3044; Hofu na majuto.

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio yoyote yale kwenye maisha yanaanzia kwenye misingi fulani ambayo huwa inajengwa na kila mtu anayehusika kwenye eneo hilo.

Mafanikio pia huwa yanahusisha kufanya mambo mapya ambayo ni tofauti kabisa na mazoea yaliyopo kwenye ebeo husika.

Inapokuja kwenye ufanyaji wa mambo hayo mapya, huwa kuna hisia kuu mbili zinazomzonga mtu; hofu na majuto.

Mtu anakuwa anahofia kuchukua hatua kwa sababu ya matokeo yasiyo ya uhakika yanayoweza kupatikana.

Lakini pia mtu anakuwa anafikiria majuto atakayokuwa nayo pale mambo yatakapokwenda tofauti na mategemeo.

Ili uweze kufanya maamuzi bora na yatakayoacha alama hapa duniani, unapaswa kufanya maamuzi kwa kupunguza majuto badala ya kuridhisha hofu.

Hofu ni kitu cha muda mfupi kwenye maisha yetu. Unaweza kuwa unahofia kufanya kitu fulani, lakini hofu hiyo itakuwa ya muda mfupi. Wale wanaoweza kuzivuka ndiyo wanaoweza kutengeneza matokeo makubwa.

Majuto ni kitu cha muda mrefu, ukishakuwa na majuto unaweza kwenda nayo kwa kipindi chote cha maisha yako. Majuto yanafanya mtu aone kama angechukua hatua fulani huko nyuma, basi matokeo yangekuwa ya tofauti.

Kwa dhana hizo mbili, kuna moja ina nguvu kubwa sana kwenye mafanikio.
Dhana hiyo ni kufanya maamuzi kwa kupunguza majuto yanayoweza kujitokeza mbeleni.

Kwenye kufanya maamuzi yoyote yale, hofu huanza kumkwamisha mtu, kumfanya aone anakosea.
Wengi huipa hofu hiyo nguvu na hivyo kushindwa kuchukua hatua.
Lakini wanachobaki nacho ni majuto ya muda mrefu sana.
Kila mara watajutia kwamba kama wangechukua hatua, matokeo yangekuwa tofauti.

Kuanzia sasa, jiambie kamwe hutakuja kukwama kufanya kitu kwa sababu ya hofu yoyote ile. Kwa sababu hofu ni kitu cha muda mfupi na cha kupita.
Kwa maamuzi yoyote unayoyafanya, jiulize ni yapi yatakuletea majuto kidogo zaidi baadaye. Ni nini hasa utajutia sana baadaye kama utafanya au kutokufanya kile unachopaswa kulipa?

Usikubali kabisa hofu ya muda mfupi ikutengenezee majuto ya muda mrefu kwenye maisha yako.
Kama kuna kitu ambacho unaona ni muhimu kufanya, basi kifanye kweli, hata kama kuna hofu iliyopo nyuma ya kitu hicho.
Majuto ya kutokufanya kabisa ni makubwa kuliko hofu ya wakati wa kufanya kitu, hasa kinapokuwa ni kitu kipya.

Wewe kuwa mchukuaji wa hatua hata kama kuna hofu kubwa unayokuwa nayo. Kuwa tayari kukabiliana na hofu yoyote ile kuliko kuwa na majuto ambayo utaenda nayo kwa muda mrefu kwenye maisha yako.

Kujenga maisha bora na ya mafanikio makubwa, punguza majuto unayoyatengeneza. Chukua hatua hata kwa mambo unayopaswa kufanya ni mapya na unayahofia.
Ni bora ukabili hofu kuliko kukabili majuto.
Fanya unachohofia sasa ili baadahe usiwe na majuto.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe