2931; Utupu hujazwa.
Rafiki yangu mpendwa,
Asili huwa haipendi utupu.
Popote panapokuwa na utupu, asili huwa inakazana kupajaza kwa haraka sana.
Kama umewahi kupangilia eneo fulani vizuri na ukabaki na nafasi, haikuchukua muda nafasi iliyobaki inajaa kwa vitu mbalimbali.
Kama umelima shamba na hukupanda chochote, magugu hupanda kwa wingi bila hata ya wewe kufanya chochote.
Na pia pale unapookoa muda wako kwa kuacha kufanya vitu fulani, unajikuta kuna vitu vingine vingi vimejitokeza vya kufanya.
Asili huwa haipendi utupu, hivyo hukimbilia kujaza kila aina ya utupu unaojitokeza.
Hii ni dhana unayoweza kuitumia vizuri sana na kwa mafanikio makubwa.
Unachopaswa kufanya ni kwanza kujiwekea viwango vya juu kabisa na kutokuvunja viwango hivyo.
Kisha kuondoa yote ambayo haifikii viwango vyako vya juu, iwe ni vitu au watu.
Kinachotokea ni utatengeneza utupu kwa kuondoa vilivyo chini ya kiwango.
Lakini asili haipendi utupu, hivyo itakazana kuujaza.
Sasa kwa kuwa umeshajiwekea viwango ambavyo huvivunji, utupu huo utajazwa na vitu vya viwango ulivyojiwekea.
Kwa dhana hii, hupaswi kuhofia kupoteza vitu au watu ambao hawaendani na viwango vyako, kwani haitachukua muda nafasi inayobaki itajazwa na vitu au watu sahihi.
Unapojiwekea viwango vya watu unaowaajiri, mwanzoni utakosa watu, lakini utupu unaojitengeneza unajazwa haraka sana.
Unapojiwekea viwango vya wateja utakaowahudumia, utaanza kwa kupoteza na kukosa wateja. Lakini baadaye utawapata wateja wengi wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi.
Hii ni kanuni ya asili na inafanya kazi mara zote. Hivyo usiwe na hofu kwamba utupu uliojengeka utabaki wazi milele. Jua haitachukua muda mrefu kabla ya kujazwa na vitu unavyoruhusu.
Muhimu ni kuwa na msimamo kwenye viwango unavyojiwekea kwenye vitu au watu unaokubaliana nao.
Kama kwa sasa umezungukwa na vitu au watu ambao siyo sahihi, anza kwa kubadili viwango vyako kisha visimamie bila ya kuyumba.
Utashangazwa na jinsi utakavyopata vitu na watu sahihi kwa haraka.
Lazima uwe tayari kupoteza kabla hujapata yale unayotaka.
Ipe nafasi kanuni ya kujazwa kwa utupu ikufanyie kazi, ndiyo njia ya kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Kocha Asante Sana kwa somo Hilo nzuri. Utupu hujazwa.
LikeLike