3045; Afya yako ya akili.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya mafanikio, afya yako ya akili ni rasilimali muhimu sana unayopaswa kuilinda.

Safari ya mafanikio imejaa vikwazo na changamoto za kila aina.
Usipokuwa imara kuvuka hayo, yatakuchosha haraka sana na kujikuta ukikata tamaa.

Ili kuimarisha afya yako ya akili, zingatia mambo haya yafuatayo;

1. Usiwe na matarajio makubwa sana kwa watu wengine. Kadiri unavyokuwa na matarajio makubwa, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kuangushwa.

2. Usiwe na mategemeo makubwa kwenye mambo ambayo yapo nje ya uwezo wako.

3. Jua hakuna mtu aliyekamilika, kila mtu ana changamoto zake. Hivyo nenda na wale ambao manufaa wanayokupa ni makubwa kuliko changamoto zao.

4. Waamini watu, lakini wape nafasi ya kukosea au kukuangusha kwenye yale unayowaamini.

5. Jua kila mtu ana maslahi yake binafsi na kila anachofanya ni kuhakikisha anayatimiza maslahi hayo.

6. Usiseme wala kufanya chochote ukiwa na hisia kali za hasira au furaha.

7. Usiwe na kinyongo na mtu yeyote yule, hata kama amekufanyia nini. Kama kuna watu umeona hawakufai tena kwenye safari yako ya mafanikio, wafute kwenye fikra zako, ila endelea kuwaheshimu kwa utu wao. Usitake kumkomoa yeyote, peleka muda wako kwenye mambo muhimu kwako.

8. Unapoomba ushauri jiulize kama unataka kweli kusikia vitu tofauti au unataka mtu wa kukubaliana na mawazo uliyonayo.

9. Unapotoa ushauri jiulize kama unayempa anataka kusikia vitu vipya au anataka ukubaliane na mawazo yake.

10. Maneno kidogo, kazi zaidi. Watu hawasikilizi sana unachosema, bali wanaangalia sana unachofanya.

11. Tekeleza zaidi ya ulivyoahidi. Pambana sana usivunje ahadi ulizotoa.

12. Jua hakuna anayeyafikiria maisha yako kama wewe. Hakuna anayekujali kuliko wewe mwenyewe.

13. Chagua vyema watu unaoshirikiana nao, ili wawe na mchango sahihi kwako. Usichukue mtu ni mtu, kuwa na vigezo unavyotumia kuchagua watu utakaoshirikiana nao.

14. Jua kila mtu anadanganya, kila mtu, hasa wale wanaosema ni wakweli watupu. Watu ni wabinafsi na wanaweka mbele maslahi yao kwa namna yoyote ile, hata ikibidi kwa kudanganya.

15. Huoni vitu kama vilivyo, bali unaviona jinsi ulivyo wewe. Unachoona wewe ni tofauti na wanavyoona wengine.

16. Kazi ndiye rafiki wa kweli, ambaye hawezi kukuangusha. Penda sana kazi yoyote unayoifanya.

17. Epuka starehe zenye raha ya muda mfupi, vitu kama ulevi vitakuchosha sana.

18. Puuza mambo yote ambayo hayana mchango kwako kupata kile unachotaka. Weka juhudi zako kwenye mambo machache na yenye tija.

19. Kabla hujafanikiwa watu watakudharau sana, ukifanikiwa watu watakuchukia sana.

20. Kuwa na muda wa kufanya tahajudi (meditation) na tafakari mbalimbali. Hii inatuliza sana akili yako.

21. Kuwa na muda wa kuyaandika mawazo yote unayokuwa nayo kwenye akili yako.

22. Wasamehe watu hata kama hawajakuomba msamaha. Waombe watu samahani hata kama kosa siyo lako moja kwa moja.

23. Unapokuwa na hofu kwenye jambo lolote jua ni hali ya kawaida unapokuwa unakabiliana na mambo mapya, usiruhusu hofu iwe kikwazo kwako kufanya.

24. Kuwa wewe na walio sahihi kwako watakuelewa. Usitake kumridhisha kila mtu, hilo huliwezi.

25. Kuwa na subira, mambo yote mazuri yanahitaji muda kujijenga.

26. Usijilinganishe na mtu yeyote yule, hakuna unachofanana na wengine.

27. Usiruhusu watu wakajua kila kitu kuhusu wewe, hasa matatizo na changamoto zako, wengi watafurahia hali hiyo. Na hata wakijua mafanikio yako, itawajengea tu wivu.

28. Sema HAPANA kwenye mambo yote ambayo hayana mchango kwenye kuyafanya maisha yako kuwa bora.

29. Huwezi kumbadili mtu yeyote, hata ufanye nini. Watu wanabadilika kama wataamua wao wenyewe.

30. Vitu vitatu ambavyo hupaswi kuviweka wazi kwa kila mtu; afya yako, utajiri wako na mahusiano yako ya ndoa/mapenzi.

Afya yako ya akili ni kitu cha kukipa kipaumbele kikubwa sana. Kila wakati jikague kwenye afya yako ya akili, kupitia kuyaandika mawazo unayokuwa nayo na kuchukua hatua sahihi za kujenga utulivu ndani yako na kujali mambo yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe