3069; Kesho itakuwa ngumu zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu huwa tupo vizuri sana kwenye kujidanganya.
Huwa tunapanga mambo yetu wenyewe, tukiwa na shauku kubwa.
Lakini wakati wa kufanya mambo hayo unapofika, tunaahirisha.
Tunajiambia tutafanya kesho.

Kama kuna kaburi ambalo lina ndoto nyingi zilizoshindwa kutimia basi ni hiyo kesho.
Hebu anza tu kwa kujiuliza wewe mwenyewe, ni mambo mangapi uliyojiambia utafanya kesho uliyafanya kweli?
Kama utaacha kujidanganya hapa, utagundua ni mambo mengi sana.

Kitu kimoja ambacho binadamu huwa tunapenda kukifanya, japo hatupo vizuri kabisa kwenye kitu hicho ni kutabiri.
Huwa tunapenda kutabiri mambo yatakayokuja nyakati zijazo.
Lakini hatujawahi kuwa vizuri kwenye zoezi hilo.

Ndiyo maana huwa tunakuwa na nia njema sana ya kupeleka kesho mambo tuliyopanga kufanya leo.
Lakini ambacho tunakosea ni kudhani kesho itakuwa rahisi kuliko leo.
Tunasahau kwamba hatujui nini kitakachokuja kesho.
Na matokeo yake, kesho inakuwa vigumu zaidi kufanya.

Kama kuna kitu chochote ambacho umepanga kukifanya.
Halafu wakati wa kukifanya unapofika unajiambia utafanya kesho.
Jua kwamba nafasi ya kukifanya kitu hicho kesho ni ndogo zaidi ya leo.

Kitu chochote ambacho umeshindwa kukifanya leo, kesho kitakuwa kigumu zaidi kukifanya.
Kazi ambayo hujaifanya leo, kesho inakuwa ngumu zaidi kuifanya.
Deni ambalo hujalipa leo, kesho linakuwa na gharama kubwa zaidi na kuwa gumu kulilipa.
Kitabu ambacho hujasoma leo, kesho kinakuwa kigumu zaidi kusoma.

Unapeleka mambo kesho kwa nia njema, ukidhani kesho itakuwa rahisi.
Lakini kiuhalisia, kama umeshindwa leo, kesho itakuwa vigumu zaidi.

Mwanasayansi Isaac Newton aligundua kanuni ya kwanza ya mwendo ambayo inasema; kitu huwa kinabaki kwenye hali ambayo kipo, mpaka nguvu ya nje itumike kubadili hali ya kitu.
Hii ni kanuni inayohusika kwenye kila eneo la maisha na inaweza kuelezea kwa nini kesho inakuwa ngumu zaidi.

Kama kuna kitu umepanga kufanya, halafu wakati wa kufanya unafika na unapeleka kesho, maana yake kanuni hiyo ya kwanza ya mwendo inafanya kazi.
Kitu kimebaki kwenye hali yake ile ile.
Hiyo ina maana hata kesho kitu kitaendelea kubaki kwenye hiyo hali yake.
Lakini kama utajilazimisha kuanza hata kufanya, unakuwa umekiweka kitu kwenye mwendo na hivyo kesho inakuwa rahisi kuendelea kufanya.

Unapoacha kufanya kabisa unakiweka kitu kwenye hali ya kutokufanyika, jambo linalofanya kizidi kuwa kigumu kufanyika.
Na unapoanza kufanya kitu, unakiweka kwenye hali ya kufanyika, jambo linalokuwa rahisi kuendelea kufanya.

Kama kuna kitu ambacho unataka kukifanya kweli, utafanya kila namna uweze kukifanya.
Na kama itashindikana kukifanya kitu kwa siku uliyopanga, itakuwa vigumu zaidi kukifanya kwenye kesho unayojiambia.

Pambana sana uweze kufanya kitu kwenye muda ambao umepanga kukifanya.
Jisukume vyovyote uwezavyo ili uweze kuanza kufanya.
Maana kama utashindwa kuanza kufanya kama ulivyopanga, itakuwa vigumu zaidi wakati mwingine.

Anza kufanya leo au jiambie tu ukweli kwamba hutafanya kabisa.
Maana ukweli huwa unauma, ndiyo maana tunajificha sana nyuma ya kesho.

Anza kufanya leo, ili kesho uwe kwenye mwendo wa kuendelea kufanya.
Usipoanza kabisa kufanya, kesho itakuwa vigumu zaidi kuendelea kufanya.
Na kama huwa unafanya kila siku, ukiruka siku moja, kesho yake inakuwa ngumu zaidi kuendelea kufanya.

Hivyo basi, ili kuifanya kesho iwe rahisi kufanya kile ulichopanga kufanya, hakikisha unakifanya leo.
Kila unapofanya kitu, unakifanya rahisi zaidi kuendelea kukifanya.
Lakini unapoacha kufanya kitu, unakifanya kuwa kigumu zaidi kuanza kukifanya.

Usiifanye safari yako ya mafanikio kuwa gumu kwa kujidanganya na kesho.
Fanya kila kitu kama ulivyopanga kufanya.
Kuna sababu kwa nini ulipanga hivyo, tekeleza.

Kama tu ungekuwa unatekeleza mambo yote unayojipangia kuyafanya wewe mwenyewe bila shuruti ya watu wengine, ungekuwa mbali zaidi ya hapo ulipo sasa.
Ila bado hujachelewa, unaweza kuanza sasa nidhamu ya kufanya kila kitu kwa jinsi ambavyo umepanga wewe mwenyewe kufanya.
Na ukaweza kuvuna matokeo makubwa na mazuri sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe