3060; Kuna vitu unafanya kwa usahihi.

Rafiki yangu mpendwa,
Takwimu nyingi za kibiashara zimekuwa zinasikitisha sana.
Biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya mwaka mmoja au miwili.

Vifo vya biashara hizo nyingi huwa vinatokana na changamoto mbalimbali ambazo waanzilishi hawakujua na kujiandaa nazo.
Lakini pia makosa, uvivu na uzembe vimekuwa vinachangia sana vifo vya biashara nyingi.

Kama umekuwa kwenye biashara moja kwa zaidi ya miaka miwili na haijafa, unatakiwa ujipongeze sana kwa sababu kuna vitu unavifanya kwa usahihi.

Unahitaji pongezi kubwa sana kama umeweza kuendesha biashara kwa zaidi ya miaka miwili bila ya kufa.
Haijalishi biashara ina ukubwa kiasi gani, kitendo tu cha kuweza kuwepo kwa zaidi ya miaka miwili bila kufa, ni cha kishujaa.

Kinachoua biashara nyingi ni mambo ya ndani na siyo ya nje ya biashara.
Wengi ambao biashara zao zinakufa hulalamikia sana hali ya uchumi, ushindani na changamoto nyingine kama sababu na biashara kufa.

Lakini ukweli ni sababu hizo za nje huwa zinamalizia tu kile kilichoanzia ndani.
Vifo vya biashara huwa vinaanzia ndani ya biashara yenyewe.
Uvivu, uzembe na tamaa vimesababisha vifo vya biashara nyingi.
Uvivu na uzembe ni kwenye ufanyaji wa mambo, huku tamaa ikiwa ndiyo inakuhamisha kibiashara na kukaribisha anguko.

Kwa mazingira yetu, kila wakati huwa kuna fursa mpya zinazokuja kila wakati.
Fursa hizo zinaonekana ni za muda mfupi na zinaisha kwa haraka, hivyo wengi wanaingia tamaa na kuzichangamkia.
Kinachotokea ni nguvu kupungua kwenye biashara kuu kutokana na umakini wa mtu kwenda kwenye kitu kingine.
Hilo linapelekea anguko kubwa la biashara.

Kwa wewe kuweza kukaa kwenye biashara kwa miaka zaidi ya miwili ni kitu kikubwa unachopaswa kukithamini.
Kuna mambo mazuri na sahihi sana unayoyafanya na ndiyo yanayosababisha biashara kuweza kuendelea kuwepo, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali.

Lakini basi, kuwa na vitu ambavyo umekuwa unavifanya kwa uzuri na usahihi haimaanishi umeshamaliza kila kitu.
Bali inamaanisha una kazi kubwa mbele yako ya kuvuka uzuri uliopo ili kufikia ubora zaidi.

Wanasema adui wa ubora ni uzuri.
Chochote mtu anachofanya vizuri huwa ni vigumu sana kujisukuma na kufanya kwa ubora.
Kwa sababu matokeo mazuri anayopata mtu huwa yanamlevya na kuona hana haja ya kubadili.

Matokeo mazuri ambayo umekuwa unayapata ndiyo yamekuwa kikwazo kwako kupata matokeo bora zaidi.
Ni kama umejiwekea ukomo kwenye matokeo unayokuwa unayapata.

Njia pekee ya kujinasua kwenye hilo ni mtu kuwa tayari kuboresha yote mazuri yanayofanyika.
Kwa kuangalia namna ya kufanya kwa ubora zaidi yale unayofanya kwa uzuri, utaziona fursa za ukuaji zaidi.

Zoezi muhimu la kufanya;
1. Orodhesha vitu vyote ambavyo umekuwa unafanya kwa uzuri na ubora kwenye biashara yako.
2. Kwa kila ulichoorodhesha, andika ni jinsi gani kimekuwa kikwazo kwako kukua zaidi ya hapo.
3. Weka mkakati wako wa ukuaji kibiashara kwenye maeneo yote ambayo tayari upo vizuri ili uweze kuwa bora kabisa.

Kilichokufikisha hapo ulipo sasa siyo kitakachokupeleka kule unakotaka kufika kesho.
Hili ni muhimu kulielewa na kuzingatia mara zote ili kuweza kujenga biashara inayoweza kukua na kufikia malengo makubwa.
Lakini hayo yote yanaanzia kwako wewe mwenyewe kwa kutambua na kujikubali kwa yale unayofanya vizuri, kisha kupata msukumo wa kuyafanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe