3043; Roho mbaya.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vikwazo vikubwa kwenye safari ya mafanikio ya wengi ni jamii inayokuwa inamzunguka.
Jamii hiyo inapokuwa na watu ambao hawana mafanikio wala hawapo kwenye safari ya mafanikio makubwa, inazuia watu wengine wasiyapambanie mafanikio.

Kwa kuwa safari ya mafanikio inamtaka mtu ajitoe sana na kusema HAPANA kwenye mambo mengi, jamii haiwakubalii kirahisi wale wanaotaka kufanikiwa.
Jamii inakuwa haikubali mtu yeyote awe tofauti na jamii hiyo.
Hivyo inatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha watu wote wanabaki kuwa sawa.

Na njia kubwa kabisa ambayo jamii huwa inatumia sana ni kuwateka watu kihisia, hasa hisia za lawama, hatia na majuto.
Jamii huwalaumu wale ambao wanakwenda tofauti na kuwafanya wajione wana hatia kubwa ili kuwajengea majuto.
Jamii inawafanya wale wanaopambana kufanikiwa wajione kama ndiyo kikwazo kwa jamii nzima.

Moja ya njia kubwa ambayo jamii inatumia kwa watu wanaotaka kufanikiwa ni dhana ya roho mbaya.
Jamii inawaona wale wanaopambana kufanikiwa kama watu wenye roho mbaya sana.
Kwa sababu wanaweka kipaumbele zaidi kwenye mambo yao na kusema hapana kwenye mambo ya wengine, wanashutumiwa kuwa na roho mbaya.

Wale wenye mioyo myepesi, ambao ndiyo wasiofanikiwa huwa wananasa kwenye mtego huo. Kuona kweli kwamba wana roho mbaya kwa kuamua kuyaishi maisha yao na hivyo kubadilika na kufuata mkumbo wa jamii.
Wanachokuwa wamefanya ni kutaka kuonekana wana roho nzuri kwa jamii, ila ukweli ni wamechagua kuwa na roho mbaya kwao wenyewe.

Kuna vitu viwili vikubwa sana unavyopaswa kujua kwenye dhana hii ya roho mbaya ili uweze kuwa huru.

Kitu cha kwanza ni dhana nzima ya roho mbaya ni mtego unaokuwa umewekewa. Watu huwa wanaona mtu mwenye roho nzuri ni yule anayekubaliana nao na wanajufaika moja kwa moja kutoka kwao na watu wenye roho mbaya ni wale wanaofanya mambo yao, ambao hawawapi kile wanachotaka kwa namna wanavyotaka wao.
Hivyo roho mbaya siyo kile unachofanya wewe, bali mategemeo ya watu kwako.
Watu ni wabinafsi, wanapoona huwapi kile wanachotaka wao, wanakuona ni mbaya, hata kama hakuna lolote baya unalofanya.

Kitu cha pili ni lazima mategemeo ya upande fulani yapuuzwe ili maisha yaweze kuendelea. Kwa mfano kama kila mtu anataka kupata muda wako na ukampa kila mtu dakika 10 kwenye siku yako, siku nzima utaimalizia kwa watu. Kwa watu hao utaonekana una roho nzuri, lakini kwa upande wako mwenyewe utabaki kuwa na roho mbaya, kwa sababu umepuuza kutekeleza yale muhimu zaidi.
Hivyo inabidi uchague kuwa na roho mbaya kwa wengine, kwa kuweka vipaumbele kwenye mambo yako au uwe na roho mbaya kwako mwenyewe kwa kuweka vipaumbele kwenye mambo ya wengine.

Kwa kifupi, kama lengo lako ni kutokuonekana una roho mbaya kwenye maisha, hiyo yenyewe tayari ni roho mbaya kwako mwenyewe.
Utakazana kumridhisha kila mtu, ila utaishia kujipuuza wewe mwenyewe.
Huwezi kufanikiwa kwa kutaka kumridhisha kila mtu kila wakati.
Anza kwa kujiridhisha wewe mwenyewe na utaweza kuwaridhisha wale wanaoendana na wewe baada ya kuwa umefanikiwa.

Hili halimaanishi kwamba uwafanyie watu ubaya ili kufanikiwa.
Bali linamaanisha uweke kipaumbele kwenye mambo yako na kupuuza mengine yote ambayo watu wanataka kukuteka nayo ili uachane na ndoto zako kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe