3055; Usijipe kazi usizoziweza.

Rafiki yangu mpendwa,
Safari ya mafanikio ambayo tupo ni safari ngumu na ndefu.
Ugumu wa safari hii ni kazi kubwa tunayopaswa kuweka ili kupata matokeo makubwa tunayotaka kuyapata.

Wengi huwa wanashindwa kazi hiyo, siyo kwa sababu haiwezekani, bali kwa sababu wanachoka kwa kazi nyingine wanazokuwa wamejipa.

Yaani wanakuwa wamejipa kazi ambazo zinachukua nguvu na muda wao, lakini hazina matokeo mazuri kwao.

Kuna kazi kubwa tatu ambazo watu wamekuwa wanajipa na zinaishia kupoteza muda wao na kuwa kikwazo kwao kufanikiwa.

Ya kwanza ni kutaka kubadili watu.
Hapa mtu anachagua kujihusisha na watu ambao hawana tabia wanazozitaka, ila wanajiambia watawabadili watu hao.
Hakuna kitu kinachowapoteza watu kama hitaji la kuwabadili watu wengine.
Wanahangaika sana kwa kila namna, lakini hakuna mafanikio wanayoyapata.
Watu huwa hawapendi kubadilishwa.
Wanaweza kuamua kubadilika wao wenyewe kama watataka na kuwa tayari kujitoa, lakini siyo kubadilishwa na watu wengine.

Ili upeleke juhudi zako zote kwenye mafanikio, ni vyema uchague kwenda na watu ambao tayari wana tabia unazotaka na huhitaji kuwabadilisha.
Anza na watu ambao wanaweza kutekeleza kile unachotaka kitekelezwe bila ya kulazimishwa kufanya hivyo.
Na hapo unakuwa umeshashinda nusu ya kazi unayopaswa kuweka ili matokeo yapatikane.

Ya pili ni kutaka kumfurahisha kila mtu.
Hivi umewahi kugundua kwamba biashara zilizojikita kwenye kuwafurahisha watu ndizo zinazotoza gharama kubwa sana?
Ndiyo, angalia burudani nyingi bora na kubwa. Watu wanalazimika kuingia gharama kubwa kuzipata.
Hiyo ni kwa sababu ni kazi kubwa sana kuwafurahisha watu.
Halafu sasa, ni jambo lisilowezekana kumfurahisha kila mtu.
Kwa mfano hata burudani ambayo ni ghali sana na inawapa watu furaha kubwa, huwa siyo kwa kila mtu.
Kuna mtu hata akipewa burudani hiyo bure, hatakuwa tayari kuipokea.

Anza kwa kujifurahisha wewe mwenyewe, kwa kufanya kile kinachokupa burudani na hapo utawaalika wale ambao wanaburudika na hicho unachoburudika wewe.
Kwa kuwa unaburudika, utakuwa tayari kufanya kwa ukubwa zaidi na hapo utaendelea kuwafurahisha wale wanaoelewa kitu hicho.
Lakini wakati huo huo kuna watu utakuwa unawatibua na kuwaudhi sana kwa hicho unachofurahia wewe.
Na hilo siyo tatizo lako wewe, bali ni tatizo lao binafsi, hivyo hakuna unachoweza kufanya.
Huwezi kumfurahisha kila mtu hata ufanyeje.
Na mbaya zaidi, unapofanikiwa, utafanikiwa pia kuwachukiza baadhi ya watu.
Kuna watu ambao wataona hustahili kupata mafanikio uliyoyapata.
Na hapo huna namna ya kuwabadili, zaidi ya kuwaacha na kisirani chao wenyewe.

Ya tatu ni kuwahamasisha watu.
Hii ni ngumu kidogo kueleweka na kukubalika, ila twende nayo taratibu.
Watu wanahitaji hamasa ili kufanya mambo makubwa.
Hamasa zipo za aina mbili; ya nje na ya ndani.
Hamasa ya nje ni ile inayotoka kwa watu wengine, hii huwa haidumu kwa muda mrefu.
Hamasa ya ndani ni ile inayoanzia ndani ya mtu mwenyewe, hii huwa inadumu kwa muda mrefu.
Lengo la kuwahamasisha watu kwa nje ni kuibua hamasa ya ndani yao ambayo itawasukuma watu kwa muda mrefu.
Lakini kama utawapa watu hamasa ya nje, huku ndani yao wakiwa hawaha hamasa, ni sawa na kuwasha kuni mbichi, utapoteza nguvu nyingi na hazitawaka.

Epuka sana kuwahamasisha watu ambao ndani yao hawana hamasa kabisa.
Badala yake chagua kwenda na watu ambao tayari wana hamasa kubwa ndani yao na kinachohitajika ni wewe kuiibua na kuwapa msukumo wa kwenda zaidi.
Hiyo ni kwa wafanyakazi, washirika na hata wateja.
Ukitegemea hamasa unayowapa watu ndiyo iwasukume kupiga hatua, utagundua wanafanya pale unapowapa hamasa na ukiacha kuwapa hamasa nao wanaacha kufanya.
Hapo unakuwa umejipa kazi ngumu ya muda wote kuwapa watu hamasa, kitu ambacho kinakuwa kikwazo kwako kufanya mambo mengine muhimu.

Unapotaka kupata moto, unaweka kazi kwenye kuwasha nishati iliyopo, iwe ni kuni, mkaa, mafuta au gesi. Ukishaweka nguvu ya mwanzo ya kuwasha, moto unaendelea kujichochea wenyewe kwa nguvu iliyo ndani ya nishati husika.
Huhitaji kuwa unapepea moto huo wakati wote ndiyo uwake.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye hamasa. Hamasa yako ya nje inapogusa mtu mwenye hamasa ya ndani, anaendelea kuhamasika na kutokuhitaji hamasa yako kila mara.
Lakini unapohamasisha watu ambao hawana hamasa ya ndani, unahitajika kuendelea kutumia hamasa yako muda wote. Inakuwa ni sawa na kuwasha kuni mbichi, ukiacha kuchochea zinazima.

Safari ya mafanikio inaweza kutuchosha na bado mafanikio yenyewe tusiyapate kama nguvu zetu zinapotelea kwenye maeneo yasiyokuwa sahihi.
Peleka nguvu zako kwenye kazi zilizo sahihi kwako ili uweze kuzalisha matokeo yenye tija na yatakayokupa mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe