3065; Maumivu hayajatosha.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu ni viumbe wa tabia, huwa tunaanza kujenga tabia, kisha tabia zinatujenga.
Asilimia kubwa ya yale tunayofanya kila siku, tunayafanya kwa tabia na mazoea na siyo kwa fikra.

Hilo ndiyo huleta upinzani mkali sana kwenye mabadiliko.
Watu huwa hawapo tayari kuachana na tabia na maumivu yao.
Njia pekee ya hilo kuwezekana ni kuyafanya maisha ya sasa kuwa magumu na yenye maumivu makali kiasi kwamba huwezi kuendelea kuvumilia.

Ni pale maumivu yanapokuwa hayawezi kuvumilika ndiyo mabadiliko huwa yanafanyika.
Kama maumivu yanavumilika, wengi huona bora waendelee na maumivu hayo kidogo kuliko kwenda kuanza kitu kipya kabisa.

Unafikiri ni kitu gani kinawafanya watu wabaki kwenye ajira ambazo hawazipendi na haziwalipi vizuri?
Pia unafikiri ni kitu gani kinawafanya watu waendelee kubaki kwenye biashara wasizozipenda na zisizowalipa vizuri?
Kote jibu ni moja, watu wanayaogopa maumivu ya badaliko kuliko maumivu ya kubaki kwenye mazoea waliyopo.

Kuna vitu viwili vya uhakika kuhusu mabadiliko ambavyo ndiyo hukwamisha wengi kubadilika.
Kitu cha kwanza ni kila mabadiliko huwa yanakuja na gharama zake.
Kitu cha pili ni kukosekana kwa uhakika wa matokeo mazuri.

Ili uweze kuvuka vitu hivyo viwili kwa uhakika, lazima uyakuze maumivu ya popote ulipo sasa.
Yafanye maumivu ya kubaki pale ulipo sasa kuwa makubwa sana kuliko maumivu ya mabadiliko.

Ukiona bado unakwama kwenye kubadilika, jua maumivu bado hayajakutosha, unaweza kuyavumilia.
Ukijikuta kwenye hali hiyo ya kukosa msimamo wa mabadiliko, ni muhimu uendelee kujisukuma mwenyewe kwa kujipa maumivu makali sana unapobaki pale ulipo.
Jipe maumivu ambayo huwezi kuyavumilia hata kwa muda mfupi ili wakati wote uwe mtu wa kuyakabili mabadiliko na kuyatumia kwa manufaa.

Nimalizie kwa hadithi fupi, ambayo nimewahi kuishirikisha ila nitairudia tena hapa ili tupate funzo.

Jirani mmoja alisikia mbwa wa jirani yake akibweka kwa uchungu mkali na kwa muda mrefu.
Jirani huyo alishindwa kuvumilia ubwekaji huo wa mbwa na kuamua kwenda kwa jirani yake kuona nini kinaendelea.
Alipofika alishangazwa kumwona jirani yake akiwa amekaa anasoma gazeti bila wasiwasi wowote, huku pembeni yake mbwa akiwa amekaa kwenye moto na kuendelea kubweka.
Mtu huyo alimuuliza jirani yake iweje amekaa kwa utulivu wakati mbwa anapata maumivu ya kuungua moto.
Jirani huyo alimjibu kwa upole; huyo mbwa hajafungwa kukaa hapo, yuko huru kutoka hapo alipo, lakini kwa sababu anaweza kuyavumilia maumivu hayo, amechagua kuendelea kuyavumilia badala ya kuamua kuondoka.

Rafiki, ni maumivu gani unayoyang’ang’ania kwenye maisha yako ili tu ubaki kwenye mazoea badala ya kwenda kwenye mabadiliko?
Ni wakati sasa wa kukuza maumivu ya chochote ambacho unataka kukibadili ili usijidanganye na kuyakwepa mabadiliko.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe