2945; Mapigo ya moyo yapo, Anapumua.
Rafiki yangu mpendwa,
Kila mmoja analalamika sana kuhusu changamoto ya wafanyakazi.
Imekuwa vigumu sana kupata wafanyakazi sahihi wa kutusaidia kwenye biashara zetu.
Ni kweli hii ni changamoto kubwa na inayowaathiri watu wengi.
Na pia ni kweli uwezo na umakini wa wengi wanaotafuta kazi upo chini.
Lakini pia hebu turudi upande wa pili, wa sisi tunaoajiri.
Je ni vigezo gani ambavyo umekuwa unatumia katika kuwachuja watu kabla hujawaajiri?
Kama huna vigezo vyovyote, yaani wewe unaajiri yeyote anayetaka kazi, basi unazidi kuchochea tatizo hili kwako mwenyewe.
Kama ukiambiwa kuna huyu ndugu yako hana cha kufanya, mpe kazi ajishikize kwenye biashara yako na wewe unafanya hivyo, maana yake kigezo unachokuwa unatumia ni mapigo ya moyo na upumuaji.
Mapigo ya moyo na upumuaji ndizo sifa pekee ambazo walio wengi wanazitumia kwenye kuajiri.
Yaani wanaajiri mtu yeyote aliye hai, mwenye mapigo ya moyo na anapumua.
Sasa unaweza kujionea wazi hapo, kwa nini changamoto ya wafanyakazi inazidi kuwa kubwa.
Huwezi tu kuchukua yeyote mwenye kutaka kazi na ukategemea upate matokeo bora.
Kitendo tu cha mtu kutokuwa na kazi au kukosa cha kufanya kinapaswa kukupa tahadhari.
Unadhani kama angekuwa bora kweli na mwenye uwezo wa kufanya kazi za kipekee, angekosa kazi za kufanya?
Wakati mwingine tunalalamikia baadhi ya mambo, lakini tunakuwa tumeyatengeneza sisi wenyewe.
Hata kama ndiyo unaanza kuajiri, hata kama huna uwezo wa kulipa mishahara mikubwa, acha mara moja kutumia sifa ya mapigo ya moyo na pumzi.
Usikubali kuajiri mtu kwa sababu tu ana mapigo ya moyo na anapumua.
Anza na kazi unayotaka ifanyike, matokeo unayotaka yazalishwe kisha sifa za mtu anayeweza kuzalisha matokeo hayo.
Kisha weka vigezo vya mtu wa aina gani utachagua kumwajiri.
Baada ya kupanga hayo, sasa unatafuta watu ambao unawapima kwa vigezo ulivyoweka.
Wale ambao hawakidhi vigezo huwapi nafasi. Unaendelea na zoezi la utafutaji mpaka upate aliye sahihi.
Zoezi hili linahitaji kazi na linachukua muda mrefu. Wengi hukwepa kazi hiyo na kuchukua yeyote, na matokeo yanayopatikana yanajidhihirisha.
Jambo lolote kwenye maisha, unapolifanya kwa urahisi, jua kabisa matokeo yake yatakuwa magumu mno.
Na unapofanya jambo kwa ugumu, matokeo yake huwa ni rahisi.
Usikimbilie urahisi, bali nenda kwenye usahihi.
Itakuwa ngumu mwanzoni, lakini itakupa kilicho bora zaidi.
Kwa wafanyakazi ulionao sasa na unawalalamikia hawafanyi kwa usahihi, hebu rudi nyuma na ujiulize ulitumia vigezo gani kuwaajiri?
Kama kigezo chako kilikuwa mapigo ya moyo na pumzi, kama ulichukua tu yeyote, basi jua unastahili kile unachopitia sasa.
Na utaendelea kupitia hizo hali mpaka pale utakapoanza kutumia vigezo sahihi kwenye kufanya maamuzi ya nani wa kumwajiri.
Wenye mapigo ya moyo na pumzi ni wengi, wanaoweza kufanya kazi kwa usahihi ni wachache.
Huwezi kuwapata hao wachache kama hutaweka kazi na muda kwenye zoezi hilo zima.
Na kilicho muhimu sana, usianze na mtu kisha kutafuta sifa ndani yake. Badala yake anza na sifa kisha tafuta aliyenazo na kuweza kuzitumia.
Ni rahisi sana kujidanganya kwamba mtu ana sifa fulani kama utaanza naye kabla ya sifa zenyewe.
Huenda unasoma haya na kuyaelewa, lakini ndani yako unajiambia hao wafanyakazi wenye vigezo hawapo, au wameshamalizwa wote.
Na hapo utakuwa unazidi kujidanganya.
Unataka kuniambia umewamaliza Watanzania wote zaidi ya milioni 60, kisha ukaenda kwenye dunia yenye watu zaidi ya bilioni 8 na kote hujaambulia walio sahihi?
Nadhani unaipata picha, sababu yoyote unayojipa, tunarudi kule kule kwamba unaangalia urahisi na siyo usahihi.
Unapoenda kwa urahisi hivyo, unatengeneza matatizo ambayo baadaye lazima yakukwamishe.
#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Nitaangalia kutenda kwa usahihi, na siyo kuangalia yaliyo rahisi.
LikeLike
Asante Sana kocha KWa ndani mzuri hasa ktk kuajiri wasaidizi wetu wa kazi.
LikeLike
Asante kocha,nitaangalia vigezo sio kujalibu au kutaka urahisi.
LikeLike
Kila la kheri
LikeLike
Kigezo cha mapigo ya moyo na upumuaji..
LikeLike
Nitatengeneza Viwango na kuandaa sifa za mfanyakazi wangu. Kwakweli sikuwahi kuwaza hili kabla
LikeLike
Sifa ndio kitu cha kuangalia kabla ya kugikoria urahisi
LikeLike