2948; Itakugharimu kabla haijakunufaisha.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vitu ambavyo vinawazuia watu wengi wasipate mafanikio makubwa ni kukosa msimamo.
Wanapanga vitu ambavyo watafanya, lakini wanapoanza kufanya na vikawagharimu, huwa wanaacha mara moja.

Kitu ambacho wengi wamekuwa hawajui ni kwamba kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama yake.
Kila maamuzi unayofanya kwenye eneo lolote la maisha yako, huwa yanakugharimu kabla hayajaanza kukunufaisha.

Maamuzi yoyote utakayofanya kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, yatabadili baadhi ya vitu ambavyo tayari ulishazoea kufanya.
Kwa kuacha kufanya vitu hivyo, kuna matokeo ambayo utaacha kuyapata.
Hapo ndipo wengi huona maamuzi waliyofanya ni ya hasara kwao na hivyo kuachana nayo na kurudi kwenye mazoea.

Kwa mfano utakapoamua kuleta mabadiliko kwenye wateja unaowahudumia kwenye biashara yako, mwanzoni utapoteza baadhi ya wateja, kitu kitakachopunguza sana mapato. Lakini hilo linatoa nafasi ya kutengeneza wateja wapya bora zaidi ambao watainufaisha zaidi biashara.

Tuchukulie kukopesha, labda umekuwa na utaratibu wa kuwakopesha wateja wako. Hilo linakupa wateja wengi, lakini pia linakupa kazi mara mbili, ya kuwahudumia wateja kile unachouza halafu kuwafuatilia walipe madeni yao.

Kama utaamua kwamba hukopeshi tena wateja, itaanza kwa kukugharimu. Wateja wengi watapungua kwa sababu hawapati mikopo waliyozoea. Hilo litapunguza kipato, kitu ambacho wengi hawawezi kuhimili na hivyo kurudi kwenye mazoea.

Lakini kama utaweza kuhimili hilo, ukavuka gharama hiyo, utapata manufaa makubwa sana baadaye. Ndiyo wateja watapungua mwanzoni, wale wachache utakaobaki nao utawahudumia vizuri sana, kitu ambacho kitawapa thamani kubwa na kuwavutia wateja wengine wazuri kuvutiwa kuja kwako.
Kwa kuwa unakuwa umeondoa kazi ya kukusanya madeni, nguvu zako zote unazipeleka kuwahudumia vizuri wateja wako.

Pia wale wateja wanaokukimbia kwa mabadiliko uliyoyaleta, wanaenda kwa washindani wako.
Unaweza kuona kama washindani hao wananufaika zaidi yako.
Lakini kumbuka ni wateja wenye changamoto, hivyo unakuwa umepeleka changamoto hizo kwa washindani wako.
Wewe umepunguza matatizo, mshindani wako ameyaongeza, unadhani nani kanufaika?

Naamini unaipata picha rafiki yangu. Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila eneo la maisha.
Maamuzi yoyote ya mabadiliko unayoyafanya, yataanza kwa kukugharimu kabla hayajakunufaisha.
Weka vigezo vya watu wa kujihusisha nao, mwanzo utakosa watu na kushawishika kupunguza vigezo hivyo, lakini kama utaendelea navyo, mbeleni utawapa wengi tu wazuri.

Chochote unachotaka kinawezekana kabisa.
Sema ni vile itaanza kwa kukugharimu kabla haijaanza kukunufaisha.
Kama utakuwa tayari kulipa gharama za awali, hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata unachotaka.

Moja ya kanuni muhimu ya mafanikio ni kusema hapana.
Hapana inakupa nguvu ya kupeleka umakini wako kwenye vitu vichache.
Hilo litakugharimu mwanzoni kwa vile vizuri utakavyoviacha.
Lakini baadaye itakupa faida kubwa kwa matokeo bora utakayozalisha.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe