwapa sababu sahihi ya wao kukufikisha kwa wengine wengi.
Kuwapa huduma bora kabisa ambayo hawajawaji kuipata kwa wengine ni njia rahisi ya kuwatumia wateja ulionao kuwafikia wateja wengine wapya.
Jiwekee mkakati wa kibiashara ambapo wateja wote ulionao sasa au wanaokutana na kazi zako, wawe na sababu ya kuiongelea biashara yako kwa wengine.
Na hilo halihitaji ufanye miujiza mikubwa, bali linahitaji uwape watu kitu ambacho kitawafanya wakiongelee kwa muda mrefu.
Jali na weka maslahi ya wengine mbele na wao watajali na kuweka maslahi yako mbele.
Hii ni kanuni ya msingi kabisa ambayo haijawahi kushindwa.
Ifanyie kazi mara zote.
Waone wateja wengi wapya kupitia wale wachache unaowahudumia sasa. Kisha chukua hatua ya kuhakikisha unapata wateja wapya kwa kila mteja ulionao sasa.
Wape kitu kitakachowafanya wakuzungumzikie kila mahali.
Kila wakati jiulize unawezaje kupata wateja zaidi kupitia wateja ulionao, kisha chukua hatua sahihi ili uweze kuwafikia wateja wapya wengi zaidi.
Fanya kila unachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana kiasi kwamba wale unaowalenga hawawezi kunyamaza. Wanapata msukumo mkubwa wa ndani yao wa kuwaeleza watu wote wa karibu kwao kuhusu mazuri waliyoyapata.
Hilo ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wako kabisa kulifanya, unachopaswa ni kuacha uvivu na uzembe, uwajue vyema wateja wako na uende hatua ya ziada wakati wa kuwahudumia.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe