3021; Haina mjadala.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha yangu sijawahi kusikia mtu anasema amekuwa bize sana kiasi kwamba amekosa muda wa kupumua.
Au mtu kusema ametingwa sana kiasi cha kushindwa kula chochote kwa siku nzima.

Kuna vitu ambavyo hata iweje lazima uvifanye kwenye kila siku yako.
Hata iwe umebanwa kiasi gani, lazima utapumua, utaoga, utakula, utajisaidia na utalala.
Unaumwa, una msiba, umesafiri au kingine chochote, bado utayafanya mambo hayo.

Unajua kwa nini lazima uyafanye mambo hayo?
Ni kwa sababu hayana mjadala.
Huna nafasi ya kuanza kujiuliza kama utafanya au la, jibu ni moja tu, kufanya ni lazima.
Hujiulizi kama una muda wa kuyafanya, ni lazima utenge muda na kuyafanya.

Lakini inapokuja kwenye mambo mengine muhimu kwenye maisha yako, mambo yanayokufikisha kwenye ndoto zako, unaruhusu mjadala.
Unaanza kujiuliza kama una muda au utulivu wa kutosha kuyafanya.
Na pale chochote kinapokuwa hakijakaa sawa kwenye maisha yako, unayaahirisha mambo hayo.

Hapa naongelea mambo kama kujifunza, kufanya kazi kwa kina, kuchukua hatua muhimu unazopaswa ili kufikia ndoto zako na majukumu mengine muhimu kwenye maisha yako.
Unaruhusu mjadala wa iwapo utafanya au la na kwa kuwa ni mambo magumu na ya kukuchosha, kila mara unapata sababu za kutokufanya.
Unajikuta unayasogeza mbele mambo hayo muhimu na kinachotokea ni huyafanyi au hata ukiyafanya siyo kwa uhakika.

Kama unataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, ni lazima uwe na orodha ya mambo ambayo lazima utayafanya kwenye kila siku yako bila ya mjadala.
Yaani kama tu upo hai, lazima uyatengee muda wa kuyafanya.
Haijalishi kama unaumwa, una msiba, umesafiri au umetingwa kiasi gani.
Kama unapata muda wa kupumua, kula na kulala, unapata pia muda wa kuyafanya hayo muhimu.

Watu wanaweza kutofautiana kwenye orodha ya mambo gani ya kufanya kila siku bila mjadala.
Lakini kwa kila anayetaka mafanikio makubwa, lazima mambo haya yawe kwenye orodha yake.
1. Kujifunza vitu vipya, hasa kupitia usomaji wa vitabu.
2. Kuwa na muda wa kufanya kazi kwa kina, hasa kwenye biashara yake.
3. Kuingiza kipato na kujenga utajiri.
4. Kujenga afya ya mwili, akili, roho na hisia.
5. Kujenga na kuimarisha mahusiano na watu wengine wa muhimu kwake.

Mambo hayo na mengine kulingana na mtu ni ya muhimu sana kufanya kila siku bila ya kuruhusu mjadala wa iwapo ufanye au usifanye.

Huianzi siku yako kwa kujiuliza kama utapata muda wa kuyafanya hayo muhimu, badala yake unapanga kwenye orodha yako ya siku ni muda gani utayafanya mambo hayo muhimu.
Ni kufanya kwa msimamo bila kuacha ndiko kunakozalisha matokeo makubwa na mazuri.

Kama kuna kitu chochote kinachoweza kukuzuia usifanye yale ambayo ni muhimu kwako kufanya, kila mara kutakuwa na kitu cha kukuzuia.
Maisha hayatakuachia upenyo wa kuyafanya hayo muhimu, kila wakati utakuwa na kitu cha kukuzuia.

Lakini kama umeondoa kabisa mjadala wa iwe utafanya au la, kama kufanya ni lazima hata iweje, utaziona fursa nyingi za kukuwezesha kufanya.
Akili zetu huwa zina nguvu za ajabu sana, huwa zinatuonyesha kile tunachotaka kuona na kutupa fursa za kukamilisha yale hasa tuliyodhamiria.

Mtu mmoja amewahi kusema kama unataka kufanikiwa kama unavyotaka kupumua, hakuna kitakachokuzuia usifanikiwe.
Leo hii ukiwa na shida yoyote ya upumuaji utahangaika kwa kila namna kuhakikisha unapumua.
Lakini ukikwama kwenye safari yako ya mafanikio, unakata tamaa.
Haipaswi kuwa hivyo, safari yako ya mafanikio ni jambo ambalo halipaswi kuwa na mjadala kwako, ni lazima ufanye yale unayopaswa kufanya ili ufanikiwe, iwe unajisikia kufanya au la.

Ukiruhusu mjadala kwenye mambo muhimu kwako, utapata sababu za kutokuyafanya, kwa sababu mambo yote muhimu ni magumu.
Ukiondoa mjadala utayafanya, hata iweje.
Ondoa mjadala na kila siku weka kwenye orodha ya mambo muhimu kukamilisha na yakamilishe kama vile umewekewa bastola kwamba usipofanya inavyatuliwa.

Ni nidhamu ya viwango hivyo ndiyo itakayokufikisha kwenye mafanikio makubwa na unayoyataka.

Swali muhimu sana kwako ni hili; je ni mambo gani matatu ambayo lazima utayafanya kila siku ya maisha yako bila ya kuruhusu mjadala wowote wa iwe utafanya au la?
Yangu ni KUSOMA, KUANDIKA na KUFUNDISHA/KUKOCHI.
Shirikisha matatu yako kwenye maoni hapo chini.
Na kwenye kila siku yako onyesha ushahidi kwamba umeyakamilisha mambo hayo matatu muhimu kwako, kupitia orodha ya mambo yako ya kukamilisha kwenye siku na tathmini zako za kila siku.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe