Rafiki yangu mpendwa,

Leo ninayo furaha kubwa sana ya kukumbuka siku yangu ya kuzaliwa.
Leo tarehe 28/05/2023 nimetimiza umri wa miaka 35 hapa duniani.
Nilizaliwa tarehe kama hiyo mwaka 1988.

Napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana wewe kuwa msomaji wa kazi mbalimbali ambazo nimekuwa ninaandika kwa miaka 10 ambayo nimekuwa kwenye uandishi, tangu 2013.

Wewe ndiyo umekuwa sababu ya mimi kulijua na kuliishi kusudi kuu la maisha yangu.
Bila ya wewe kuniamini, kusoma kazi zangu, kufanyia kazi unayojifunza na kupata matokeo bora, kazi hizi zingekosa maana na kusudi langu lisingetimia.

Nikukumbushe kusudi kuu la maisha yangu ni; KUWAWEZESHA WATU KUWA NA MAISHA BORA KUPITIA KAZI NINAZOFANYA.
Hapa ndipo mimi na wewe tunapoungana, mimi nikiwa nawajibika kwako.

Nikukumbushe malengo makuu mawili ambayo nayapambania kila siku ya maisha yangu na nina uhakika wa kuyafikia;
1. Kuwa bilionea (kwa thamani ya dola za Marekani).
2. Kuwa raisi wa Tanzania mwaka 2040.
Hayo ndiyo malengo makubwa kabisa yanayonikosesha usingizi kila siku.
Nayapambania bila kuchoka wala kukata tamaa.

Kwa nini nasema NIMEJIPATA.

Rafiki yangu mpendwa,
Ni miaka 11 sasa tangu nimeanza kuishi maisha ya kujitegemea mimi mwenyewe.
Hapo namaanisha kujitegemea kwa asilimia 100, bila ya kutegemea msaada wa mtu mwingine yeyote kwenye kuendesha maisha.

Kwenye miaka hiyo 11, nimefanya vitu vingi sana vya kuingiza kipato.
Baadhi ya vitu hivyo ni;
1. Kufundisha shule za sekondari na vyuo vya kati.
2. Kufanya biashara za nafaka, uwakala wa fedha na vyakula vya mifugo.
3. Kuwatengenezea watu website na blogu.
4. Kuwapa watu huduma za matangazo ya mtandaoni.
5. Kuandika vitabu.
6. Kusoma vitabu na kuuza chambuzi.
7. Kufanya kilimo cha matunda.
8. Kufanya ufugaji wa kuku.
9. Kukochi.
10. Kutibu

Hayo ni baadhi ya yale niliyofanya kwenye miaka hiyo na yakaniingizia kipato.
Kuna mengine mengi nilijaribu hapo katikati lakini hayakuweza kuniingizia fedha.

Baada ya kufanya mambo hayo mengi kwa kipindi hicho, nimefika hatua ya kuachana na mengi na kuweka nguvu zangu zote kwenye mambo machache na muhimu ambayo yatakamilisha kusudi langu na kuniwezesha kufikia malengo makubwa niliyonayo.

Hivyo basi, kuanzia sasa kwenda mbele, nitafanya mambo matatu tu; KUSOMA, KUANDIKA na KUKOCHI.

Na hata kwenye hayo, bado pia nitapunguza upana wa kuyafanya.
Huko nyuma nilikuwa nikisoma na kuandika kwa upana kwenye eneo zima la maendeleo binafsi.
Hivyo nilisoma na kuandika kwenye maeneo kama;
1. Fedha na uwekezaji
2. Biashara na ujasiriamali
3. Malezi na Mahusiano
4. Afya na Ustawi
5. Ajira na kujiajiri
6. Uongozi na Usimamizi
7. Hamasa
8. Ushauri

Lakini kuanzia sasa kwenda mbele, nitasoma, kuandika na kukochi kwenye maeneo matatu tu;
1. FEDHA
2. BIASHARA
3. UWEKEZAJI

Ni vigumu sana kuacha mambo ambayo unaweza kuyafanya vizuri.
Lakini ili uwe bora kabisa, lazima uachane na hayo mazuri.
Hivyo nakwenda kuwa bora kabisa kwenye KUSOMA, KUANDIKA NA KUKOCHI kwenye FEDHA, BIASHARA NA UWEKEZAJI.
Hapo ndipo nimejipata, hapo ndipo nitayaishi maisha yangu yote yaliyobaki hapa duniani.

Nahitaji zaidi ushirikiano wako.

Ili niweze kuliishi kusudi langu na kuyafikia malengo makubwa niliyonayo, nahitaji sana ushirikiano wako wa karibu.

Ushirikiano wako nauhitaji kwenye ngazi tatu;

Ngazi ya kwanza ni uendelee kujifunza bure kabisa kwenye maeneo hayo ninayokwenda kujikita zaidi.
Hayo utajifunza kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA ambao utaendelea kuwa na makala bora kabisa za kukuwezesha uwe na maisha bora.
Makala za AMKA MTANZANIA utaendelea kuzipata kwenye mtandao; www.amkamtanzania.com na pia kutakuwa na channel maalumu ya mafunzo kwenye mtandao wa Telegram kwa anwani; www.t.me/amkamtanzania

Ngazi ya pili ni kuwa balozi wa Harakati kuu ninayoandaa sasa ya MTAALA WA UTAJIRI.
Hii ni harakati ya kuleta uelewa mkubwa wa kifedha kwa Watanzania wenzetu, ambao wengi wapo gizani inapokuja kwenye eneo la fedha.
Ushirikiano ninaouhitaji kwako hapa ni uwe sehemu ya harakati hii ili tuweze kuwafikia wengi zaidi.
Kwa sasa naandaa kitabu cha Mtaala Wa Utajiri, kitakapokamilika tutakuwa na harakati hiyo ya mapinduzi ya kifedha.
Tutaenda kuwa na klabu za #MtaalaWaUtajiri ili kuishi kwa uhalisia harakati hiyo kubwa.
Taarifa zaidi kuhusu harakati hiyo ya Mtaala Wa Utajiri zinapatikana kwenye mtandao; www.utajiri.tz na kwenye channel maalumu ya Telegram; www.t.me/utajiritz

Ngazi ya tatu huduma kuu ya Mafunzo na Ukocha ninayotoa ya CHUO CHA MAUZO na BILIONEA MAFUNZONI.
Hapa ndipo ninapokwenda kuweka nguvu zote ili kuwajenga mabilionea na mimi kuwa bilionea.
Hiyo ndiyo kanuni yangu kuu, nitakuwa bilionea kwa kujenga mabilionea wasiopungua 100.
Wale wanaokuwa kwenye huduma hii nawapambania hasa mpaka wafikie ubilionea, kwa sababu ni kwa wao kuwa mabilionea ndiyo na mimi nitakuwa bilionea.
Hiyo siyo safari rahisi, inataka mtu ujitoe hasa.
Hivyo hii siyo huduma ya wote, bali ya wachache ambao wanakidhi vigezo vilivyipo.
Kupata taarifa zaidi kwenye ngazi hii, ingia kwenye mtandao; www.mauzo.tz na channel maalumu ya Telegram; www.t.me/chuochamauzo

Rafiki, kanuni ninayofanyia kazi kuanzia sasa kwenda mbele ni hii;
1. Kuliishi kusudi; AMKA MTANZANIA.
2. Kufikia ubilionea; CHUO CHA MAUZO NA BILIONEA MAFUNZONI.
3. Kuwa raisi wa Tanzania; MTAALA WA MAUZO.
Hapo ndipo nitakapofia, nitakapopambania usiku na mchaka.

Ombi langu kwako ni tafuta mahali ambapo tutaweza kuendana pamoja na karibu twende pamoja.
Ninachokuahidi ni sitaishia njiani kwenye haya, nitayatimiza kwa uhakika au nitakufa nikiwa nayapambania.

Sijioni nikiwa na maisha mengine hapa duniani nje ya hapo.
Nitaendelea kuboresha mengi kadiri tunavyokwenda, lakini nitabaki huko huko.

Nikushukuru tena wewe rafiki yangu ambaye tunaendelea kuambatana pamoja.
Safari ndiyo kwanza imeanza, karibu sana tuendelee pamoja kwenye hii safari.

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini,
Mwanafalsafa ya Ustoa,
Mkuu wa Chuo Cha Mauzo,
Kocha Dr. Makirita Amani
amakirita@gmail.com
www.amkamtanzania.com / www.t.me/amkamtanzania
www.utajiri.tz / www.t.me/utajiritz
www.mauzo.tz / www.t.me/chuochamauzo