3050; Wateke.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye malengo makubwa matatu tunayoyafanyia kazi kwenye kujenga biashara, yaani MFUMO, TIMU na WATEJA, lengo la TIMU ndiyo limekuwa gumu zaidi.

Kila ambaye ameshachukua hatua kwenye kujenga timu, amekutana na changamoto nyingi sana.
Changamoto ya kwanza ni kukosekana kwa watu sahihi ambao wanaweza kutekeleza majukumu yaliyopo.
Changamoto ya pili ni uzembe, uvivu na kutokupenda kujifunza kwa wale wachache wanaoonyesha dalili za kuweza kuwa sehemu ya timu.
Na changamoto ya tatu ni kutokukaa kwao kwa muda mrefu kwenye kazi pale wanapopewa nafasi.

Changamoto ya kwanza na ya pili hatutazizungumzia hapa, kwa hakika hatuhitaji hata kuzizungumzia, kwa sababu kama mtu hawezi kazi, ni mzembe, mvivu na hapendi kujifunza, huyo hapaswi hata kupewa nafasi.
Kama atapewa nafasi kwa sababu hakuna sahihi wanaopatikana kwa wakati huo na uhitaji upo, iwe ni kwa kushikiza tu, wasiwekewe matumaini makubwa.
Najua unaweza kuwa na matumaini kwamba mtu atabadilika, lakini usijiweke kwenye kuvunjika moyo.

Sasa tuje kwenye changamoto ya wale sahihi wanaopatikana kutokukaa kwenye nafasi zao kwa muda mrefu.
Hawa ni wale ambao angalau wana afadhali, wanaweza wasiwe kamilifu kama wanavyohitajika, lakini angalau wanajituma na wapo tayari kujifunza.
Lakini sasa, wakati wewe unategemea uwajenge kwa ajili ya muda mrefu, unakuja kugundua nao wanatafuta mahali pengine pazuri pa kwenda.

Hili ni jambo linaloumiza sana, wewe umeweka imani kwa mtu na umejitoa kumwendeleza ili awe bora na kufanya vizuri. Lakini yeye anakuwa anatafuta mahali pengine pazuri zaidi.

Hilo linaweza kukufanya uwaone ni wasaliti, ambao hawajajitoa kweli kwenye majukumu unayowapa.
Unaweza kutaka kuwaondoa kwenye kazi kwa sababu unaona hawawezi kudumu.

Lakini nataka nikuambie hupaswi kutaharuki kwa sababu ya hilo.
Kama mfanyakazi uliyekuwa unamtegemea umegundua anatafuta kazi mahali pengine, furahi.
Furahi kwa sababu anaamini anaweza kufanya zaidi ya majukumu ambayo umempa.
Angekuwa haamini anaweza zaidi, asingefikiria kingine nje ya kazi uliyompa.

Jambo jingine kubwa kabisa ni kuwa tu mkweli kwako.
Kama wewe ndiyo ungekuwa umeajiriwa kwa mtu mwenye biashara kama yako, anayeiendesha jinsi unavyoendesha biashara yako, ungekuwa tayari kuweka matumaini yako hapo kwa miaka 30 ijayo?
Yaani mtu anaendesha biashara bila ya mfumo wowote, maamuzi yote yanatoka kwenye kichwa chake, tena kwa kuchochewa na hisia na hakuna mpango wowote wa ukuaji unaofanyiwa kazi.
Je ungekaa kwa kujiamini kabisa kwamba hapo ndiyo umefika mwisho wa maisha yako?
Kama utakuwa mkweli, jibu ni hapana.

Na hapo sasa ndiyo nataka nikupe mpango ambao utakusaidia kuwabakisha wafanyakazi wazuri kwenye biashara yako kwa muda mrefu.
Mpango huo ni kuwateka.
Ninaposema uwateke simaanishi uwakamate na kuwafungia kwa nguvu kwenye biashara yako.
Badala yake uwawekee mtego ambao utawanasa na wasiwe tayari kuondoka hata pale wanapopata nafasi mahali pengine.

Njia ya uhakika ya kuwateka binadamu, ni kuwapa uhakika. Hakuna kitu ambacho watu wanakipenda kama uhakika.
Ndiyo maana watu huwa tayari kukaa kwenye kazi inayowalipa mshahara kidogo kuliko kwenda kufanya biashara yenye fursa ya kuwaingizia kipato kikubwa.
Mshahara, japo ni mdogo unakuwa wa uhakika kila mwezi, tofauti na faida ya biashara isiyokuwa ya uhakika.

Ili kuwateka wafanyakazi na kuweza kujenga timu imara ya kukuza biashara, wape uhakika kwenye maeneo haya matano.

1. Mshahara
Mshahara huwa ndiyo kitu cha kwanza kwa wengi kuangalia.
Na huu siyo lazima uwe mkubwa sana, lakini muhimu ni uwepo uhakika wa kuupata mshahara huo.
Kiasi chochote kile ambacho mmekubaliana, wape uhakika kwa kuwalipa mara zote kama mlivyokubaliana.
Walipe kwa ukamilifu na kwa wakati.
Hilo litawajengea utegemezi fulani.
Nasim Taleb amewahi kusema kuna vitu vitatu ambavyo vina uraibu mkali sana, ambavyo ni sukari, madawa ya kulevya na mshahara wa kila mwezi.
Watu wakishauzoea wanakuwa na uraibu nao na kutokutaka kuukosa.

2. Ndoto kubwa
Watu wengi hawana ndoto zozote kubwa kwenye maisha yao, wala hawaamini wanaweza kufanya makubwa.
Hivyo wanapopata mtu mwenye ndoto kubwa na ambazo zina matumaini ya kufikiwa, wanakuwa tayari kuambatana naye.
Ni muhimu kuwapa watu uhakika kwenye ndoto kubwa kwa kuzungumzia ndoto hiyo kila mara na kuwa na mkakati wa jinsi ya kuifikia.
Wafanye watu waone wana mchango mkubwa kwenye kufikia ndoto hiyo na watakuwa tayari kujitoa sana.

3. Mfumo
Hakuna kitu ambacho kinawavuruga watu kama kukosekana kwa utaratibu wa jinsi mambo yanavyopaswa kufanyika.
Hilo linawafanya washindwe kujua kama wanafanya kwa usahihi au la, kitu kinachowanyima kujiamini.
Uwepo wa mfumo unawapa watu uhakika wa jinsi mambo yanavyopaswa kufanyika.

4. Misingi
Ni muhimu sana kuwepo na misingi ambayo inasimamiwa kwenye biashara. Misingi hiyo ndiyo inayokuwa inawaongoza watu wote kwenye biashara na hakuna mtu yeyote anayekuwa juu ya misingi hiyo.
Hilo linawapa watu uhakika wa mambo kufanyika kwa usahihi na siyo kwa mihemko.
Misingi inapofuatwa, changamoto nyingi hukwepeka.

5. Jamii
Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na hivyo huwa tunapenda sana kuwa ndani ya kundi fulani.
Kwa kujenga jamii bora ya wale wanaofanya kazi kwenye biashara yako, kunawavutia watu kupenda kubaki ndani ya jamii hiyo.
Hilo linawafanya watu kuwa tayari kubaki kwa muda mrefu kwa sababu wanapenda kuwa ndani ya jamii husika.

Maeneo hayo matano yana nguvu ya kuwajengea wafanyakazi uhakika ambao unawafanya wakae kwenye biashara kwa muda mrefu.
Kazana kuyajenga mambo hayo kwa msimamo kwenye biashara yako ili uweze kujenga timu bora.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe