3048; Usinipange.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mwenendo fulani ninaouona kwa watu wanaokuwa wananiomba ushauri kwenye mambo mbalimbali.
Mtu anaelezea jambo lake jinsi lilivyo na kuomba ushauri wa hatua gani za kuchukua.

Tunajadiliana namna bora ya kulikabili jambo linalokuwa mbele ya mtu na kufikia tamati ya hatua sahihi za kwenda kuchukua.
Lakini sasa cha kushangaza, mtu anakwenda kuchukua hatua za tofauti kabisa na zile tulizoshauriana.

Kumbe mtu anakuwa ameshapanga kabisa nini anataka kufanya kwenye jambo husika.
Anapokuja kwangu kwa ushauri ni kama anataka tu mimi niyabariki maamuzi yake.
Ili ajiridhishe kwamba hata Kocha pia amekubaliana na hili.

Huko ni kunipanga,
Na haitafanya kazi,
Kwa sababu huwezi kunipanga.
Unapokuja kwangu kwa ushauri, sitakuambia kile unachotaka kusikia, bali kile unachopaswa kusikia.
Tutajadiliana kwa kina umefikaje pale ulipo sasa na ipi njia bora ya kutoka.
Halafu kwa pamoja tutaafikiana zipi hatua za kuchukua na wapi unakwenda kuanzia.

Simaanishi kwamba nakupangia namna ya kuendesha mambo yako.
Na wala sikulazimishi ufanyie kazi ushauri wowote ninaokupa.
Lakini kama umekuja kwa ushauri, halafu tukashauriana jambo fulani na ukakubali utakwenda kufanyia kazi yale tuliyoshauriana, lakini ukaenda kufanya kinyume kabisa, hilo halijakaa sawa.
Ni kupotezeana muda wa kujadili vitu ambavyo unajua kabisa huendi kufanyia kazi.
Kwa nini tusiokoe huo muda na ukaendelea na mpango ambao tayari upo?

Ninachosema ni kama una changamoto au hali fulani unayopitia na tayari ndani yako una maamuzi fulani unayotaka sana kuyafanya, endelea na maamuzi hayo.
Kama tayari unaona nini unataka kufanya na haupo tayari kufanya kitu cha tofauti, okoa muda wa kufanya kitu hicho.

Usijaribu kunipanga mimi, kwa kuniomba ushauri kimtego, ukiweka upendeleo fulani kwa kile unachotaka kufanya ili nikibariki.
Hilo halitafanya kazi.
Unaweza kujifanganya wewe mwenyewe kadiri unavyotaka.
Lakini ukija kwangu, sitaungana na wewe kwenye kujidanganya.
Sitakuambia kile unachotaka kusikia.
Badala yake nitakuambia kile unachopaswa kusikia.
Bila ya kujali kinakuumiza kiasi gani.

Siyo kwamba ushauri nitakaokupa mimi ndiyo wa uhakika kwa asilimia 100 kwamba utafanya kazi na hautaleta changamoto.
Bali ni ushauri ambao umezingatia pande zote za jambo, faida na hasara.
Na kufikia hatua yenye unafuu kuchukua, ambayo bado itakuwa na changamoto zake pia.

Uko huru kuyaishi maisha yako vile unavyotaka,
Una uhuru wa kufanya au kutokufanya chochote unachopanga.
Lakini inapokuja kwamba umeomba ushauri kwenye jambo, na ukakubaliana na ushauri huo, haina maana kwenda kufanya kitu kingine cha tofauti kabisa.
Kama unajua kabisa hutaenda kufanyia kazi ushauri unaopewa, ni bora kueleza wazi kwamba hutatumia ushauri huo.

Kama lengo lako la kuomba ushauri ni kutaka tu kusikilizwa ukijieleza, lakini la kufanya tayari unalo, ni vyema kueleza hilo wazi kabisa.
Usijifiche nyuma ya kichaka cha ushauri kwa kutaka kupitisha ajenda zako binafsi.
Kwa hilo utakwama.

Ningekuwa sikupendi, ningekuambia kile unachotaka kusikia.
Lakini kwa kuwa nakupenda, ninakuambia kile unachopaswa kusikia.
Hata kama kinaumiza, lakini angalau kuna msingi unakuwa umetumika kwenye kuyafikia maamuzi husika.

Mimi kama kiongozi wako sitaendeleza uongo unaojidanganya nao mwenyewe.
Sitakuwa kama wengi ambao wanakuzunguka, ambao hawapo tayari kukuambia ukweli pale unapokuwa unakosea.
Nitakueleza wazi vile ilivyo, iwe utajisikia vizuri au vibaya.
Na nategemea na wewe utetee hoja zako na unishawishi kwa nini kile unachotaka wewe ni bora kuliko kile kilichozingatia manufaa ya pande zote mbili.
Na hatimaye tunafikia tamati ya hatua za kwenda kuchukua juu ya jambo fulani.

Usinipange,
Kwa sababu sipangiki.
Kama kuna kitu unataka sana kukifanya, kifanye.
Kama upo njia panda, hujui kipi ufanye na kipi usifanye, karibu tushauriane.
Na kwenye kushauriana, kuwa wazi kwenye maazimio yanayoafikiwa.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu wengine wote unaowaomba ushauri.
Usiende ukiwa tayari na mpango wako na unachotaka ni wakubariki.
Nenda ukiwa na akili iliyo wazi kwa ajili ya kujifunza na kuliona jambo kwa mtazamo wa tofauti.
Ni mtazamo huo wa tofauti ndiyo unaochangia kufikia maanuzi sahihi ya namna ya kukabiliana na jambo husika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe