Kila mmoja wetu kuna magumu fulani ambayo anapitia kwenye maisha yake. Na kwa binadamu ni kitu cha kawaida kabisa lakini sisi binadamu pale mambo yanapokuwa shwari tunasahau kama kuna magumu ambayo tunaweza kukutana nayo. Kwa mfano, kama kwa sasa unafurahia jua na kinyume chake kinakuhusu.
Falsafa ya Ustoa inatufundisha kuwa mabaya na mazuri yote ni sehemu ya maisha yetu. Kila mmoja anapaswa kulijua hilo, hakuna mtu ambaye atapitia mazuri tu kwenye maisha yake, na mabaya yasimkute.
Chukulia mfano wewe kama mfanyabiashara, faida na hasara ni sehemu ya biashara. Lakini , kama wewe ni mtu unayeangalia faida tu, basi jua na hasara pia inakuhusu. Kumbe basi, faida na hasara ni sehemu ya maisha pale tunapochukulia maisha yetu ni kama biashara.
Kuna baadhi ya watu hujiona kwamba wao hawastahili kupata magumu, lakini magumu ni sehemu ya kila mmoja wetu. Na siyo kwamba kuwa mstoa maana yake ni kutokuwa na hisia hapana, ndiyo maana tuna misingi kama vile UJASIRI, ujasiri ndiyo unakusaidia wewe kupambana na yote unayokutana nayo maana bila ujasiri, maisha yatakushinda na utaona duniani siyo sehemu ya kuishi.
Wiki iliyopita tulijifunza kwamba kiasili hakuna kitu kibaya wala kizuri ila tafsiri zetu ndiyo zinaamua kitu kiwe kizuri au kibaya. Mwanafalsafa Marcus Aurelius aliwahi kunukuliwa akisema, ukichukulia mtu amekuumiza na utaumia na ukichukulia kwamba mtu hajakuumiza na wala hutoumia. Hapa tunaondoka na somo kwamba, maono yetu binafsi juu ya kitu chochote kile ndiyo yanaamua sisi tuumie au tusiumie.
Magumu na changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Lakini pale yanapotokea huwa yanatuumiza sana kwa sababu mara nyingi tunakuwa hatutegemei yatokee. Seneca anasema kujenga kitu kunachukua juhudi kubwa na muda mrefu. Lakini kubomoa kitu ni rahisi sana na kwa muda mfupi.
Wote tumewahi kupitia magumu mbalimbali kwenye maisha ambayo kwa sehemu kubwa ni kupoteza vitu au watu tuliokuwa tunawahitaji na kuwategemea sana. Seneca anatushirikisha njia bora ya kukabiliana na magumu hayo ili yasivuruge kabisa maisha yetu. Maana bila njia bora ya kuyakabili, ni rahisi yakavuruga maisha yetu na kutukosesha furaha.
Njia ya kwanza ni kutambua wema pekee ndiyo kitu bora. Hapa Ustoa unatukumbusha kurudi kwenye asili yetu binadamu ambayo ni viumbe wa kufikiri. Hivyo tunapaswa kuziweka fikra zetu vizuri na tusitawaliwe na hisia zozote mbaya. Kwani kinachofanya mambo yaharibike wakati tunapitia magumu ni tunaporuhusu kutawaliwa na hisia.
Njia ya pili ni kutambua baadhi ya mambo yapo nje ya uwezo wetu kabisa. Kwamba tunaweza kufanya kila tunachopaswa kufanya lakini bado tukakutana na magumu kwa sababu kuna yaliyo nje ya uwezo wetu yanayokuwa yameingilia. Ni muhimu kujua mambo yapi yako ndani ya uwezo wetu na kuyafanyia kazi, huku yale yaliyo nje ya uwezo wetu kuyapokea kama yalivyo.
Kwa kutumia njia hizi mbili kwa pamoja, hakuna gumu lolote linaloweza kututikisa, kwani tunafikiri kwa usahihi na kujua yaliyo nje ya uwezo wetu hatuna namna ya kuyaathiri.
Hata pale magumu yanapotokea hatupati taharuki au kuumia sana kwa sababu siyo kitu kinachokuja kwetu kwa mshangao kwa sababu tulishajiandaa kwamba magumu yapo.
Hatua ya kuchukua leo; usikubali magumu yakutawale, badala yake yakabili yale ambayo yako ndani ya uwezo wako na yale ambayo yako nje ya uwezo wako iachie asili au wenyewe mamlaka wapambane nayo.
Wewe kama mstoa, yachukulie magumu kama kitu cha kupita, ishi kwa tahadhari kwamba chochote kile ambacho una miliki sasa siyo chako, bali umeazimwa kwa muda tu na siku ukiambiwa urudishe kwa wenyewe usishtuke.
Chukulia biashara, familia, ndugu na vyote unavyomiliki iko siku utavipoteza, na siku vikija kuondoka hutapata mshangao au mshtuko wa kutokea kwa sababu tayari ulishavuta picha ya namna hiyo itatokea.
Tukutane wiki ijayo, ambapo tutajifunza namna ya kujiandaa na magumu na fursa ndani ya magumu. Usipange kukosa.
Rafiki na Mstoa mwenzako,
Mwl. Deogratius Stanslaus Kessy
ahsante mwl deo ukiwa mstoa hakuna suprise.
LikeLike
Asante Mwl Deogratius kwa falsafa hii nzuri inayotuandaa kwa kupokea mazuri na mabaya kama sehemu ya maisha.
LikeLike
Asante sana kwa msingi huu mhimu wa hakuna mazuri tu kuna. Mabaya pia yapo na yanaweza kutokea
LikeLike
Asante sana Mstoa Deo Kessy, haya mafunzo yamefika kwangu wakati sahihi na nitaiishi hii misingi ya USTOA
LikeLike
Asante sana kwa Elimu nzuri ya ustoa,ktk maisha bila kujiandaa kukabiliana na magumu itakuwa shida, vinginevyo utakuwa mtu wa kulalamikiwa na kulaumu kumbe vingine ni asili inafanya kazi yake.
LikeLike