3052; Siyo unachotaka, bali unachotoa.

Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kila mtu kwenye maisha anataka kupata mafanikio makubwa.
Lakini kwenye uhalisia ni watu wachache sana wanaopata mafanikio makubwa wanayoyataka.

Tafiti nyingi zimefanywa ili kujua nini kinawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Vitu vingi vya nje ambavyo wengi walidhani ndiyo vinawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa, vimeonekana kutokuwa na mchango.

Mafanikio yameonekana kuwepo kwenye kila eneo na kwa kila aina ya watu.
Kwenye mazingira ya aina moja, kuna watu wanafanikiwa sana na kuna watu ambao wanashindwa.

Matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa kwenye eneo la mafanikio zinaonyesha tofauti za wanaofanikiwa na wanaoshindwa zinaanzia ndani ya mtu.

Maisha ni mwendelezo wa kutoa kafara.
Ili kupata kitu chochote kile unachotaka, lazima uwe tayari kutoa kitu fulani kinachohitajika sana.
Hivyo basi, inapokuja kwenye mafanikio, swali muhimu zaidi siyo nini unachotaka, bali nini upo tayari kutoa kafara ili kupata unachotaka.

Kujua unachotaka ni hatua ya kwanza, ambayo wengi wamekuwa wanaijua hatua hii, hata ambao hawafanikiwi.
Kujua kafara ya kutoa na kuwa tayari kuitoa kafara hiyo kwa jinsi inavyopaswa kutolewa ni hatua ya pili muhimu, ambayo wachache sana ndiyo wanaifanyia kazi.

Ni jambo la kushangaza sana jinsi ambavyo watu wengi wanavyotaka mafanikio kwenye maisha yao, lakini watu hao hao wakiwa hawapo tayari kubadilika.

Mafanikio pia huwa yanakuja kwa ngazi na awamu.
Mafanikio makubwa huwa hayaji yote kwa wakati mmoja, bali yanakuja hatua kwa hatua.
Yanakuja mafanikio kidogo kwanza, ukishaweza kuyakabili vizuri na kutoa zaidi kinachohitajika ndiyo unapanda ngazi kwenda kwenye mafanikio makubwa zaidi.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana baadhi ya watu huwa wanakwama kwenye hatua ndogo za mafanikio wanayokuwa wameyapata.
Yaani mafanikio kidogo ambayo mtu anakuwa ameyapata yanakuwa kikwazo kwake kupata mafanikio makubwa zaidi.

Kabla hujalaumu kukosa unachotaka, anza kwa kulaumu kushindwa kutoa kafara unazopadwa kutoa ili kupata unachotaka.

Kila kitu unachotaka, asili inaweza kukupa.
Lakini asili haitakupa tu kwa sababu unataka, bali itakupa kama utaionyesha kweli umedhamiria kukipata, kupitia kafara unazotoa.

Na ieleweke wazi kwamba ninaposema kafara hapa simaanishi kuwaumiza wengine kwa namna yoyote ile.
Bali namaanisha kutoa kitu ambacho kinakuumiza sana wewe binafsi.
Lazima uwe tayari kuachilia vile ulivyokamatia sana ndiyo uweze kufungua uwanja wa mafanikio.

Mafanikio yako makubwa unayoyataka yanapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye maisha yako.
Kama kuna kitu kingine chochote ambacho unakipa nafasi kuliko mafanikio unayoyataka, kitu hicho ndiyo kitakuwa kikwazo kikubwa sana kwako kuyapata mafanikio hayo.

Vikwazo vingi kwenye safari yako ya mafanikio vinaanzia ndani yako mwenyewe, kwenye vitu ambavyo tayari unavipenda sana.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuachana navyo ili ufungue milango ya mafanikio makubwa kwako.

Kwa lolote unalokwama kwenye maisha yako, jiulize ni kitu gani bado hujawa tayari kukiacha.
Ukijua na kuacha, mafanikio yatakuwa uhakika sana kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe