2929; Biashara na ndugu.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa nia njema unaweza kuwaweka watu wako wa karibu kwenye biashara yako.
Ndugu, jamaa na marafiki zako wanaweza kuwa hawana cha kufanya na ukaona ni vyema uwape kazi kwenye biashara yako.

Ni jambo jema kufanya kiutu, lakini mara nyingi huwa linakuwa baya sana kibiashara.

Watu wengi wa karibu wanaoajiriwa kwenye biashara, kwa sababu ya ukaribu wao, huwa wanaishia kuwa wasumbufu sana kwenye biashara hizo.

Huwa wanajiona wao siyo sawa na wafanyakazi wengine na hivyo kutokufuata taratibu mbalimbali zilizopo kwenye biashara

Hilo hupelekea kuzalisha matatizo mengi sana ya kibiashara. Wanavuruga timu kwa wao kutokufuata taratibu zilizopo.
Pia wanapelekea hasara na upotevu mkubwa.

Kama unataka kujenga biashara kubwa na yenye mafanikio, unapaswa kuwa makini sana na watu wa karibu unaowaajiri kwenye biashara yako, hasa pale kigezo cha kuwaajiri kinapokuwa ni ukaribu wao.

Kama umemwajiri ndugu, mwenza, mtoto au rafiki kwenye biashara yako kwa sababu hana cha kufanya, jua umenunua matatizo.
Kuna sababu kwa nini mtu huyo hana cha kufanya. Je unadhani biashara yako itaweza kuhimili hali za watu hao wa karibu?

Sisemi tusiwaajiri watu wa karibu kwenye biashara zetu.
Ila ninachosema ni watu wote wanaoajiriwa kwenye biashara, kwanza waajiriwe kwa sifa ambazo nafasi wanayopewa inazitaka.
Na wakishaajiriwa kwenye biashara, wanapaswa kufuata sheria na tararibu zote za kibiashara, bila kujali ukaribu wao.
Na pale wanapofanya makosa kwenye biashara, waadhibiwe kama watu wengine na siyo kupendelewa kwa sababu ni watu wa karibu.

Biashara haijui na wala haijali nani wa karibu yako na nani siyo wa karibu.
Yenyewe inataka misingi fulani ifuatwe.
Misingi hiyo isipofuatwa, biashara itayumba na hata kufa, hata kama uliyemweka kwenye biashara hiyo ni mtoto wako mwenyewe au mwenza wako.
Kila aliye kwenye biashara anapaswa kuiheshimu sana biashara.
Anapaswa kuweka pembeni kabisa mahusiano mliyonayo nje ya biashara.

Kama mtu wako wa karibu, uliyemweka kwenye biashara yako anashindwa kufuata utaratibu wa biashara na hata ukimwambia bado hafuati, unapaswa kumwondoa kwenye biashara hiyo.
Najua hilo linaweza kuwa gumu kwa sababu ya mahusiano mnayokuwa nayo, lakini jua wazi kwamba biashara haiyajui hayo mahusiano yenu.
Biashara inachotaka ni taratibu zilizopo zifuatwe bila ya kuvunjwa.
Ni mtu wako wa karibu sana lakini hafuati taratibu za biashara, hapaswi kuwa hapo.
Tena kadiri unavyochelewa kumwondoa, ukidhani atabadilika, ndivyo madhara yake yanavyokuwa makubwa kwenye biashara.

Mwondoe mtu kwenye biashara kwa vigezo ambavyo vipo wazi kabisa. Iwe ni makosa amefanya au utafatibu ameshindwa kufuata.

Mahali pa gumu ni unafanyaje sasa baada ya kumwondoa mtu wa karibu kwenye biashara?
Maama yataibuka maneno mengi na ya lawama kwako kwamba huwajali watu wako wa karibu.
Utaonekana una roho mbaya kwa kuwanyima watu wako wa karibu kazi, ambao wana uhitaji sana wa kazi.

Kama una ngozi ngumu (ambayo unapaswa kuwa nayo kama unataka mafanikio makubwa) unapuuza hayo yote. Wewe unaendelea kupambana kujenga biashara yako. Utalaumiwa sana mwanzoni, lakini baadaye itakuja kudhihirika wazi nani ni tatizo hasa.

Kama una ngozi nyepesi na hutaki kuonekana una roho mbaya, wafungulie watu hao wa karibu biashara zao wenyewe, ambazo wataziendesha kwa vile wanavyotaka wao.
Unachojua ni biashara hizo zitakufa kwa misingi kutokuzingatiwa.
Lakini utakuwa umeondoa lawama, kwa sababu itaonekana wazi tatizo lipo kwa nani.
Hili utaliweza kama una fedha ambayo upo tayari kuipoteza, maana lazima utaipoteza.

Mahusiano binafsi hayapaswi kuachwa yaathiri biashara.
Kama unampa mtu wa karibu kazi kwenye biashara yako, achukuliwe kama watu wengine na hivyo afanye yale yote yanayotakiwa kufanyika.
Akishindwa anaondolewa kama wengine wanavyoondolewa.
Kama hutaweza kuwa na msimamo wa aina hii, watu wako wa karibu wataziua sana biashara zako, au kuzizuia zisikue.

Ingekuwa biashara ni rahisi kama watu wako wa karibu wanavyodhani, tayari wangekuwa na biashara zao na wasingehitaji kufanya kazi kwenye biashara yako.
Lazima wajue biashara siyo rahisi kama wanavyodhani na wameajiriwa na biashara, siyo wewe. Biashara hiyo itawafukuza pale wanapokuwa mzigo.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe