Barua ya V; Kuhusu Kuishi Kwa Falsafa Na Maisha Ya Mafanikio.

Rafiki yangu Mstoa,
Moja ya vitu vinavyofanya watu wengi wasiyafurahie maisha ni kutokuishi maisha halisi kwao.
Wengi wanaishi maisha ya kuiga na kuwaridhisha wengine.
Wengi sana wanaishi maisha ya maigizo kwa nje, huku ndani yao wakiwa tofauti kabisa.

Tumekuwa tukiona watu ambao wanajionyesha washika dini na wenye maadili wakija kuumbuka kwa maovu waliyokuwa wanafanya.
Na wanaojionyesha matajiri kwa nje wakija kuumbuka kwa madeni makubwa waliyonayo.
Wanaoonyesha furaha nje wakiwa na sonona ndani.
Mifano ni mingi na dhahiri.

Kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii, ndiyo hilo limezidi kuwa tatizo kubwa sana.
Kila mtu anaonekana kuwa na maisha mazuri na ya furaha huko mtandaoni.
Lakini inapokuja kwenye uhalisia, maisha ya wengi ni magumu, yenye taabu na msongo mkubwa.

Tatizo siyo maisha kuwa magumu au kuwa na changamoto, hayo yote ni sehemu ya maisha. Tatizo ni pale mtu anapoishi maisha ya kuigiza ili kuonyesha kwa nje kitu ambacho ni tofauti na ndani.
Ukichanganya changamoto za maisha na maigizo ambayo watu wanafanya, haishangazi kwa nini watu wengi sana wana msongo na sonona.

Hili la kuishi maisha ya kuigiza siyo geni, limekuwepo tangu enzi na enzi.
Mstoa Seneca kwenye barua yake ya tano kwa rafiki yake Lucilius, alizungumzia juu ya watu kuishi falsafa kwa maonyesho badala ya uhalisia.
Kuna mambo mengi ya kujifunza kwenye barua hiyo ambayo tukiyatumia tutaweza kuvuka hali ya maisha ya sasa ya kuishi kwa maigizo.

Karibu tujifunze jinsi ya kuishi falsafa na hata maisha kwa ujumla kwa uhalisia wake na siyo maigizo.

1. Kazana kuwa bora kila siku.

Seneca anasisitiza umuhimu wa kila mtu kuendelea kujifunza na kuwa bora kila siku. Anataka tufurahie ung’ang’anizi wa kuendelea kujifunza kila siku.
Ni wajibu wetu kujiendeleza na kuwa bora.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku kazana kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa siku iliyopita. Hiyo ndiyo njia pekee ya kujenga maisha bora.

Nukuu;
“You make it each day your endeavour to become a better man. I do not merely exhort you to keep at it; I actually beg you to do so.” – Seneca
“Kila siku weka juhudi kuwa mtu bora zaidi. Siyo tu nakuhimiza ufanye hivyo, ila nakuomba ufanye hivyo.” – Seneca

2. Usifanye kwa maonyesho.

Nia yako ya kukazana kuwa bora kila siku, itakosa maana kama utafanya hivyo kwa maonyesho.
Kama utafanya kwa sababu umeona wengine wanafanya, au utafanya ili uonekane unafanya, itapoteza maana nzima.
Watu huwa wanaenda mbali zaidi na kufanya mambo ambayo yanaleta mijadala kwenye jamii ili tu waonekane ni wa aina fulani.
Kwa mfano kuvaa kwa namna fulani, kuishi kwa namna fulani ya tofauti.
Pale unapokazana sana ili uonekane, unakosa maana ya kile unachofanya.

Hatua ya kuchukua;
Usifanye chochote kwa kuiga au ili kuonekana na wengine. Badala yake fanya kwa sababu ni muhimu kwako kwenye kuyaboresha maisha yako. Hilo litakupa utulivu mkubwa wa kufanya kwa tija.

Nukuu;
“I warn you, however, not to act after the fashion of those who desire to be conspicuous rather than to improve, by doing things which will rouse comment as regards your dress or general way of living.” – Seneca
“Nakuonya, usifanye kwa kuiga au kuonekana, bali fanya ili kuwa bora, usihangaike na mavazi au kuishi maisha ambayo yatafanya wengine wakuongelee.” – Seneca

3. Usitofautiane sana na wengine.

Hapa ndipo penye mtego mkubwa ambao wengi huwa wananasa pale wanapochukua hatua za kuyaboresha maisha yao.
Kwa sababu wanafanya mambo ya tofauti, basi hutaka kujitofautisha na wengine na kuonyesha hilo wazi.
Wengi huona kwa sababu wanafanya mambo ya tofauti, ambayo kwao ni bora basi wanapaswa kuyaonyesha kwa wengine, ili kupata sifa za juhudi zao. Lakini wanachoambulia ni chuki kutokana na jinsi walivyochagua kufanya.
Hapo ndipo Seneca anapotuambia kwa ndani tunaweza kuamua kuwa tofauti kadiri tunavyotaka, ila kwa nje tunapaswa kuendana na wengine.
Ni jambo linaloweza kutatiza, lakini litakusaidia sana kupunguza usumbufu usio na maana.

Hatua ya kuchukua;
Acha kuonyesha kwa wengine maboresho unayofanya kwenye maisha yako ambayo yanatofautiana na wao. Wengi hawatafurahishwa na kitendo cha wewe kuwa tofauti na wao na hivyo watakupinga kwa kila namna. Kwa nje onekana kama wao ila kwa ndani kuwa wewe.

Nukuu;
“Inwardly, we ought to be different in all respects, but our exterior should conform to society.” – Seneca
“Kwa ndani tunaweza kuwa tofauti kadiri tunavyotaka, ila kwa nje tunapaswa kuendana na wengine.” – Seneca

4. Tusifanye kwa kupitiliza.

Changamoto nyingine kubwa kwenye kuboresha maisha ni tabia ya watu kufanya kwa kupitiliza. Kila kitu kina kiasi chake cha kufanya. Ukienda zaidi ya kiasi hicho unaishia kuharibu kuliko kujenga, unapata maumivu badala ya furaha.
Ni tabia ya watu kupenda kupata matokeo makubwa na kwa haraka na hivyo kufanya mambo kwa kupitiliza.
Kwenye kuiishi falsafa na kuyaboresha maisha, kufanya kwa kupitiliza hakujengi bali kunabomoa, hakuwavutii watu kwako bali kunawafukuza.
Hivyo chochote unachofanya, fanya kwa kiasi na hilo litajenga matokeo mazuri.

Hatua ya kuchukua;
Zuia hali ya kutaka kufanya kwa kupitiliza ukidhani ndiyo njia ya kupata matokeo ya haraka. Utajichelewesha zaidi kwa kupitiliza kuliko kwa kufanya kwa kiasi.
Maboresho ya maisha yape muda, usiyaharakishe.

Nukuu;
“Our life should observe a happy medium between the ways of a sage and the ways of the world at large; all men should admire it, but they should understand it also.” – Seneca
“Maisha yetu yanapaswa kuwa kwenye wastani wa mambo ya kitakatifu na mambo ya kidunia; watu wote wanatakiwa kuyatamani, lakini pia wanatakiwa kuyaelewa.” – Seneca

5. Jinsi ya kuonyesha tofauti yako kwa wengine.

Mambo tunayojifunza hapa yanachanganya sana.
Kwa ndani tuwe vile tunavyotaka, lakini kwa nje tuwe kama wengine.
Sasa wengine watawezaje kujua sisi tupo tofauti ili nao wajifunze na kuwa bora?
Hapo ndipo Seneca anapotuambia kitu cha kufanya; tuyafanye maisha yetu kuwa bora kiasi cha watu kuja kwetu kutaka kujua siri ya hilo na wanapotusogelea karibu ndiyo tuwaonyeshe jinsi tulivyotofauti.
Kwa watu kutaka wenyewe kujua nini kinatupa matokeo ya tofauti na wakaona jinsi tulivyo tofauti, watashawishika zaidi na wao kubadilika.

Hatua ya kuchukua;
Usikazane kuwapigia watu kelele wawe tofauti, wewe kuwa na matokeo ya tofauti kwenye maisha yako, yatakayowafanya watu waje kwako kutaka kujua una siri gani na hapo ndipo utawaonyesha jinsi ulivyo tofauti. Wanaokuja wenyewe wana mapokeo tofauti na wale utakaowafuata wewe.

Nukuu;
“Well then, shall we act like other men? Shall there be no distinction between ourselves and the world?” Yes, a very great one; let men find that we are unlike the common herd, if they look closely. If they visit us at home, they should admire us, rather than our household appointments.” – Seneca
“Je tutaendelea kuwa kama wengine? Hakutakuwa na tofauti kati yetu na dunia? Ndiyo, tofauti itakuwepo kubwa; lakini wacha watu wajue tunatofautiana na wengine baada ya kutuangalia kwa karibu. Kama watatembelea nyumbani kwetu, watukubali sisi na siyo vitu tulivyonavyo.” – Seneca

6. Unachotumia kisikubadili.

Kwenye mabadiliko ya maisha, wapo watu wanaobadilishwa sana na vitu vya nje na kupoteza ile maana ya ndani.
Seneca anatuambia vitu vya nje havipaswi kuwa na usumbufu wowote kwetu.
Hivyo ni vitu tunavyopaswa kuvitumia na siyo kuruhusu vitutawale.

Hatua ya kuchukua;
Tumia vitu kwa matumizi yake, badala ya kuvipa nguvu ya kuvitawala. Hata kama una gari zuri, litumie kwa usafiri na siyo kwa kujionyesha kwamba una gari zuri.

Nukuu;
“He is a great man who uses earthenware dishes as if they were silver; but he is equally great who uses silver as if it were earthenware.” – Seneca
“Ni mtu mkuu yule anayetumia vyombo vya udongo kama vile ni vya fedha; lakini pia ni mkuu yule anayetumia vyombo vya fedha kama vile ni vyombo vya udongo.” – Seneca

7. Utajiri usikupagawishe.

Kitu kingine kikubwa tunachokiona kwenye maendeleo binafsi ni watu ambao wanaanzia chini kabisa, wanakuwa wanyenyekevu, wanajifunza, wanajita na kupiga hatua kubwa. Baada ya kupiga hatua wanabadilika na kuacha yale yote waliyofanya mpaka kufika hapo.
Matokeo yake wanapata anguko kubwa.
Huko ndiyo kupagawishwa na utajiri ambapo kumewapoteza watu wengi walioanzia chini na kupiga hatua.

Hatua ya kuchukua;
Usisahau ulipotoka na usisahau kilichokufikisha popote ulipofika. Mara zote endelea kuwa mnyenyekevu, ukijifunza na kuchukua hatua ili kuendelea kuwa bora. Siku ambayo utaona umeshajua kila kitu ndiyo siku ambayo utaanza kuanguka.

Nukuu;
“It is the sign of an unstable mind not to be able to endure riches.” – Seneca
“Ni ishara ya akili isiyo imara kushindwa kuhimili utajiri.” – Seneca

8. Hofu na matumaini vinakwenda pamoja.

Licha ya watu kupiga hatua kubwa, bado hofu imekuwa inawaandama. Hili limekuwa mzigo mkubwa kwa wengi kiasi cha kushindwa kuyafurahia maisha yao.
Seneca anaeleza ni hali ya kawaida kabisa kwa matumaini na hofu kwenda pamoja.
Na hilo linatokana na akili zetu kushindwa kukaa kwenye wakati uliopo, badala yake kuangalia tuliyoshindwa kwenye yaliyopita au kuangalia tusiyojua yanayokuja.
Tunaweza kuwa na matokeo mazuri sasa, lakini tukashindwa kuyafurahia kwa sababu tunaangalia yaliyopita na yanayo.
Seneca anafananisha matumaini na hofu kwa mfungwa na anayelinda mfungwa, ambao wote ni kama wapo kwenye pingu.
Pia anatuonyesha jinsi ambavyo wanyama wanatushinda kwenye hilo, mnyama akiwa kwenye hatari, atafanya kila namba aivuke hatari hiyo, na akishaivuka anaisahau. Ila sisi binadamu tunaendelea kuibeba hatari hata baada ya kuwa tumeshaivuka.

Hatua ya kuchukua;
Weka fikra zako kwenye wakati uliopo na furahia yale unayopitia sasa.
Usijutie ya nyuma, yameshapita na huwezi kuyabadili.
Usihofie yajayo, bado hujayafikia hivyo huwezi kuyaathiri.
Angalia uliyonayo sasa na uyafurahie.

Nukuu;
“Many of our blessings bring bane to us; for memory recalls the tortures of fear, while foresight anticipates them. The present alone can make no man wretched.” – Seneca
“Baraka zetu nyingi huwa zinaishia kuwa laana kwetu, kwa sababu kumbukumbu zinaturudisha kwenye mateso ya hofu za nyuma, wakati utabiri wetu ukitegemea mateso ya hofu zijazo. Ni wakati uliopo pekee ndiyo unaoweza kumzuia mtu asiteseke.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, tumejifunza mengi hapa kuhusu kuishi maisha ya kifalsafa na kupiga hatua kwenye maisha bila ya maonyesho kwa wengine wala kuathiriwa na hofu.
Kama jinsi ambavyo falsafa ya Ustoa ilivyo ya vitendo, tutanufaika na haya kama tutayaweka kwenye vitendo.
Twende tukayaishi haya ili tuweze kuwa na maisha ya mafanikio na tunayoyafurahia.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.