2971; Uongozi, usimamizi na ufuatiliaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu ambaye anaajiri watu wa kumsaidia majukumu ya kibiashara, anajua changamoto nyingi ambazo anakutana nazo.

Imekuwa ni changamoto kubwa sana kupata wafanyakazi sahihi na kuweza kukaa nao kwenye biashara kwa muda mrefu.

Kumekuwa na maumivu, malalamiko, kukatishwa tamaa na kuvurugwa kwa wengi ambao wanaingia kwenye zoezi la kuajiri.

Wapo ambao wanaona ni bora waachane kabisa na zoezi la kuajiri na warudi kufanya kila kitu peke yao.

Lakini hilo siyo suluhisho, huwezi kukua bila watu. Pamoja na changamoto zao nyingi, bado unawahitaji sana watu.

Kwa muda mrefu tumekuwa tunaliangalia tatizo la wafanyakazi kama tatizo lao na siyo letu.
Tumekuwa tunalalamika wafanyakazi hawajiwezi, hawajui nini wanataka na hawataki kujifunza wala kujituma.
Mwishowe wanashindwa kazi na kukimbia.

Lakini kwenye maisha, kila jambo lina pande mbili. Na hili la changamoto ya wafanyakazi, pamoja na mapungufu waliyonayo, bado pia upande wa waajiri unachangia sana kwenye hilo tatizo.

Ndiyo, wewe unayeajiri pia una changamoto zako ambazo zinachangia wafanyakazi wanakuwa siyo wazuri na hatimaye kukimbia.

Kuna changamoto ya matarajio yasiyo sahihi. Unamwajiri mtu, ambaye haijui biashara yako kama wewe unavyoijua na hana maono makubwa uliyonayo halafu unategemea mara moja aanze kufanya kwa viwango vya juu unavyotaka wewe. Kwa kifupi ni kitu kisichowezekana, wanahitaji muda na mafunzo mpaka waweze kufanya kwa ubora unaotaka.

Pia kuna changamoto ya kushindwa kuelewa mahusiano ya msingi yaliyopo kati ya mwajiri na mwajiriwa. Kwa ndani kabisa haya ni mahusiano ya upinzani. Ajenda zako wewe mwajiri na ajenda za mwajiriwa ni tofauti kabisa.
Wewe unataka unaowaajiri wafanye kazi zaidi kwa malipo kidogo.
Waajiriwa wanataka wafanye kazi kidogo kwa malipo makubwa.
Kwa kushindwa kuelewa mahusiano haya ya msingi na kudhani mko upande mmoja inachangia sana kwenye changamoto zinazojitokeza.

Halafu kubwa kuliko yote ni kushindwa kutekeleza mahitaji makubwa matatu ya kuajiri, ambayo ni uongozi, usimamizi na ufuatiliaji.

Kwenye kuajiri kunahitajika uongozi. Uongozi unahusisha maono, mfano na hamasa. Kama kiongozi unapaswa kuwa na maono makubwa ambayo wafanyakazi wanavutiwa kuwa sehemu ya maono hayo. Unapaswa kuwa mfano kwa kila unachowaambia wafanye, usiwaelekeze tu kufanya, bali waonyeshe jinsi ya kufanya. Na zaidi, unapaswa kuweka morali yao juu kwa kuwapa hamasa endelevu, kuna wakati mambo yatakuwa magumu na wao kuelekea kukata tamaa, wape hamasa, hakikisha morali wao unakuwa juu. Kama wewe kiongozi utaonekana kukata tamaa, unaowaongoza wataona giza mbele yao.

Usimamizi ni muhimu sana kwenye kuajiri. Huwa tunadhani watu wanajua wanachopaswa kufanya, lakini ukweli ni hawajui. Ukiwaacha watu wafanye kile wanachotaka, unajua unachoishia kupata, ambacho ni hakuna, kwa sababu watu wakiachwa kwa utashi wao wenyewe, wanavurugwa na usumbufu na hakuna wanachofanya.
Unapaswa kuwapangia wafanyakazi kile wanachopaswa kufanya na kuwaelekeza namna ya kukifanya. Unapaswa kuwasimamia kwa karibu kuhakikisha kweli wanafanya na hawapotezwi na usumbufu mwingi unaowazunguka. Na pia unapaswa kuwasaidia kuendelea kuwa bora kwenye kile wanachofanya ili wawe na ufanisi mkubwa zaidi.

Ufuatiliaji ni kitu cha tatu muhimu kwenye kuajiri ambacho wengi sana huwa hawakizingatii.
Wengi hudhani kwa kuwa na usimamizi mzuri inatosha kuwafanya wanaowaajiri walete matokeo wanayopata. Na wanakuja kushangaa pamoja na kuwa na usimamizi mzuri, bado matokeo wanayopata siyo mazuri.
Ili kujihakikishia matokeo mazuri kwenye kuajiri, lazima uwe na ufuatiliaji mzuri na wa karibu sana kwenye yale yanayofanywa na wafanyakazi walioajiriwa.
Unaweza kuwaeleza vizuri wanachopaswa kufanya na kuwafundisha jinsi ya kufanya.
Kwa nje wanaweza kuonekana kama wanafanya, lakini matokeo wanayozalisha yakawa tofauti.
Hapo jua kwa ndani hawafanyi kama unavyoona kwa nje.
Ili ujue kile wanachofanya kwa ndani, lazima uwe na ufuatiliaji wa karibu. Lazima uweze kuona kila wanachofanya kwa undani na kujua usahihi wake.
Iko hivi, watu huwa wanaheshimu kile kinachokaguliwa, hivyo haitoshi tu kuwaambia watu cha kufanya, unapaswa pia kukagua ufanyaji wao. Ni kupitia ukaguzi wako ndiyo utaona wapi wanapaswa kuboresha.
Pia pale watu wanapojua wanakaguliwa, wanafanya kwa umakini mkubwa.

Leo kuwa mkweli kwako ili uweze kuvuka changamoto hiyo ya kuajiri inayokuandama.
Ni wapi umekuwa unakosea kama mwajiri?
Je umekuwa na matarajio ambayo siyo sahihi? Unabadilije hilo?
Je umekuwa unashindwa kuelewa mahusiano ya msingi kati ya mwajiri na mwajiriwa? Unakwenda kubadilije hilo?
Na je umekuwa unakosa uongozi, usimamizi na ufuatiliaji? Unakwenda kuchukua hatua gani hapo?

Weka maoni yako hapo chini ya hatua za tofauti unazokwenda kuchukua kwa upande wako ili kupunguza changamoto unazokutana nazo kwenye kuajiri.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe