Barua ya IV; Kuhusu hofu ya kifo.

Rafiki yangu Mstoa,
Moja ya hofu ambazo zimekuwa zinatusumbua sana sisi binadamu, ni hofu ya kifo.
Sote tunajua kuna siku tutakufa, siku ambayo hatuijui. Lakini kila tunapofikiria kuhusu kifo, huwa tunaingiwa na hofu kubwa.

Hofu ya kifo imekuwa moja ya vitu vinavyowazuia watu wasiyaishi maisha yao kwa uhuru na kuyafurahia.
Wengi hujikuta wakizuiwa na hofu hizo wasifanye makubwa waliyotaka kufanya kwenye maisha yao.

Hii siyo hali mpya, bali imekuwepo tangu kuwepo kwa wanadamu hapa duniani.
Na kwa kuwa hakuna mwenye uhakika nini kinaendelea baada ya kifo, hofu yake imekuwa kubwa zaidi.

Zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita, Mstoa Seneca aliandika barua kwa rafiki yake Lucilius akimweleza jinsi ya kukabiliana na hofu ya kifo iliyokuwa inamsumbua.

Hapa tunapata nafasi ya kujifunza mambo muhimu ya kuzingatia ili tuweze kuiondoa hofu ya kifo na kuyaishi maisha yetu kwa uhuru mkubwa.

1. Kuyafurahia maisha, tafakari kwa utulivu.

Seneca anaianza barua kwa kumwambia rafiki yake anaweza kuharakisha kwenye mambo yake ili apate muda mrefu wa kufurahia muda tulivu na akili yake.
Anamhakikishia kwamba atapata furaha kwa kuwa na akili tulivu.
Lakini atapata furaha ya tofauti kama atatafakari kwa utulivu.
Yaani badala ya kuiweka tu akili kwenye utulivu, mtu unapaswa kuitumia kutafakari.

Hatua ya kuchukua;
Tenga muda ambao utaiweka akili yako kwenye utulivu na kuyatafakari maisha yako.
Hili ni muhimu sana kwenye hizi zama zenye usumbufu wa kila aina, watu hatupati muda wa kutosha kuyatafakari maisha yetu, na hivyo kukosa nafasi ya kuyafurahia.

Nukuu;
‘Doubtless you will derive enjoyment during the time when you are improving your mind and setting it at peace with itself; but quite different is the pleasure which comes from contemplation when one’s mind is so cleansed from every stain that it shines.’ – Seneca
‘Bila shaka utafurahia kuwa na muda wa kuiweka akili yako kwenye utulivu; lakini utafurahia zaidi kama utaiweka akili yako kutafakari kwa utulivu.’ – Seneca

2. Kila hatua ya maisha ina kitu cha kuhofia.

Mara nyingi watu hudhani wakishavuka hatua fulani ya maisha basi hawatakuwa tena na cha kuhofia.
Tukiwa watoto kuna vitu tunahofia, tukiwa vijana tunahofia vitu vingine, kadhalika mpaka uzee.
Tunapotoka ngazi moja ya maisha kwenda ngazi nyingine huwa tunakuwa na furaha, tukidhani mambo ya nyuma tumeyaacha.
Lakini tunakuja kugundua mambo hayo hatujayaacha, kwa sababu yapo ndani yetu.
Seneca anaeleza mambo mengi yanayoendelea kutusumbua tunakuwa tumetoka nayo kwenye hatua za awali za maisha.

Hatua ya kuchukua;
Usiweke matumaini yako ya hofu kuisha pale unapotoka hatua moja ya maisha kwenda nyingine.
Jua unachohofia kipo ndani yako, hakuna namna unaweza kukitoroka, badala yake unapaswa kukielewa na kukikubali.

Nukuu;
‘Boys fear trifles, children fear shadows, we fear both.’ – Seneca
‘Vijana wanahofia mambo madogo madogo, watoto wanahofia vivuli, tunahofia vyote.’ – Seneca

3. Itumie hofu kupiga hatua zaidi.

Seneca anatuambia wajibu wetu ni kuendelea kupiga hatua zaidi kwenye maisha. Hatupaswi kuruhusu hofu ya kifo kuwa kikwazo kwetu kupiga hatua zaidi kwenye maisha.
Iwe tutahofia au hatutahofia, bado tutakufa.
Hivyo haina maana kuhofia kitu ambacho huwezi kukibadili.
Badala yake tutumie hiyo hali ya hofu kupiga hatua zaidi kwenye maisha yetu.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapohofia kifo, tumia hofu hiyo kujisukuma kufanya mambo makubwa zaidi.
Kwa kuwa unajua utakufa, jisukume kufanya makubwa kwa kipindi hiki ambacho bado upo hai.

Nukuu;
‘All you need to do is to advance; you will thus understand that some things are less to be dreaded, precisely because they inspire us with great fear.’ – Seneca
‘Unachohitaji ni kuendelea kupiga hatua; utaelewa kwamba baadhi ya vitu havipaswi kuhofiwa, kwa sababu vinatuhamasisha kwa hofu yake.’ – Seneca

4. Huishi na hufi.

Seneca anaeleza mtego ambao watu wengi wamenasa kwenye maisha.
Wanakuwa wanatamani sana kuishi, lakini pia wanahofia sana kufa.
Kwa kutamani kuishi wanakuwa hawapo tayari kufa na kwa kuhofia kufa wanashindwa kuyafurahia maisha, hivyo inakuwa ni sawa na hawaishi.
Anasema njia ya kutoka kwenye mtego huo ni kuishi maisha yako huku ukijua wakati wowote unaweza kuyaacha.

Hatua ya kuchukua;
Chagua kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu huku ukiwa tayari kuyaacha wakati wowote.

Nukuu;
‘Most men ebb and flow in wretchedness between the fear of death and the hardships of life; they are unwilling to live, and yet they do not know how to die.’ – Seneca
‘Watu wengi wamenasa kwenye mawimbi ya uovu kati ya hofu ya kifo na ugumu wa maisha; hawapo tayari kuishi,  lakini pia hawajui jinsi ya kufa.’ – Seneca

5. Unafurahia kitu unachoweza kukipoteza.

Sisi binadamu huwa tuna tabia ya kuzoea vitu ambavyo tunakuwa navyo kwa muda mrefu.
Tukishazoea vitu, huwa hatuvifurahii tena.
Hivyo ndivyo Seneca anavyotushauri tuyafurahie maisha, kwa kujua kwamba hatutakuwa nayo kwa muda mrefu.
Kwa kuwa hatutaishi milele, tunapaswa kufurahia huu muda tulionao hapa duniani kwa sasa.

Hatua ya kuchukua;
Kila unapohofia kifo, jikumbushe hiyo ndiyo sababu ya wewe kuyafurahia maisha sasa, kwa sababu hutakuwa nayo milele.

Nukuu;
‘No good thing renders its possessor happy, unless his mind is reconciled to the possibility of loss;’ – Seneca
‘Hakuna kitu kizuri kinachoweza kumpa mtu raha kama hakuna uwezekano wa kukipoteza.’ – Seneca

6. Ulishaanza kufa kitambo.

Tunasumbuka sana na kifo kwa sababu tunakichukulia kama tukio la mara moja.
Lakini kwa uhalisia, kifo siyo tukio, bali ni mchakato.
Tangu umezaliwa, umekuwa unakua, lakini pia umekuwa unakufa kidogo kidogo.
Kadiri muda unavyokwenda, ndivyo unavyoendelea kuyaacha maisha yako nyumba, ambayo huwezi kurudi kuyaishi tena.
Kwa kujua kwamba unakufa kila siku, iwe unahifia au huhofii, inakupa sababu ya kuacha kuhofia na kuanza kuyafurahia maisha uliyobakiwa nayo hapa duniani.

Hatua ya kuchukua;
Ishi kila siku kama ndiyo siku yako ya mwisho, kwa sababu huo ndiyo ukweli, siku ikishapita huwezi kurudi kuiishi tena, inakuwa ndiyo imepita moja kwa moja.
Siku ambazo umeshaziishi ni siku ambazo umeshakufa.
Hivyo hupaswi kuhofia kifo, kwa sababu tayari kinaendelea kwenye maisha yako.

Nukuu;
‘Take my word for it: since the day you were born you are being led thither. We must ponder this thought, and thoughts of the like nature, if we desire to be calm as we await that last hour, the fear of which makes all previous hours uneasy.’ – Seneca
‘Chukua neno langu; tangu siku uliyozaliwa umekuwa ukiendelea kupungua. Tunapaswa kutafakari hilo na kupata utulivu wakati tunaisubiri saa ya nwisho, ambayo kwa kuihofia, kunapoteza maana ya masaa yaliyopita.’ – Seneca

Kwa kuwa kifo ni kitu cha uhakika kwenye maisha yetu, hatupaswi kukihofia. Badala yake tunapaswa kukikubali ili tuweze kuyaishi maisha yetu kwa furaha.
Tuyaishi maisha yetu kwa ukamilifu wake, yatakuwa na maana na tutayafurahia.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.