2935; Somo kutoka makaburini.
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa na hofu ya makaburi kulingana na mitazamo na imani ambazo tumejengewa kwenye jamii zetu.
Kuna hadithi nyingi juu ya yanayoendelea kwenye makaburi ambazo siyo sahihi.
Lakini pia kuna mengi ya kujifunza kwenye makaburi, ambayo tukiyaelewa na kuyafanyia kazi, tutaweza kupiga hatua kubwa sana.
Kuna mafunzo maarufu kutoka makaburini.
Kama makaburi yamejaa ndoto nyingi kubwa ambazo hazikutimizwa.
Na pia kamaburi yamejaa watu ambao walikuwa wanasema watafanya kesho, na hiyo kesho hawakuiona.
Hivyo kila unapoona kaburi, hakikisha huzikwi na ndoto zako kubwa na pia chochote unachojiambia utafanya kesho, kifanye mara moja.
Sasa leo kuna somo kubwa zaidi ambalo nataka kukushirikisha kutoka makaburini.
Somo ambalo ukilielewa utaweza kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu wake na bila ya hofu yoyote ile.
Somo hilo ni makaburi yamejaa watu ambao walidhani hawawezi kuondolewa kwenye nafasi zao (indispensable).
Wakati raisi wa kwanza wa Tanzania, Mwl J. K. Nyerere anafariki, kuna watu walisema nchi itaingia kwenye vita na machafuko. Waliona kuondoka kwake ndiyo mwisho wa yote. Lakini nchi imeendelea kuwa na amani na utulivu.
Wakati raisi aliyekuwa madarakani, John Magufuli anafariki dunia, watu walidhani nchi haitaweza kwenda tena, hasa kutokana na mabadiliko mengi aliyokuwa ameyaanzisha. Lakini nchi inaendelea, hata kama siyo kama alivyokuwa anaenda yeye.
Somo kubwa kabisa hapa ni kwamba hakuna mtu ambaye hawezi kuondolewa kwenye nafasi yake.
Hakuna mtu ambaye akiondoka kwenye nafasi yake basi dunia itasimama.
Hayupo kabisa.
Ndiyo kuna vitu vitakosekana pale mtu anapoondoka, lakini maisha yataendelea.
Kuna mambo mawili makubwa ya kuondoka nayo hapa;
Moja, ishi maisha yako kwa ukamilifu wake, pambania ndoto zako na hangaika na yale yanayokuhusu. Usijipe kazi ya ukiranja wa dunia kudhani kila kitu lazima uhusike nacho ndiyo kiende sawa. Ukifa leo, dunia itaendelea kama kawaida na hakuna kikubwa kinachosimama.
Ndiyo kuna watu wataumia na kuathirika kwa kuondoka kwako, lakini baada ya muda, maisha yataendelea.
Mbili ni kwa wale wanaokuambia huwezi bila wao. Yeyote anayekuambia kuna jambo lako huwezi bila uwepo wake yeye, kwanza mcheke. Jikumbushe hili la makaburi na jichekee mwenyewe na kumpuuza.
Iwe ni biashara ambayo mfanyakazi au mbia anakuambia huwezi bila uwepo wake, mpuuze.
Hata kwenye maisha ya kawaida, yeyote anayekuambia kuna kitu huwezi bila yeye, mpuuze kabisa.
Usikubali yeyote akufungie kwenye kitu chochote.
Jua wewe ni kiumbe huru na kwenye haya maisha unaweza kufanikisha chochote bila kuzuiwa na yeyote.
Hili halinaanishi udharau watu na kuwapuuza.
Waheshimu sana watu.
Shirikiana vizuri na watu.
Ila pale wanapoleta ujinga kwamba huwezi bila wao, hapo sasa waonyeshe namna ambavyo wewe ni kiumbe huru.
Wapuuze na fanya bila wao.
Usikubali kuyajenga maisha yako, kazi yako au biashara yako kutegemea ulazima wa uwepo wa watu fulani.
Iwapo kuna kitu umeshakijenga hivyo, kwamba kuna watu wameshakuonyesha huwezi bila wao, chukua hatua mara moja ya kuchukua uhuru wako.
Anza kwa kuwaondoa na kufanikisha bila wao ili ujumbe uwe wazi kwamba hutafungwa na yeyote.
Tunapambana kutafuta haya mafanikio kwa machozi, jasho na damu, ili pia tuweze kujijengea uhuru kamili.
Kuruhusu yeyote au chochote kuwa kikwazo cha uhuru wetu ni kujidharau.
Hebu fikiria, ujibane kupata mtaji wa kuanzisha biashara, uanzishe biashara na kupitia hasara mbalimbali, ukabiliane na taasisi mbalimbali za kiserikali, halafu aje atokee mfanyakazi akiambie bila mimi hii biashara yako haiwezi kwenda!
Yaani huyo ni wa kuanza naye mara moja, kwa kumwondosha na kuhakikisha biashara inakwenda bila kuyumba.
Jenga mfumo ambao hakuna yeyote anakukwamisha popote.
Ndiyo, wapo watakaoweza kukupa vikwazo na changamoto mbalimbali. Lakini wa kukuangusha kabisa, asiwepo hata mmoja.
Huo ndiyo uhuru wa kweli.
Hilo ndiyo tunalolipambania.
Tusijiangushe.
Tujifunze kutoka kwenye makaburi.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Hakika!
Dunia haitasimama.
LikeLike
Ni kweli dunia inajiendesha yenyewe bila kututegemea sisi. Dunia ina mifumo mingi ambayo wala hatuijui inajiendeshaje.
LikeLike
Ni kweli kabisa, sitakiwi kujifanya kilanja wa dunia. Kwani nikiondoka duniani, dunia haitasimama
LikeLike
Dunia haiwezi kusimama kwa ajili ya kutokuwepo kwangu, Muhimu ni kufanya yangu ya muhimu.
LikeLike