Mwanafalsafa Socrates aliwahi kunukuliwa akisema, maisha ambayo hayatathiminiwi ni maisha ambayo hayana maana kuishi.
Kwa msingi huo basi, tunatakiwa kufanya tathmini zetu kujua siku zetu zimekwendaje, unapoamka asubuhi na kuanza siku yako ni kama vile umepanda na jioni ni muda wa kuvuna kile ulichopanda na kuvuna ni kupitia siku yako yote kuanzia ulivyoamka mpaka pale unapotaka kulala tena.
Hatuwezi kujua kama tunaenda mbele au tunarudi nyuma. Na kumbuka, kwenye maisha hakuna kusimama, ni aidha uwe unaenda mbele au unarudi nyuma.
Kila siku tunayoishi ni nafasi nzuri kwetu kuwa bora zaidi, kwa sababu kuna mengi tunakutana nayo ya kujifunza, kuna makosa tunayoyafanya na yapo mazuri pia mazuri tunayoyafanya.
Watu wengi wamekuwa wanakosa nafasi ya kuzitumia siku zao kuwa bora zaidi kwa sababu hawapati muda wa kutafakari kila siku yao.
Kupitia falsafa ya ustoa, tunashauriwa kuipima na kutafakari kila siku yetu kabla ya kulala.
Kupitia kufanya tathmini, tunapata nafasi ya kujifunza na kujiandaa kuwa bora zaidi kwenye siku inayofuata.
Inapofika jioni, unapoimaliza siku yako, usikimbilie tu kulala na kuona siku imeisha badala yake unahitaji kuwa na tahajudi ambayo utaipitia siku yako yote.
Mwanafalsafa Epictetus kwenye moja ya kauli zake anasema “Allow not sleep to close your wearied eyes, Until you have reckoned up each daytime deed: “Where did I go wrong? What did I do? And what duty’s left undone?” From first to last review your acts and then Reprove yourself for wretched [or cowardly] acts, but rejoice in those done well.”
Akiwa na maana kwamba usikubali usingizi ufumbe macho yako kabla hujahesabu kila tendo ulilofanya kwenye siku yako. kipi umekosea, kipi umefanya vizuri na kipi ambacho hujakamilisha. Kuanzia tendo la kwanza mpaka la mwisho, jikaripie kwa yale uliyofanya vibaya na jisifie kwa yale uliyofanya vizuri
Kwenye tahajudi hii, pitia siku yako nzima, kwa kufikiria kila ulichofanya kwenye siku yako, kila uliyekutana naye na mawazo na hisia ulizokuwa nazo siku nzima.
Kisha jiulize na kujijibu maswali haya matatu;
Moja; vitu gani umefanya vibaya? Katika yale uliyofanya kwa siku nzima, je vitu gani umefanya kwa ubaya au kwa njia ambazo siyo sahihi?
Mbili; vitu gani umefanya vizuri? Katika vitu vyote ulivyofanya kwa siku nzima, vipi ambavyo umevifanya kwa uzuri, ni kwa namna gani umeishi misingi na tabia za ustoa?
Tatu; Vitu gani utakwenda kufanya tofauti? Ni vitu gani unahitaji kuvifanya kwa utofauti ili kuweza kuishi kulingana na msingi na tabia za ustoa?
Kwa kujiuliza na kujipa majibu ya maswali hayo matatu, utaweza kujipima kwa kila siku yako, na pia kujiandaa vema kwa siku inayofuata.
Pia utaepuka kurudia makosa uliyofanya kwa siku husika.
Kutoka kwa Rafiki na Mwanafalsafa mwenzako wa Ustoa,
Mwl Deogratius Kessy
Asante sana kwa tafakari hii..
Imekuwa siku Bora Sana kwangu japo majukumu yalinizidia lkn ninayo nafasi Tena kesho ya kuwa Bora zaidi.
LikeLike
Vitu gani nimekamilisha.?
Vitugani nimefanya vizuri?
Vitu gani nimefanya vibaya?
Nini nitafanya ili kufanya vizuri?
LikeLike
Hili ni muhimu sana na wengi hatufanyi kwa usahihi ikifika jioni au usiku tunalala bila kutafakafi siku na pia kuona nini tufanye kesho kwa ubora kuliko leo tukibadili tabia zetu hizi tunaweza kuwa bora sana
LikeLike