2925; Jiamini kupitiliza.
Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio makubwa uliyopo, upinzani unaokabiliana nao ni mwingi na mkubwa sana.
Kila kitu kinakuzuia wewe usipate mafanikio makubwa unayoyataka.
Upinzani huo unaanzia ndani yako mwenyewe. Tabia zako binafsi ni kikwazo kikubwa sana kwako kufanikiwa. Uvivu, uzembe na kukata tamaa na vitu vinavyokukwamisha usifikie mafanikio makubwa unayoyataka.
Halafu kuna wale watu wa karibu yako wanaokuzunguka. Hawa wanataka ufanikiwe, ila usifanikiwe sana kuwazidi wao. Maana ukifanikiwa kuwazidi, utaonyesha dhahiri uvivu na uzembe wao.
Hivyo watafanya kila kitu kuhakikisha wanakuzuia usipate mafanikio makubwa.
Mazingira yanayokuzunguka pia ni kikwazo kikubwa kwako kufanikiwa. Mengi unayokuwa unayahitaji ili kufikia lengo lako yanakuwa hayapatikani kwenye mazingira uliyopo.
Pia kuna mifumo mbalimbali ya kijamii, kidini na hata kiserikali ambayo inakuzuia usifanikiwe sana. Kwa sababu mifumo hiyo inajua ukifanikiwa sana hutatawalika, utakuwa huru kuishi vile utakavyo. Mifumo hiyo inataka kukutawala milele, hivyo itafanya kila namna kuhakikisha hufanikiwi sana.
Kuna mengi sana unayopaswa kufanya ili kuvuka upinzani huo mwingi wa mafanikio yako.
Lakini la kwanza kabisa na muhimu ni KUJIAMINI WEWE MWENYEWE KUPITILIZA.
Unapaswa kujiamini sana ndiyo uweze kuvuka vikwazo vyote vilivyopo kwenye safari yako ya mafanikio.
Lazima ujiamini wewe ndiye bora kabisa kuwahi kutokea na unao uwezo wa kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Unapaswa kuamini bila ya shaka yoyote kwamba lazima utayafikia mafanikio makubwa unayoyataka.
Kwamba hakuna chochote kinachoweza kukuzuia wewe kufikia mafanikio yako.
Uamini kilichopo kati yako na mafanikio makubwa unayoyataka ni muda tu.
Lazima uamini pasi na shaka yoyote ile kwamba hakuna kinachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Kwamba kuna vitu vingi vitajaribu kukuzuia, lakini una uhakika wa kuondoa vikwazo vyote na kupata unachotaka.
Imani hiyo kubwa unayokuwa nayo haitawafurahisha wengi, hasa ambao hawana uthubutu wa kujiamini kupitiliza.
Hivyo watakupa shutuma za kila aina. Watakuambia una matatizo ya akili, unajigamba na utaanguka.
Hayo yote yapuuze, hayana maana yoyote kwako.
Wajibu wako ni kujiamini kupitiliza na kuamini hivyo bila ya shaka yoyote.
Hata kama mbele yako huoni kabisa njia ya kukufikisha kwenye mafanikio unayoyataka.
Hata kama mbele unaona giza kubwa.
Usiwe na shaka yoyote kuhusu kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Jiamini bila ya shaka yoyote kwamba utapata mafanikio makubwa unayoyataka.
Inaanza imani kwanza halafu mengine ndiyo yanafuata.
Unapokuwa na imani thabiti na isiyoyumbishwa na chochote, inapelekea asili kukupisha upate kile unachotaka.
Hata pale unapopitia magumu na changamoto mbalimbali, usipoteze imani kwamba wewe ni bora na utapata kile unachotaka bila ya shaka yoyote.
Kuthibitisha hili, anza na thamani ya muda wako.
Upe muda wako thamani ya kifedha, kulingana na kipato unachotaka kuingiza.
Anza na kipato unachotaka kuingiza kwa mwaka, kisha gawa kwa mwezi, wiki, siku na saa.
Jua thamani ya saa yako moja ni kiasi gani.
Kisha tumia hicho kama kigezo kwa vitu unavyojihusisha navyo.
Ukishaijua thamani ya muda wako, usifanye chochote ambacho hakiendani na thamani hiyo.
Unahakikisha chochote unachofanya kinaweza kukuingizia thamani ya muda wako au kinakuweka kwenye nafasi ya kuweza kukuingizia thamani hiyo.
Kwa mfano kama thamani ya muda wako (saa moja) ni Ths laki moja (100,000/=), (kiwango cha chini kabisa kwa kila aliye kwenye KISIMA CHA MAARIFA kwa sasa), unahakikisha kila unachofanya kina uwezo wa kukuingizia hiyo laki moja kwa saa, au kinakuandaa kuja kuweza kuingiza kiasi hicho.
Kataa kabisa kujihusisha na chochote ambacho thamani yake ni chini ya hapo.
Wafanye watu wajue wazi kabisa thamani ya muda wako na vitu gani utakavyokubali na vipi utakavyokataa.
Kwa kujiamini kwenye hiyo thamani ya muda wako, utaanza kuvutia yaliyo sahihi kwako.
Lakini kama hutajiamini, utayumbishwa na kuangushwa mara moja.
Kadiri unavyotaka mafanikio makubwa ndivyo unavyopaswa kujiamini kupitiliza.
Imani hiyo inakuwa kinga kwako kujilinda na magumu na pia inakuwa msaada kwako kuinuka pale unapoanguka.
Kushinda au kushindwa kwenye maisha kunaanzia na kiwango cha wewe kujiamini mwenyewe.
Kama hujiamini kupitiliza, bila ya shaka yoyote ile, hakuna namna utaweza kuvuka vikwazo vyote vilivyo kwenye safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Uvivu, uzembe na kukata tamaa ndiyo maadui wakubwa kwenye mafanikio! Nitawashinda maadui hawa ili niweze kupata kile ninachotaka.
Asante sana Kocha, Dr.Makirita Amani
LikeLike
Hakika nafanyia kazi maharifa haya
LikeLike