3068; Kuweka na kutoa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna hadithi nyingi tulizokuwa tunafundishwa tulipokuwa watoto, ambazo zilikuwa na mafunzo makubwa sana kuhusu maisha.
Nyingi zilikuwa na mafunzo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wetu kuelewa kwenye hicho kipindi.

Kwa mfano kuna hadithi ya kijana ambaye alipewa kazi ya kwenda kulisha mifugo nje kidogo ya kijiji.
Kijana huyo alikuwa mvivu na hakuipenda kazi ile.
Akiwa analisha mifugo hiyo, akajiuliza atawasumbuaje watu wengine?
Akapata wazo kwamba apige kelele kuna simba anakamata wanyama.
Kweli akafanya hivyo, akapaza sauti sana kwamba kuna simba.
Wanakijiji waliposikia sauti yake, walikuja mbio sana wakiwa na silaha za kumshambulia simba huyo.
Walipofika hakukuwa na simba, walipomuuliza kijana huyo akabaki anacheka tu.
Wakamuonya na kuondoka zao.

Siku nyingine tena kijana akarudia kitu hicho, hakukuwa na simba, ila akapiga kelele za simba.
Wanakijiji wakaja na silaha kwa ajili ya kumkabili simba huyo. Lakini hakukuwa na simba. Waliondoka wakiwa na hasira kali. Kijana alibaki anacheka tu, akiona amewakomoa sana.

Sasa basi, siku ya siku kijana akakutana na simba kweli. Simba alianza kujitokeza kwa mbali. Kijana akaanza kupiga kelele za simba, alipaza sauti sana.
Wanakijiji waliposikia sauti hiyo wakaambiana ni kawaida yake huyo kijana, hakuna simba yeyote.
Kijana alipiga sana kelele bila ya kupata msaada wowote.
Na alipoona hapati msaada, alianza kukimbia, hapo ndipo simba naye akamkimbiza, alimkamata na kumgeuza kitoweo.
Maisha ya kijana huyo yakaishia hapo.

Hadithi hiyo inaweza kuwa na mafunzo mengi sana kwa namna unavyoweza kufikiri.
Lakini funzo moja kubwa sana kuhusu mafanikio ambalo nataka tulijadili leo ni imani.

Kwenye safari ya mafanikio, imani ni kiungo muhimu sana.
Tunaweza kusema imani ni kama fedha kwenye mafanikio.
Kadiri watu wengi wanavyokuamini, ndivyo unavyofanikiwa.
Imani huwa inajengwa kwa matendo na siyo maneno.
Unaweza kusema sana, lakini watu watakuamini kupitia yale unayofanya.
Kila unachofanya kwenye maisha yako, kinagusa imani yako kwa wengine kama fedha kwenye akaunti ya benki.

Ukifanya mambo ya kuaminika unakuwa umeweka fedha kwenye hiyo akaunti yako. Hivyo unazidi kuaminiwa na watu zaidi.
Ukifanya mambo ambayo siyo ya kuaminika unakuwa umetoa fedha kwenye hiyo akaunti yako. Hilo linafanya imani ya watu kwako ipungue.

Sasa basi, watu wanakuamini kiasi gani inategemea sana na salio lako kwenye benki yako ya imani.
Kama umeweka sana (yaani umefanya matendo mengi ya kuaminika) salio lako linakuwa limejaa na unaaminika sana na wengine.
Na kama umetoa sana (yaani umefanya matendo mengi ya kutokuaminika) salio lako linakuwa pungufu na huaminiki na wengine.
Kuna ambao wameshato kupitiliza (overdraft) na hawa ndiyo ambao wamefika hatua ambayo hawaaminiki tena.

Ili upate mafanikio makubwa sana, unahitaji kuaminiwa na watu wengi sana.
Siyo tu imani ya juu juu, bali imani ya kina na isiyo na mashaka yoyote.
Imani ya aina hiyo itaanzia kwenye benki yako ya matendo ya imani.
Ili uaminiwe bila ya shaka, unapaswa kufanya kitu kimoja tu kwenye akaunti yako ya imani, kuweka.
Kamwe usitoe kwenye akaunti hiyo.
Wewe endelea kuweka tu, kwa kufanya matendo yanayojenga imani mara zote.
Kamwe usifanye tendo lolote ambalo linakuondolea imani kwa watu.
Kwani kuna baadhi ya matendo ukiyafanya ni kama umechukua mkopo mkubwa na kuutumia vibaya.
Watu wanakuwa hawakuamini tena baada ya hapo.

Usifanye tu matendo ya uaminifu pale unapokuwa mbele ya wengine, bali yafanye hata unapokuwa peke yako.
Kwa sababu kwa zama tunazoishi sasa, hakuna tena siri.
Hata mambo unayoyafanya kwa kificho, kuna namna huwa yanakuja kujidhihirisha wazi.

Leo fanya zoezi la kuikagua akaunti yako ya imani, imejaa au iko tupu kiasi gani?
Kwa salio lolote ulilonalo sasa kwenye hiyo akaunti yako, fanya kazi moja kubwa ya kuweka tu bila kutoa.
Fanya matendo yanayofanya uaminike na achana na matendo yanayofanya usiaminike.

Ipo ndani ya uwezo wako kuwafanya watu wakuamini au wasikuamini.
Ugumu au urahisi wa kufanya hivyo unategemea salio lililopo kwenye akaunti yako ya imani sasa.
Kama salio lipo chini sana, au una mkopo, kwa maana umefanya matendo mengi yanayofanya usiaminike, unakuwa na kazi kubwa na ya muda mrefu ya kujenga upya imani ya watu kwako.
Unachohitaji ni kufanya kazi ya kujenga imani hiyo kupitia matendo unayokuwa unayafanya.

Kila wakati tunza vizuri akaunti yako ya imani, kwani hiyo ndiyo inayoathiri akaunti yako ya fedha pia.
Kama akaunti ya imani iko chini, hata akaunti ya fedha itakuwa chini.
Kuanza kujaza akaunti ya fedha, anza kujaza akaunti ya imani.
Pamoja na ugumu wake, ni kitu kinachowezekana kama utakivalia njuga.
Weka kazi ya kutosha kwenye kujenga akaunti yako ya imani na utaweza kujenga akaunti yako ya fedha.

Jiwekee mwiko wa kutokutos kwenye akaunti yako ya imani, kitu ambacho utakusaidia sana.
Kamwe usifanye jambo lolote ambalo linavunja uaminifu wa watu kwako.
Kuwa tayari kupitia mateso makali kuliko kuvunja imani ambayo watu wameshaijenga mwako.
Kuwa na imani kali ambayo itawafanya wengine wakuamini bila ya shaka.
Hilo litakuwa na mchango mkubwa sana kwenye mafanikio yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe