3058; Wote tupo chini ya misingi hii.

Rafiki yangu mpendwa,
Tawala nyingi za kidikteta huwa zinaanza vizuri sana.
Kiongozi ambaye ni dikteta, anaanza akiwa na nia njema kabisa ya kufanya maisha ya watu kuwa bora.
Anapata imani kubwa ya watu mwanzoni na mambo yanaenda vizuri sana.
Mabadiliko mazuri yanaonekana mwanzoni na watu kunufaika.

Lakini sasa, kadiri muda unavyokwenda, mambo huwa yanabadilika na tawala hizo za kidikteta kuanza kufanya vibaya.
Watu wanawachoka na kukosa imani na viongozi hao madikteta.

Hali hiyo imekuwa inasababishwa na uongozi wa kidikteta kutokuwa chini ya sheria au misingi yoyote.
Kiongozi ambaye ni dikteta anaamua kufanya chochote anachotaka bila ya kufuata maelekezo, sheria au misingi yoyote ile.

Mwanzoni hali hiyo inakuwa nzuri, kwani maamuzi mengi wanayofanya yanakuwa na manufaa.
Lakini baadaye mambo yanabadilika, kwa sababu ya madhaifu ya kibinadamu na kutokuwepo kwa sheria au misingi ambayo kiongozi anaifuata, maamuzi mengi anayoyafanya yanakuwa na makosa.
Makosa hayo yanakuwa na madhara makubwa kwa watu, hivyo aliyeonekana shujaa mwanzoni anageuka kuwa mtesi.

Hivyo ndivyo inavyokwenda kwenye kila ngazi ya uongozi, mpaka kwenye ngazi ya familia.
Pale inapokosekana misingi ambayo inasimamiwa na kila mtu, kiongozi anajikuta akifanya makosa ambayo yanawaumiza wengi.
Anaweza kuwa na nia njema kabisa, lakini kwa madhaifu ya kibinadamu, anaishia kuleta madhara na siyo manufaa.

Kuondokana na hili, kwenye programu yetu ya KISIMA CHA MAARIFA na BILIONEA MAFUNZONI wote tupo chini ya misingi inayotuongoza.
Hakuna mtu yeyote aliye juu ya misingi mikuu tuliyokubaliana ituongoze kwenye safari yetu ya kufikia mafanikio makubwa.

Misingi hiyo ni kama ifuatavyo;

Msingi mkuu ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA.
Kila mmoja wetu anakuwa na NIDHAMU ya hali ya juu sana ya kupanga na kufanya kama alivyopanga.
Kila mmoja anafanya kilicho sahihi mara zote, bila ya kujali anaonekana au haonekani na huo ndiyo UADILIFU.
KUJITUMA ni kwenda hatua ya ziada kwenye kile ambacho mtu anafanya na hivyo ndivyo wote tunavyoenda.

Mwongozi wa kufanya maamuzi ni AFYA, UTAJIRI na HEKIMA.
Maamuzi yote tunayofanya tunahakikisha yanazingatia maeneo hayo matatu;
Yanafanya AFYA zetu kuwa imara zaidi.
Yanatujengea UTAJIRI zaidi.
Na yanatuongezea HEKIMA.
Kama maamuzi hayana manufaa kwenye eneo lolote kati ya hayo matatu tunaachana nayo, hayana manufaa kwetu.

Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO na HUDUMA.
KAZI ndiye rafiki yetu wa kweli na tunaipenda sana. Kazi ndiyo kipaumbele chetu cha kwanza.
UPENDO ndiyo imani yetu kuu inayotuunganisha pamoja. Tunajipenda sisi wenyewe, tunawapenda wale wanaotuzunguka na tunapenda kile tunachofanya. Kwa upendo huo tunajenga mahusiano bora sana baina yetu.

Kwenye kujifunza endelevu tunakuwa na UPEKEE, UDADISI na UBUNIFU.
Tunakuwa na UPEKEE kwenye kila kitu tunachofanya kwa kuepuka mazoea na kufuata mkumbo.
Tunakuwa na UDADISI wa kuhoji na kuchunguza kila kitu ili kuelewa kwa kina.
Tunakuwa na UBUNIFU wa kujaribu vitu vipya na vya tofauti kabisa.

Kwenye kujenga jamii na jumuia ya tofauti kabisa, tunaongozwa na USHIRIKIANO, UTEGEMEANO na UWAJIBIKAJI.
Tunakuwa na USHIRIKIANO wa karibu na wote ambao tupo kwenye safari moja ya mafanikio. Tunakuwa wawazi baina yetu na kuweza kushirikiana vizuri.
TUNATEGEMEANA kwenye yale ambayo tunafanya kwa kusaidiana kupiga hatua kubwa zaidi kwenye safari ya mafanikio.
Tunakuwa na UWAJIBIKAJI wa hali ya juu kwa wale ambao tupo nao pamoja, kwa wao kutushikilia kwenye safari hii na kutuhoji pale tunapokwenda tofauti na mipango na mchakato mkuu wa safari.

Sisi wote tupo chini ya misingi hiyo, tukiifuata, kuiamini na kuitumia kwenye maamuzi yoyote tunayokuwa tunayafanya.
Ni kuifuata misingi hiyo ndiyo kunakotuhakikishia wote mafanikio makubwa kwenye safari tuliyopo.

Misingi hii ndiyo inawajengea watu wengine imani ya kutufuata na kushirikiana vizuri na sisi, kwa kujua maamuzi yote tunayokwenda kufanya ni maamuzi bora kwa sababu yanazingatia misingi sahihi tuliyojiwekea.

Kwenye biashara unayojenga na timu unayokuwa nayo, kuwa na misingi ambayo inafuatwa na watu wote ikiwepo wewe mwenyewe.
Hakikisha misingi hiyo inajulikana na kila mtu, siyo tu kwa maneno, bali kwa vitendo kwa wewe kiongozi wa biashara kuwa mfano kwenye kusimamia na kuiishi misingi hiyo.

Watu wanakuamini, kukufuata na kujitoa sana pale wanapoona kuna misingi ambayo inawaongoza wote.
Pale ambapo maamuzi yote yanafanyika kwa misingi iliyopo, watu wanayapokea hata kama sivyo walivyotaka wao wenyewe.

Lakini misingi inapokosekana, maamuzi yanafanyika kwa hisia na mazoea, kitu ambacho kinakuwa na madhara kwa wote wanaohusika.
Hilo linapoteza imani ya watu kwa mfanya maamuzi na hivyo kutokufuata maamuzi yake.

Kama unataka kuwa kiongozi bora, lazima kwanza uwe mfuasi bora.
Unakuwa mfuasi bora pale unapokuwa na misingi unayoisimamia kwenye mambo yote unayofanya.
Watu watakuamini na kukufuata pale wanapojua kuna misingi inakuongoza.
Lakini ukikosa misingi, unafanya maamuzi kwa hisia na mazoea, kitu ambacho kinakuwa na madhara kwa wote wanaohusika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe